Thursday, 10 October 2013

MWANAMKE ULIYENAYE SASA ANAKUPENDA AU ANAKUCHUNA???????

RAFIKI zangu, wiki mbili zilizopita nilikuwa nachambua mada inayohusu namna ya kugundua hisia za ndani za mwanaume.

Ni mada ambayo iliwafumbua wanawake kuwajua waume zao sawasawa. Kwamba wapo kwenye uhusiano hai au wenye mashaka.

Ilikuwa na changamoto nyingi sana, baadhi ya wasomaji waliwasiliana nami na kueleza maoni yao. Wanaume walisema wameonewa kuchambuliwa peke yao, wakaomba mada ya kuwachambua wanawake. Kilio hicho kimesikika na hii hapa ni mada itakayokupa njia rahisi za kugundua kwamba mwanamke uliyenaye ana mapenzi ya kweli au ana mambo yake!

Unajua wakati mwingine unaweza kuwa katika uhusiano na mwanamke ambaye ndani ya nafsi yake hana mapenzi kabisa lakini anajifanya anakupenda sana, kumbe ana nia yake anayoijua.

Kuna wanawake wazuri sana, ambao ukiwa nao kwenye uhusiano unajiona ulivyo mkamilifu na mwenye kujiamini hata mbele ya watu wanaokuzunguka.

Tatizo ni kwenye moyo wake, hana mapenzi, hana nia na wewe, hakuwazii wala hafikirii chochote kuhusu maisha yenu ya baadaye.

Wakati hayo yakiwa akilini mwake, wewe unamhesabia kama mwanamke sahihi kwako, mwanamke wa maisha yako ya baadaye, unayempenda kwa kila hali lakini hakupendi. Na kama kweli unampenda kwa dhati ndiyo kabisa huwezi kujua kama hakupendi kwa sababu wewe utakachokuwa unajua ni mapenzi tu.

Hata hivyo, si rahisi kuficha kila kitu, zipo tabia ambazo anaweza kuzionesha kwako lakini kwakuwa unampenda, usigundue kuwa zinadhihirisha jinsi asivyo na mapenzi.

Zipo nyingi sana lakini hapa nitakupa dalili kumi ambazo ukiona mwanamke wako anakufanyia, ujue hana penzi la moyoni.

Anateka hisia zako...
Mwanamke ana haki ya kudeka kwa mwanaume wake lakini siyo kwa nia nyingine yoyote zaidi ya kunakshi penzi. Huyu hana nia hiyo, anadeka kwa ajili ya kukupagawisha kimahaba ili aweze kuzishika hisia zako sawasawa.

Mchunguze vizuri, utagundua kwamba hata sauti yake anayoitumia kuzungumza na wewe siyo anayotumia akiwa na shoga zake. Anailegeza sana na kuiremba kwa kila hali.
Anataka kukupagawisha.

Hiyo ndiyo nia yake, kukupagawisha sana maana yake hutapindua na hutakuwa na wazo la kuwa na mwanamke mwingine zaidi yake.

Fedha mbele!
Ni kawaida mwanamke kumuomba fedha mpenzi wake lakini huyu asiye na mapenzi ya kweli, huwaza fedha mara zote. Hata kama utazungumza kuhusu kutoka naye ‘out’, bado ataulizia kuhusu dau lake. Ana mahitaji mengi, mara rasta, nguo mpya zimeingia, vocha na hata mahitaji mengine ambayo kimsingi hayakuhusu.

Mwanamke wa aina hii, ukitoka naye nje ya mji au kulala naye hotelini, asubuhi atataka chake! Jiulize ni mpenzi wako au anajiuza? Mbaya zaidi, hata kama utakuwa mgonjwa na amekuja kukutazama siyo ajabu kumsikia akisema: “Baby kama simu yako ina ‘balance’ naomba unipunguzie kidogo.” Kaka unaibiwa, hakuna mtu hapo!

Hakuheshimu
Kwakuwa hakupendi na wala hafikirii kuwa na wewe katika ndoa, sifa za uanamke hatakuwa nazo. Inawezekana kabisa anazifahamu vizuri lakini hana muda nazo.

Hasikii ukimwambia kitu, mjeuri na wala haheshimu kauli zako. Kama mpenzi wako, ambaye una malengo naye ya baadaye, una haki ya kumzuia aina fulani ya mavazi, kampani au tabia ambazo huzipendi, kwa mwanamke wa aina hii, kumwambia ni sawa umemruhusu!  Mwanamke huyu, neno heshima ni msamiati mgumu sana kwake.

Mkali wa mapenzi
Ujanja katika kunogesha penzi, wapenzi wanapokuwa faragha unakubalika kunakshi penzi lakini kwa mwanamke ambaye amekufanya kitega uchumi ni mkali zaidi upande huu. Anaweza akakosa sifa zote lakini akawa anakupeleka puta kwenye sita kwa sita! Anafanya haya kwa sababu ndiyo silaha yake ya mwisho.

Hata hivyo, siyo kila mwanamke mwenye uwezo mkubwa faragha anaweza kuwa tapeli wa mapenzi lakini wengi wao huwa wanawapagawisha wapenzi wao wakitaka kuwaza kuwaacha, wahofie kukosa mapenzi.

Msiri
Ni mpenzi wako lakini ni msiri kuliko kawaida, ni msiri wa mambo yake lakini pia hataki uhusiano wenu ujulikane. Hata kama utamwambia unataka kujulikana na ndugu zake, hatakubali. Anasingizia bado ni mapema wewe kwenda kwao.

Ni lini mwanamke akakataa mwanaume mwenye msimamo asijitambulishe kwao? Hata kama unampenda sana lakini unapoona alama hii lazima uwe makini. Huenda alishapeleka msururu wa wanaume au tayari yupo au hakupendi tu! Umeona eeh!

Hukidhi viwango!
Hapa mwanamke wa aina hii hashindwi kukuonyesha dalili kwamba wewe siyo chaguo lake. Mwanamke huyu ni mjanja sana na mwenye akili nyingi. Anapanga mipango yake taratibu, anaifanyia mazoezi kabla ya kuonesha wazi.

Hapa atakuonesha kwamba huna viwango hasa vya kuwa naye, anaweza akamuona mwanaume fulani kwenye filamu, gazeti au jarida akamsifia. Hata kama mmetoka pamoja, anaweza kumsifia mwanaume mwingine aliyepita karibu yenu.

Siyo ajabu kumsikia akisema: “Ah! Napenda sana wanaume warefu, yaani huyu kaka mh...” Kama anasema maneno haya na wewe ni mfupi, maana yake huna sifa za kuwa naye na anachokifanya ni kukuonesha kuwa yupo na wewe kwa muda na wala hutakiwi kufikiria mipango ya baadaye.

Hashindwi kumsifia mwanaume ambaye ana rasta au ameweka nywele ‘wave’ wakati wewe huna. Anafanya mambo haya ikiwa ni alama kwamba, hafikirii kuwa na wewe katika maisha yake badala yake anakula ‘good time’ tu!Ni hayo tu

No comments:

Post a Comment