Wednesday, 12 February 2014

MAMBO TISA MUHIMU KUHUSU SIKU YA VALENTINE


NAAM. Ni wakati mwingine wa Valentine, ile siku ya wapendao ambayo huangukia mwezi huu. Wapo wapenzi, hususan wanaume ambao hawana wasiwasi wowote kuhusiana na ‘sikukuu’ hii. Lakini pia wapo wale ambao wanakuna vichwa, wakifikiria watawapa nini wapenzi wao ili kuonesha kuwa wanawapenda kweli.


Katika zama hizi, wasichana wengi wameingiwa na utamaduni wa Valentine na wapo wanaosubiri ili wapime mapenzi ya wapenzi wao kwa kuangalia jinsi watakavyofanyiwa siku ya Valentine ambayo mwaka huu inaadhimishwa kesho Jumatatu Februari 14, 2011.

Hata hivyo, hupaswi kuwa na shinikizo wala wasiwasi kuhusiana na suala hili, kwani pamoja na suala zima la zawadi, Valentine ni wakati muafaka wa kumfurahisha mpenzi wako na kumwonesha kuwa unamjali.

Zipo imani ambazo watu wamezishika tangu enzi na enzi kuhusiana na jinsi ya kusherehekea siku ya wapendanao. Kutokana na imani hizo, baadhi ya watu hupenda kupuuza taratibu za mapokeo na kutaka kufanya kitu kipya kwa mpenzi.

La msingi ni kutafuta njia iliyo rahisi zaidi kwako, ya kumfurahisha laazizi wako. Na kama bado unasitasita, mambo yafuatayo yanaweza kukusaidia: -

1. KUTOADHIMISHA VALENTINE'S DAY

Baadhi ya watu husema si lazima kusherehekea siku ya wapendanao, kwani si utamaduni wetu.

Ni kweli kwamba maadhimisho ya Valentine yameanzia Magharibi, lakini unapaswa kuangalia matazamio na matamanio ya mpenzi wako.

Mwanamke mwingine anaweza kujiona kama hapendwi anapobaini kuwa wanaume wengine waliwaandalia wapenzi wao hafla ya Valentine.

Kwa hiyo, badala ya kuipuuza kabisa siku hii, waweza kuipa umuhimu mdogo tu na ukatafuta njia zako mwenyewe za kuisherehekea.

Mathalani, waweza kupanga shughuli maalumu kwa ajili yako na mpenzi wako, ambayo mtaifanya kwa ushirikiano, huku akitambua kuwa siku hiyo ni siku ya wapendanao.

2. NI LAZIMA KUADHIMISHA FEB. 14?

Hakuna msahafu unaosema lazima siku ya wapendano iadhimishwe Februari 14. Kwa hiyo unaweza kuchagua siku nyingine kama huna nafasi siku hiyo, kwa ajili ya kumwonesha mpenzi wako kuwa unamjali na kumpenda.

Uzuri ni kwamba siku hiyo nyingine mnaweza kupata utulivu zaidi kwani hata katika kumbi za starehe hakutakuwa na watu wengi.  Mwanamke anayejali, hatajali mmeadhimisha lini, bali ataiangalia nia yako ya dhati ya kumfurahisha na kumwonesha kuwa unamjali.

3. MATUMIZI MAKUBWA YA FEDHA

Baadhi ya watu hufanya maandalizi makubwa kwa ajili ya siku ya wapendanao. Hata hivyo, kama una jambo jingine muhimu zaidi la kufanya, mathalani unasoma, hupaswi kutumia fedha nyingi kwa ajili ya siku hiyo.

Badala yake, kuwa mbunifu na kufanya jambo ambalo kwa hakika litamwonesha mpenzi wako kuwa unamjali kwa siku hiyo maalumu. Mathalani, mnaweza kufanya mtoko mdogo tu wa kwenda nje ya mji kwenye utulivu na kutafakari uhusiano wenu.

Atafurahi kuwa pamoja na majukumu mengi uliyo nayo, bado umekumbuka kuadhimisha mapenzi baina yako na yeye na kumfanya kujiona maalumu kwako.

4. WAPENZI AMBAO HAWAJAZOEANA

Baadhi ya watu ambao bado ni wapya katika mapenzi wanaweza kuona tatizo kusherehekea Valentine, maana hawana uhakika sana kama wanapendana.

Ni kweli kuwa si vema kufanya mambo makubwa na mpenzi ambaye hujafahamu mwelekeo wake, lakini haina maana kuwa umpuuze kabisa siku ya wapendano.

Iwapo utaipuuza kabisa V-Day anaweza akawa na shaka kuhusiana na mapenzi yako kwake, akidhani yamkini huna mapenzi ya dhati kwake.

