Hata kama yuko mbali, muamini, usimsaliti mtadumu!
Nina uhakika baadhi yetu tuna wapenzi ambao wako mbali, hilo lisikupe
shaka. Bado unaweza kuendelea kuliboresha penzi lako na mwisho kutimiza
ndoto zenu mlizojiwekea za aidha kuoana kwa wale ambao bado wapo wapo
au kudumisha ndoa yenu kwa ninyi mliooana.
Katika hili kuna mambo mawili ya msingi ambayo leo nataka
kuyazungumzia ili kuhakikisha uhusiano wenu hautetereki.
Kwanza, hakikisha humsaliti mpenzi wako. Ukitaka kufurahia mapenzi,
lazima usiwe msaliti. Upo msemo usemao, ukimsaliti mpenzi wako ujue
nawe utasalitiwa, sasa ili uepukane na hilo ni vyema ukajiwekea dhana
ya uaminifu wewe kama wewe kwanza.
Jisemee mwenyewe; “Kwa nini nimsaliti mpenzi wangu? Nampenda sana na
najua nikimsaliti hatajua, lakini na yeye akinisaliti je?” Tafakari
maneno hayo kwa makini sana, naamini kuna kitu utajifunza.
Jichunge mwenyewe, usikubali kabisa kuharibu thamani yako kwa kumruhusu
mtu mwingine aujue mwili wako kwa kuwa tu umesikia ‘hamu’.
Kumbuka mwili wako ni kwa ajili ya mpenzi wako pekee, endelea na dhana hiyo siku zote utakazokuwa mbali naye, naamini utafurahi!
Kwa kufanya hivyo, hutaona faida yake kwa haraka lakini fikiria hili
kwa makini, kama wewe umeamua kuwa mwaminifu kwa mwenzi wako kwa
kutambua thamani yake, kwa nini Mungu asikulindie huko alipo? Ila
lazima ufahamu jambo moja, Mungu anaweza kukulindia mwenzi wako ikiwa
naye anakupenda kwa dhati na ana nia ya kuishi na wewe hapo baadaye.
Jambo lingine la msingi ni kujenga uaminifu kwake. Baada ya kuhakikisha
kwamba humsaliti, sasa ni wakati wako wa kuhakikisha unamwamini katika
kiwango cha mwisho. Usimwoneshe mashaka sana na nyendo zake. Wakati
mwingine unaweza kumpigia simu asipokee, hilo lisikuchanganye.
Kuna baadhi ya watu, akimpigia simu mpenzi wake akiona hajapokea,
tayari hisia zake zinakuwa mbali na muda huo huo anamwandikia meseji
mbaya za ukali na kumtuhumu kwamba anajua huko aliko anamsaliti! Huna
haja ya kufanya hivyo, onyesha kumwamini.
Kama umempigia na simu yake haipatikani, ni wakati wako wa kumwandikia
meseji ya kumpa pole kwa kazi kutokana na kutambua kwako kwamba muda
huo alikuwa bize.
Mwandikie hivi; “Natambua ni majukumu mengi uliyonayo muda huu ndiyo
yaliyosababisha ushindwe kupokea simu yangu, usijali kwa hilo. Nakupenda
sana na natambua kwamba mimi ndiye mwenye jukumu la kuhakikisha nakuwa
karibu na wewe kwa kila kitu, nakupenda mpenzi wangu, kazi njema.”
Ujumbe huo utamfurahisha, kama alikuwa na nia ya kukusaliti, hawezi
kufanya hivyo kwani atakuwa anajua anamsaliti mwenzi ambaye anamwamini
katika kiwango cha mwisho.
Kumuamini kwako kutamfanya aone ni jinsi gani ambavyo wewe mwenyewe
unavyojiamini na usivyo na wazo la kumsaliti! Kwa nini yeye akufanyie
hivyo? Lazima atabadilisha wazo lake.
Mpenzi msomaji wangu, hayo ni mambo mawili ya msingi ambayo unatakiwa
kuyazingatia pale unapokuwa mbali na mpenzi wako. Kumbuka kuwa mbali na
huyo uliyetokea kumpenda haiwezi kuwa sababu ya nyie kutengana.
Mtatengana tu endapo hakuna mapenzi ya dhati kati yenu lakini kama
mmependana kiukweli kutoka mioyoni mwenu, hata muwe mbali kwa muda
mrefu kiasi gani, bado hakuna cha kuliua penzi lenu.
No comments:
Post a Comment