IMAMU wa msikiti wa Maziwa Ngo’mbe Kisiwani Pemba, Omar Hussen Said (42) amepigwa na kujeruhiwa jicho baada ya kutokea vurugu ndani ya msikiti wakati wa ibada ya Ijumaa Juni 7 mwaka, imefahamika jana.
Vurugu hizo zimesababishwa na baadhi ya waumini wa msikiti huo ambao wanapinga Imamu Said kuendelea kushika wadhifa huo kutokana na kitendo chake cha kujivua uanachama wa CUF na kujiunga na chama tawala CCM mwaka huu.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Kamishina Msaidizi (ACP) Mohammed Shakani, amethibitisha kutokea kwa vurugu hizo na watu watatu wamekamatwa kwa tuhuma za kuhusika na shambulio dhidi ya kiongozi wa dini Zanzibar.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni, Mfaki Ali Juma, Faki Ngome Juma na Abdallah Masoud, wote wakaazi wa Maziwa Ngo’mbe Wilaya ya Micheweni.
ACP Shakani, alisema kwamba Jeshi la Polisi linamsaka Mbwana Haji Mbwana ambaye ametoroka kwa kukimbilia kisiwani Unguja muda mfupi badaa ya tukio hilo.
“Watuhumiwa watafukishwa Mahakamani Jumatatu wakati Jeshi la Polisi tukiendelea kumsaka Mbwana Haji Mbwana ambaye ametorokea Unguja,’alisema ACP Shakani.
Aidha alisema kwamba tangu imamu Said kuamua kujivua uanachama wa chama cha wananchi CUF na kujiunga na CCM kumeibuka kikundi cha waumini ambao wanapinga kuendelea kuwa imamu wao kutokana kutokana na kitendo hicho.
Akifafanua kuhusu vurugu hizo, alisema kwamba wakati Imamu Said, akitoa mawadha ya Ijumaa katika membari ya msikiti alivamiwa na kuanza kupigwa na kujeruhiwa jicho la kushoto na kutibiwa katika hospitali ya Micheweni kisiwani Pemba.
Hata hivyo alisemas kwamba vurugu hizo zilidhibitiwa na haraka kwa kutumia mtandao wa askari kanzu waliokuwa wameimarisha ulinzi katika misikiti mbali mbali wakati wa ibada ya Ijumaa.
Alisema kwamba watu wanao tuhumiwa kuhusika na vurugu hizo wamekamatwa na kufunguliwa mashitaka katika kituo cha Polisi Micheweni.
Alisema kwamba Imamu Said anaendelea vizuri baada ya kupata tiba katika hospitali ya Micheweni wakati polisi inaendelea kumsaka mtuhumiwa mmoja.
ACP Shakani amewataka wananchi Kisiwani Pemba kujiepusha na vitendo vya kuchukua sheria mkononi kwa vile vinakwenda kinyume na misingi ya utawala wa sheria.
Imamu Said ni kati ya wanachama 30 wa Chama cha wananchi CUF walioamua kukihama chama cha wananchi CUF na kujiunga na CCM na walipokelewa Rais wa Zanzibar na Makamu Mwenyekiti wa CCM DK Ali Mohamed Shein Mey mwaka huu.
Pamoja na sheria Namba 5 ya vyama vya siasa ya Mwaka 1992 kukataza nyumba za ibada kutumika kwa shughuli za kisiasa bado tatizo hilo limendelea kujitokeza na kuathiri viongozi wa dini ikiwemo kupigwa risasi na kumwagiwa tindikali visiwani Zanzibar.
Hata hivyo Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Dadi Faki Dadi, amewataka wananchi Mkoa humo kujiepusha na vitendo vya vurugu ikiwemo kuchukua sheria mkononi.
Source: Nipashe
No comments:
Post a Comment