Monday 27 January 2014

Kama una dalili hizi, basi jua kwamba hujiamini…!



1. Kugusika kirahisi: Mtu asiyejiamini huwa anagusika kirahisi sana, jambo dogo linaweza kumnyima furaha kwa kiwango kikubwa. Jambo dogo linaweza kumuudhi kupindukia. Kuna watu ambao kwa utani mdogo sana wa kawaida wanakasirika sana, wanajihisi vibaya na kuumia sana.

2. Kuwategemea wengine kuthibitisha: mtu asiyejiamini siku zote haamini kuhusu uwezo wake, maamuzi yake au hisia zake, hadi athibitishiwe na wengine kwanza. Hata kama anajua jambo, ana kipaji, hawezi kuamini katika uwezo na nguvu hizo hadi watu wengine wamthibitishie kuhusu usahihi na ubora huo.

3. Kujilinganisha katika kufanya mambo au thamani: Wengi tunakabiliwa na kutojiamini kwenye eneo hili. Tunajilinganisha sana na wengine. Tunafanya mambo yetu mengi wa kushindana na kujilinganisha kuliko kufanya kwa ajili yetu na kwa viwango vyetu. Unanunua gari, siyo kwa sababu unahitaji gari, bali kwa sababu fulani amenunua gari, unataka kumuoneshea. Kila unachofanya ni kwa sababu ya wengine, siyo kwa sababu yako.

4. Kujishusha na kujipandisha thamani kuliko wengine: Kuringa na na kutamba ni dalili ya kutojiamini na sio kujiamini, kama wengine wanavyodhani. Mtu anayeringa na kujikweza sana anajaribu kupunguza maumivu ya hisia zake zilizo chini kuhusu thamani yake. Hii ni sawa na kujishusha. Mtu anajishusha kwa sababu anaamini kwa kujishusha watu watamwona ni wa maana na anayestahili. Lakini bado kujishusha maana yake ni kutafuta huruma na kukubaliwa na wengine, kutokana na hisia za kuwa mtupu. Mtu anayejishusha na yule anayejikweza wote ni mtu mmoja, bali wenye pande mbili tofauti. Kujikweza na kujishusha ni jambo lile lile kwa sura mbili tofauti.

5. Kutaka kuwafurahisha wengine kwa gharama, hasara yake: Asiyejiamini yuko tayari kuumia, lakini awafurahishe wengine, yaani wengine wamuone kuwa wa maana au wasimshushe. Mtu anatakiwa kulipa mchango wa tukio fulani, yaweza kuwa mchango wa harusi au harambee ya kuchangia jambo fulani ambapo kiwango kilichopangwa labda ni shilingi 20,000 tu. Lakini mtu huyu anaweza kusimama na kutangaza kutoa mchango mkubwa kupita kiasi kilichopangwa wakati fedha hizo hana, ili tu kujionyesha kwamba na yeye anazo. Mwisho wa siku anaingia kukopa na kulipa fedha hizo kwa maumivu makubwa sana. Angeweza kulipa kiwango alicho nacho au hata kama hana kuwa mkweli. Hapana, anataka wengine wamuone wa maana, lakini kwa gharama inayompa maumivu makubwa sana. Mifano ni mingi, lakini huu mmoja nadhani unakupa picha nazungumzia watu wa namna gani.

6. Kuogopa kuwajibika na kutupia wengine mizigo: Wengi tuna udhaifu huu. Mtu asiyejiamini, hayuko tayari kuwajibika, kwani kuwajibika kunamfanya ahisi kushuka. Kwa hiyo ili asishuke, hata akikosea, atajitahidi kusingizia au kuwatupia wengine lawama. Hata kwenye kosa la wazi kabisa, ataanza kutafuta kosa dogo hata la mwaka juzi na kulitumia kosa hilo, kujisafisha. Hebu kagua kwenye uhusiano, hasa kwenye ndoa utaona sana udhaifu huu ukijitokeza. Mpenzi au mke anabeba mimba, mwanaume anakuwa wa kwanza kulaumu, “Wewe kazi yako kuzaa zaa tu kama panya.” Mwanaume anaweza kusema kwa kejeli na kulaumu. Hayuko tayari kuwajibika kwamba, hata yeye ana mchango katika jambo hilo. Kwake yeye mwanamke ndiye mwenye makosa.

7. Kutumia nguvu nyingi kulinda hadhi ya uongo: Kuna watu ambao wanaazima magari, wanaazima nguo na vitu vingine ili waonekane kuwa watu wa maana. Hufanya hivyo kwa matumizi ya nguvu nyingi kiakili, kihisia na kimwili ili wajionyeshe. Kuna idadi kubwa ya watu ambao hulinda hadhi za uongo kwa lengo la kutaka kuonesha kwamba, wana thamani. Hii kwa kawaida, ni tabia ambayo inatokana na kutojiamini.

8. Kuogopa sana au kutokuwa tayari kukosolewa, lakini kupenda sana kukosoa: Mtu asiyejiamini anaogopa na kuchukia sana kukosolewa. Ukimkosoa, bila kujali kama ni kwa njia ya kujenga au kubomoa, hatakubali. Mtu asiye jiamini ana kawaida ya kujihami sana, ili asionekane au kujulikana kuwa hajui au hawezi. Kwa hiyo, kumkosoa ni sawa na kumtia msumari wa moto kwenye kidonda. Ili sasa asionekane kuwa hajui, ili udhaifu wake usionekane, anakuwa na kawaida ya kuwakosoa wengine. Anataka wengine waonekane kuwa hawawezi, hawana nguvu, hawastahili na mwengine yanayofanana na hayo. Lengo lake ni kuwashusha hao wengine, akiamini kuwa, hiyo itampandisha yeye.

9. Aibu za ziada na kushindwa kutazama watu usoni: Mara nyingi aibu ni dalili ya mtu kushindwa kujiamini. Aibu maana yake ni kwamba, mtu anaamini na kuhisi kama vile wengine wana mashine za x-ray kiasi kwamba, wanawaona hadi tumboni. Kwa kutojiamini, mtu anahisi kama vile, kila anachofanya kinaonwa na kufanyiwa tathmini, hivyo anaogopa atakosea na kila mtu atajua. Hiyo hasa ndiyo maana ya aibu. Aibu nyingine ni matokeo ya mtu kuamini kwamba, hana thamani, ukilinganisha na wale watu alionao. Hivyo, kwa kuhisi hana thamani, hujiona kama yuko chini mbele ya wale anaoamini kuwa wanathamni zaidi.

10. Kutawaliwa na majuto ya jana na hofu za kesho: watu wasiojiamini wamejaa majuto ya siku za nyuma na wamesheheni hofu za maisha yao ya baadaye. Ni mara chache kwa mtu asiyejiamini kuishi maisha ya leoleo. Kama hajuti kuhusu maisha yake yaliyopita, basi atakuwa amejaa hofu za maisha yake ya kesho.

No comments:

Post a Comment