MBUNGE
wa Kondoa Kusini, Juma Nkamia (CCM), kwa mara nyingine ameingia katika
kashfa nzito akituhumiwa kutaka kumpiga Mbunge wa Viti Maalumu CUF,
Moza Abeid ndani ya Ukumbi wa Bunge.
Tukio hilo lilitokea mwanzoni
mwa wiki ambapo imeelezwa kuwa Nkamia mbali na kutaka kumpiga mbunge
huyo, pia alimtolea matusi mazito ya nguoni..
Kwa mara ya kwanza
mbunge huyo aliingia katika kashfa baada ya kutoa kauli bungeni kuwa
hazungumzi na mbwa, bali anazungumza na mwenye mbwa kabla ya kuingia
katika mzozo na wahariri na baraza la habari aliposema kuwa Jukwaa la
Wahariri na Baraza la Habari ni NGOs za kutafuta fedha.
Uchunguzi
wetu ambao umethibitishwa na Nkamia mwenyewe umebaini kuwa
chanzo cha tukio hilo ni kutokana na kuzomewa kwa Nkamia katika kampeni
za uchaguzi mdogo Kata ya Dalai Wilaya ya Chemba.
Kwa mujibu wa
wabunge mashuhuda ambao waliliona tukio hilo, ilielezwa kuwa Nkamia,
ambaye pia ni mwandishi wa habari, alianza kumshushia matusi Moza
wakiwa ndani ya Bunge hadi walipotoka nje alimfuata na kutaka kumpiga.
“Kweli
pale jamaa yetu, alitia aibu, hata hivyo kusema kuwa alikuwa amelewa
siyo kweli maana mimi namfahamu Nkamia vizuri ila ilikuwa ni hasira
tu,” alisema mmoja wa wabunge walioamua ugomvi huo.
Akizungumzia
tukio hilo Moza, alisema kuwa wakati akitoka nje ya ukumbi, alipita
karibu na kiti anachokaa Nkamia na ghafla akaitwa, lakini akashangazwa
na kitendo cha kuanza kurushiwa matusi.
“Kweli
Nkamia na mimi tunatoka wilaya moja, lakini siku ile nilishangaa
alinitukana matusi ya nguoni kabisa ……… (anayataja), lakini mimi kule
sikusema kitu hadi nilipotoka nje alinifuata na mimi hasira ilinishika
nikaanza kumjibu akatupa vitabu ili aje anipige wabunge wenzake
wakamkamata,” alisema Moza.
Alisema
kuwa chanzo cha matusi hayo ilikuwa ni tuhuma kwamba Nkamia alimtuhumu
Moza kuwa aliandaa vijana katika Kata ya Dalai wakati wa kampeni za
uchaguzi wa udiwani ili wamtukane.
“Hata
hivyo, waliomwambia hivyo kwamba niliandaa vijana au nilimtukana
walimdanganya kwani mimi wakati huo nilikuwa bungeni, lakini yeye ndiye
aliyeniporomoshea matusi katika kampeni hizo na ushahidi wa sauti
ninao,” alisisitiza Moza.
Kwa
upande wake Nkamia, ambaye kabla ya kuwa mbunge alikuwa mtumishi wa
Serikali katika Shirika la Tanzania Broadcasting Corporation (TBC)
alikiri kutokea kwa tukio hilo, lakini alikanusha kuingia bungeni akiwa
amelewa kama ilivyoaminika na watu.
Nkamia alitoa sababu za ugomvi huo
kuwa ni kutokana na taarifa kuwa Moza aliandaa kikosi cha vijana wahuni
kulishambulia gari la Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na kuwazomea
viongozi wake akiwemo yeye.
“Ile
ilikuwa ni hali ya kawaida kwa binadamu kupatwa na hasira unapoambiwa
kitu kama hicho, lakini sina shida na mbunge Moza na wala sioni kama
hilo ni tukio kubwa kiasi cha kuandikwa,” alisema Nkamia
mwananchi
mwananchi
No comments:
Post a Comment