Wednesday 4 December 2013

AIBU:SAKATA LA MCHUNGAJI MWINGIRA KUZAA NA MKE WAMTU LACHUKUA SURA MPYA..!! MLALAMIKAJI ADAI FIDIA YA SHILINGI BILIONI 7.5 ZA KITANZANIA..!!

LILE sakata la Nabii na Mtume Josephat Mwingira kudaiwa kuzaa na mke wa mtu Dk. Phills Nyambi limeendelea kupamba moto, mlalamikaji Dk. Morris William, raia wa Liberia amefungua kesi Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, akidai fidia ya shilingi bilioni 7.5.
 
Mtume na Nabii Josephat Mwingira.
Katika kesi hiyo iliyofunguliwa na Dk. William, anayewakilishwa na Wakili Desidery Ndibalema amemshitaki Mwingira kama mlalamikiwa namba moja na mke wa mlalamikaji, Dk. Philis Nyimbi ni mshtakiwa wa pili.
Tayari shauri hilo lililopelekwa mahakamni Novemba 21, mwaka huu na kupewa usajili namba 306 la 2013 limepangwa kutajwa Desemba 12, mwaka huu na hakimu atakayelisikiliza ni Hakimu Mkazi Hellen Riwa.
 Chanzo chetu ndani ya Mahakama ya Kisutu, kimesema kuwa katika nyaraka za mashtaka (nakala tunazo) zilizowasilishwa mahakamani hapo,  Dk. William amedai kuwa katika  tarehe ambayo haijulikani Mwingira aliingia katika uhusiano wa kimapenzi na mkewe.
Dk. Philis Nyimbi anayedaiwa kuzaa na Nabii Mwingira.
Nyaraka hizo zinaeleza kuwa baada ya mlalamika kugundua kuhusu hilo, alimuuliza mkewe ambaye alijitetea kwamba alibakwa.
Zinaeleza kuwa uhusiano huo haukuishia katika kupewa mimba tu bali pia mke wake kupata changamoto nyingine za kiafya ambazo hata hivyo hakuzitaja.
 HOJA YA WAKILI WA MLALAMIKAJI
Katika nyaraka hizo, Wakili Ndibalema alisema kuwa mteja wake baada ya kubaini kwamba mkewe amezaa na Mwingira, vilevile amepata changamoto za kiafya, aliamua kutoa ripoti Kituo cha Polisi Kati, Kibaha, Pwani.
“Polisi walimjibu mteja wangu kuwa hiyo ni kesi ya madai, siyo jinai, wakamshauri afungue madai mahakamani,” anaeleza Ndibalema kwenye hati hiyo ya mashtaka.

Mtoto wa Nabii Mwingira aliyezaa na Dk. Philis.
Anaendelea kusema, mtoto ambaye Mwingira analalamikiwa kuzaa na Dk. Philis ana umri wa miaka mitano hivi sasa.
Wakili Ndibalema anaeleza: “Uhusiano huo wa kimapenzi, umesababisha usaliti katika ndoa ya halali ya mteja wangu, imemsababishia kukata tamaa ya maisha na kuathirika kisaikolojia.
 “Uwezo wa utendaji kazi wa mteja wangu umeshuka kwa kiwango kikubwa, anaongoza taasisi isiyo ya kiserikali ya kimataifa ambayo sasa imekosa udhamini kutoka kwa mtu mmoja mmoja au vikundi vya taasisi mbalimbali duniani.
“Kwa hatua hiyo, mteja wangu amevunjiwa heshima na kushushwa hadhi yake siyo Tanzania tu bali duniani kote.”
 
ANACHOHITAJI DK. WILLIAM KWA MWINGIRA
Katika maelezo yake, Dk. William anaomba kupitia kwa wakili wake kwamba mahakama iamuru yeye, Dk. Philis na Mwingira, wakapimwe Ukimwi na mtoto afanyiwe uchunguzi wa DNA.
Dk. William   pia amedai kuwa ana vifaa vya hospitali vyenye thamani ya dola za Kimarekani 6,500,000 (zaidi ya shilingi bilioni 10), ambavyo Mwingira amevichukua baada ya kula njama na Dk. Philis.
 
ANAOMBA ALIPWE SHILINGI BILIONI 7.5
Katika hoja hiyo, Dk. William anaomba kwanza arudishiwe vifaa vyake ambavyo amedai Mwingira na Dk. Philis kuvitaifisha na baada ya kurejeshewa, alipwe fidia ya shilingi bilioni 7.5.
Dk.  William ametoa hoja ya kwa nini alipwe kiasi hicho kwamba; yeye ni mtaalamu wa kimataifa wa afya ambaye amewahi kutambuliwa na Ikulu ya Marekani (White House) chini ya marais Bill Clinton na George Bush.
 Taasisi yake iitwayo Global 2000(2010) International ambayo imejikita Texas, Marekani ilitambuliwa na Umoja wa Mataifa na alibuni vifaa mbalimbali vya matumizi katika sekta ya afya na magari nchini Marekani ambavyo thamani yake ni dola za Kimarekani 100,000,000 (zaidi ya shilingi bilioni 160). Alikuwa na mpango kwa kushirikiana na mkewe  kujenga kituo cha utafiti cha afya na hoteli ya nyota tano mkoani Kilimanjaro na alinunua hekari 37 kwa ajili hiyo, hata hivyo, mkewe alimpa Mwingira zawadi.
Alichaguliwa kuwa mmoja wa watu wanaotambuliwa katika huduma za afya kwa karne ya 21 kutokana na utendaji wake katika tasnia hiyo nchini Marekani.
Alikuwa akiishi vizuri na mkewe na alishaanza kumtafutia viza ili aweze kwenda kufanya naye kazi na kuishi Marekani.
 
DK. WILLIAM  AZUNGUMZA
Dk. William alipotafutwa na waandishi wetu alikiri kufungua kesi hiyo, akasema:
“Nina mpango wa kumfulia Mwingira kesi nyingine ya madai katika mahakama ya kimataifa kama nitaona hapa Tanzania sitendewi haki.”
 
MWINGIRA JE?
Kwa upande wa Mwingira bado ni vigumu kumpata, kwani jitihada za waandishi wetu kumtafuta kuzungumza naye hazikuzaa matunda, kwani zilikwamishwa na wasaidizi wake ambao hawataki kabisa bosi wao ahojiwe.
 

No comments:

Post a Comment