Monday, 8 July 2013

MWANAFUNZI WA CHUO CHA VETA MKOANI DODOMA AJILIPUA KWA PETROL.....KISA NI WIVU WA MAPENZI


MWANAFUNZI wa Chuo cha Ufundi (VETA), mkoani Dodoma, Taliki Juma (22), amefariki dunia baada ya kujilipua kwa mafuta ya petroli. Mbali na mwanafunzi huyo kufariki, watu wengine wanane waliokuwa karibu na moto huo nao walijeruhiwa vibaya.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma na kusainiwa na Kamanda wa Polisi wa mkoa, David Misime, tukio hilo lilitokea juzi saa 12.30 jioni katika Kitongoji cha Machaka, Kata ya Nzughuni.

Kamanda Misime alisema, katika tukio hilo marehemu alinunua mafuta ya petroli lita tano katika kituo cha mafuta cha Nanenane na kisha kujilipua.

“Juma ambaye ni mwanafunzi wa fani ya ufundi wa magari, alimwaga petroli hiyo ndani ya saluni ya Irene Mapunda na kujilipua.

“Watu waliokuwa karibu naye walijaribu kumsihi asijilipue lakini hawakufanikiwa, kwani aliwasha kibiriti ndani ya saluni hiyo na kusababisha moto mkubwa kulipuka ambao uliwaunguza wengine waliokuwa karibu naye pamoja na mali zote zilizokuwa ndani ya Saluni hiyo.

“Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa chanzo cha tukio hilo ni wivu wa kimapenzi, hata hivyo Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma linaendelea na uchunguzi wa kina juu ya tukio hili,” ilieleza taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo waliojeruhiwa ni Mugina Hessein (32), Benson Mushi (11) Japhet Japhet (18), Meshack John (18), Swaibu Kassim (20),Ester Silau (30), Shaban Pili (20) na Fedrick Gabriel (21).

Majeruhi wote wamelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma (General) na tathimini ya hasara iliyosababishwa na moto huo bado haijafahamika.

No comments:

Post a Comment