Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi.
“Ni vizuri tukakumbusha kuwa migogoro ndani ya vyama vya siasa ni mojawapo ya vyanzo vya uvunjifu wa amani… ni vizuri waandishi wa habari watafakari kwa undani athari za taarifa zao kwa jamii kabla ya kutoa taarifa kwa wananchi kuhusu mgogoro wa ndani ya chama chochote cha siasa,”
Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi amekitaka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kujiepusha na vurugu na uvunjifu wa amani kinapotatua mgogoro wake na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wake, Zitto Kabwe.
Mapema wiki hii, wafuasi wa Chadema walipambana na
wale wanaodaiwa kuwa wafuasi wa Zitto katika eneo la Mahakamu Kuu
wakati kesi hiyo ikiendelea kusikilizwa na hatimaye kutolewa hukumu
iliyompa ushindi Zitto.
Akizungumza kupitia taarifa yake kwa vyombo vya
habari jana jijini Dar es Salaam, Jaji Mutungi alisema vitendo hivyo
vinakiuka sheria ya vyama vya siasa namba 5 ya mwaka 1992.
“Ninawaasa viongozi wa Chadema na Zitto Kabwe
kuwazuia wafuasi wao kujihusisha na vitendo vya uvunjifu wa amani wa
aina yoyote wakati wote ambao mgogoro baina yao unaendelea,” alisema
Jaji Mutungi na kuongeza:
“Mojawapo ya majukumu ya Ofisi ya Msajili wa vyama
vya Siasa ni kusimamia utekelezaji wa Sheria ya vyama vya siasa namba 5
ya mwaka 1992 na kanuni za maadili ya vyama vya siasa ya mwaka 2007
zinazokataza vyama hivyo kuruhusu wanachama au mashabiki wake
kujihusisha na vitendo vya vurugu na uvunjifu wa amani.”
Amewaasa pia waandishi wa habari kujiepusha kushabikia migogoro hiyo kwani ina athari kubwa katika jamii.
“Ni vizuri tukakumbusha kuwa migogoro ndani ya
vyama vya siasa ni mojawapo ya vyanzo vya uvunjifu wa amani… ni vizuri
waandishi wa habari watafakari kwa undani athari za taarifa zao kwa
jamii kabla ya kutoa taarifa kwa wananchi kuhusu mgogoro wa ndani ya
chama chochote cha siasa,” alisema Jaji Mutungi na kuongeza:
“Napenda pia kusisitiza kwamba ni vyema viongozi
na wanachama wa vyama vya siasa waonyeshe ukomavu wa siasa kwa
kushughulikia tofauti zao na migogoro baina yao kwa ustaarabu, utulivu
na amani huku wakizingatia sheria zote za nchi. Hiyo ndiyo demokrasia ya
kweli.” Onyo la Msajili limekuja kutokana na vurugu zilizozuka hivi
karibuni baina ya wafuasi wa Chadema na wale wa Zitto wakati wa kesi
baina ya pande hizo iliyokuwa inasikilizwa Mahakama Kuu jijini Dar es
Salaam.
No comments:
Post a Comment