Kwenye
Saluni nyingi za wanawake, mazungumzo mengi yanahusu maisha ya watu na
hasa kuhusu mapenzi na kipato, kashfa na saikolojia zisizo rasmi kuhusu
ndoa na uhusiano. Kuna mazungumzao ya kukatishana tamaa na kuumizana
zaidi, kwa sababu kila mmoja anajaribu kuonyesha kwamba ana nafuu
fulani.
Lakini
mbaya zaidi ni kwamba, saluni za wanawake hutumiwa na wanawake hao kama
maeneo ya kusemea hisia zao chungu na kutoa jumuisho kuhusu wanaume na
uhusiano. Huko saluni hakuna wataalamu, bali kuna wazungumzaji ambao
wanaamini wao ni wataalamu, na wengine kwa sababu ya kuzidiwa na mzigo
wa matatizo hasa ya uhusiano na pengine ya kipato, huwaaamini hao
wataalamu wasio rasmi.
Huko
saluni ndiko ambako wanawake wanaambiana`kwamba, mwanaume akiacha
kufanya tendo la ndoa kwa wiki moja na mpenzi wake, ni lazima mwanaume
huyo atakuwa na ‘nyumba ndogo.’ Ndiko ambako wanafundishana kwamba,
ukipata Mganga wa nguvu unaweza kumshika mwanaume. Ndiko huko ambako
hutajwa orodha ya wanawake ambao wamewashika waume zao kupitia kwa
waganga. Ndiko huko ambako majina ya waganga maarufu hutajwa.
Lakini ndiko huko saluni ambako, wanawake hutaja orodha ya wanawake
wenzao waliopata mali kupitia ‘mabuzi,’ ambao huwapa mitaji ya biashara
inayowawezesha kusafiri hadi Uchina. Pia hutajwa majina ya wanaume
wanaohonga sana. Ni saluni ambako wataalamu wasio rasmi hutoa suluhu ya
matatizo ya ndoa. Ndiko ambako wataalamu hao huwaambia wanawake wenzao
kwamba, ukimuonyesha mwanaume kwamba unampenda sana, atakudharau na
kukuacha.
Kwa hiyo mwanamke akitoka saluni anakuwa ametoka shule anayoiamini .
ambapo huacha kumwonesha mumewe kwamba, anampenda. Ni wazi shule hii ya
saluni haijui kwamba, unapoonesha kutokupenda, nawe utaoneshwa
kutokupendwa. Kwani unachopanda ndicho unachovuna. Wakati mwingine shule
hii inajua jambo hilo, isipokuwa inataka waliopotea na kuharibikiwa
wawe wengi.
Ni huko saluni ambako utasikia wanawake wakifundishana namna ya
kuwadanganya wanaume zao. Hufundishana namna ya kujenga nyumba bila
kunaswa na mume, kwani wanaume hawaaminiki, huwezi kuacha kujiandaa.
Lakini shule hii haijui kuwa, hiyo ni sumu kubwa kuliko sumu nyingine
kwenye ndoa, kutafuta mali na kujenga msingi wa kipato kwa siri.
Ni hukohuko saluni ambako wanawake huambiana uongo kuhusu wakwe, watoto
wa kambo, na mawifi. Hufundishana kwamba, kumpenda mama mkwe au wifi ama
mtoto wa kambo ni kutafuta muhali. Haiishia hapo huendelea kufundishana
hata namna ya kuwachukia watu hao.
Mwanaume, kama
ukiona mwenzi wako anakwenda saluni na akitoka huko amekuwa mtu mwingine
kabisa, unapaswa kujua kwamba, huenda amepata ‘dozi’ ya wataalamu hao.
Wanawake, nawashauri jihadharini sana na maneno ya saluni. Kwani katika kila maneno mia moja, ni moja tu linalokaribia ukweli. Kumbuka, linalokaribia ukweli . siyo kuwa ni la kweli……
No comments:
Post a Comment