Kwa hiyo, andaa kitu, si lazima kiwe cha kimahaba. Mathalani, waweza kuandaa shughuli ambayo inachangamsha, ambayo mtaifanya pamoja siku hiyo, au kumpeleka kwenye ukumbi wa maonesho ya sanaa, ambako mtapata nafasi ya kucheka na kufurahi pamoja.

5. CHAKULA SIKU YA VALENTINE

Watu huandaa chakula siku ya Valentine, kwa ajili ya kula na wapenzi wao, au wanaweza hata wakaenda kwenye migahawa ya bei mbaya katikati ya jiji kwa ajili ya kubadilisha mazingira.

Hata hivyo, si lazima kuingia gharama zisizo za lazima kwa ajili ya chakula. Katika jamii za Magharibi ambako ndiko ilikoanzia Valentine, watu hujishughulisha zaidi na mambo ambayo huwaweka pamoja, mathalani kuogelea, au kujifunza kitu chochote mathalani kupika, kucheza muziki na kadhalika na si lazima chakula. Waweza hata kumpa ofa ya kupaka rangi kucha zake na sherehe ikawa imeisha.

6. ZAWADI ZA CHOKOLETI NA MAUA

Kama ilivyobainishwa katika suala la chakula, chokoleti na maua si mambo mabaya kumpa mpenzi wako siku hiyo, lakini vimezoeleka na vinaweza visilete tofauti katika suala zima la mapenzi.

Badala yake, wakati watu wengine watakapovamia maduka ya maua , chokoleti na zawadi nyingine, wewe tafuta kitu ambacho ni ubunifu wako mwenyewe.  Mtafutie mpenzi wako kitu ambacho si mazoea.

Kama anapenda kusafiri na ikatokea kuwa siku hiyo haendi kazini, mpe tiketi ya kwenda mahali ambako mtakwenda pamoja. Kama anapenda muziki, mpe tiketi ya kwenda kwenye onesho maalumu la wapendano na kisha nenda naye.

7. ZAWADI ZA BEI MBAYA

Watu wenye fedha huweza kutumia fedha nyingi kununua zawadi za ghali kwa ajili ya wapenzi wao siku ya wapendanao. Lakini upendo wa dhati ndio muhimu katika siku ya wapendano.

Kwa sababu hiyo, mpe zawadi ndogo lakini yenye maana kubwa. Unaweza kufikiria zawadi yoyote rahisi ambayo una uhakika kuwa ataichukulia kuwa ishara ya mapenzi makubwa uliyo nayo kwake.

Wakati mwingine zawadi inaweza isiwe ya kitu halisi. Pengine ana wasiwasi kuwa humpendi, basi siku hiyo ndiyo siku ya kumhakikishia kuwa unampenda.

8. UTARAJIE ZAWADI KUTOKA KWAKE?

Mara nyingi watu huidhania sikukuu ya Valentine kama sikukuu ya kumfurahisha mwanamke na pengine ndivyo hata makala hii inavyoashiria.

Hata hivyo, hakuna sheria inayomzuia mwanamke kumfanyia kitu kikubwa mpenzi wake katika siku hiyo. Kwa hiyo hata usipotarajia zawadi kutoka kwake anaweza akakupa.

Lakini kama suala la zawadi linakusumbua na pengine ungependa uwepo usawa katika maadhimisho, basi waweza kuzungumza naye na mkashirikiana kupanga jinsi mtakavyoadhimisha siku yenu.

9. NI ZAWADI GANI MUAFAKA?

Hakuna sheria inayosema kuwa zawadi ya Valentine lazima iwe ya kimahaba, au kitu fulani tu. La muhimu zaidi ni kuifanya siku hiyo kuwa ya furaha na kuchangamka.

Baadhi ya watu hupenda kuwanunulia wapenzi wao nguo za ndani katika siku hiyo, lakini mara nyingi hiyo huwa sehemu tu ya safari ya kuelekea katika mapenzi.

Jambo muhimu zaidi la kuzingatia ni kuhakikisha kuwa unaweka mazingira ya ubunifu kwa ajili ya kumfurahisha mpenzi wako siku ya Valentine. Epuka kumwingiza katika mazungumzo yatakayomkera, bali zaidi tafuta kumfurahisha na kumchangamsha.

Siri ya kuifanikisha siku ya wapendano ni kuifanya kuwa siku yako, kisha kuwa mbunifu wa mambo ambayo una uhakika yatamfurahisha mpenzi wako na kumwonesha kuwa ni mtu wa pekee na muhimu kwako.

Siku ya Valentine haiko mbali. Ni kesho. Kwa hiyo kama una lolote unaloliwaza kuhusisana na mpenzi wako, ni vema kutafakari maelezo yaliyotolewa hapa, ili ujue jinsi ya kusherehekea.

No comments:

Post a Comment