Thursday, 20 March 2014

Microsoft yaja na jibu la tatizo la wizi mitandaoni


Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni mpya ya mawasiliano ya simu ya Smart, Abdellatif Bouziani akizungumza na waandishi wa habari kwenye hafla ya uzinduzi wa kampuni hiyo jijini Dar es Salaam.

Wavumbua kompyuta itakayotatua tatizo hilo ambalo ni tishio kwa Afrika na dunia kwa ujumla.


Kampuni ya Microsoft, inayojishughulisha na utengenezaji wa kompyuta pamoja na programu, imebuni mbinu mpya ya kukabiliana na wizi wa mitandaoni ambao umezisababishia hasara benki, kampuni na watu binafsi katika maeneo mengi duniani.

Mkakati huo umekuja wakati benki nyingi nchini zikiathiriwa na wizi huo kupitia mashine za kutolea fedha maarufu kama ATM pamoja na miamala inayofanyika kupitia mifumo ya mawasiliano ya kompyuta.
Takwimu zinaonyesha katika kipindi cha Oktoba 2012 hadi Februari 2013, Tanzania inakadiriwa kuwa Sh700 milioni ziliibwa katika benki kwa nyakati tofauti.
Kutokana na hali hiyo Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Profesa Benno Ndulu aliziagiza taasisi za fedha kuchukua hatua ili kukabilina na hali hiyo.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Microsoft, David Finn imeeleza kuwa wamebuni kompyuta mpya pamoja na programu ambazo zinaziba mianya ya wizi. Imeweka wazi kuwa uuzaji holela wa programu za kompyuta duniani umekuwa chanzo cha wezi hao kutumia ujanja katika kufahamu taarifa za siri zilizohifadhiwa kwenye kompyuta za taasisi na hata watu binafsi zilizounganishwa kwenye mtandao.
“Kampuni na taasisi na Serikali zinashauriwa kununua kompyuta mpya kwa mawakala maalumu zitakazowekewa ‘software’ (programu) zilizo halali,” alisema Finn na kuongeza:
“Utafiti uliotolewa mwaka huu na kampuni ya kimataifa ya teknolojia ya mawasiliano ya kompyuta ikishirikiana na Chuo Kikuu cha Singapore unaonyesha, wizi wa kwenye mtandao unagharimu kampuni zaidi ya dola za Kimarekani bilioni 315 kwa mwaka sawa na Sh504 trilioni,”.
Sehemu ya ripoti hiyo imeeleza kuwa maeneo mengi ya Afrika yanakua kwa kasi katika matumizi ya mitandao kutokana na vitendo vya kiharamia na wengi wamejikuta wakipata hasara kwa kuibiwa fedha zao.
“Wizi wa njia ya mtandao unahamasishwa na tamaa ya pesa bila jasho kwa kutumia werevu wa teknolojia kuingilia na kuchukua taarifa muhimu za mtu, kitambulisho, namba za siri au hata pesa, hivyo Microsoft imedhamiria kudhibiti vitendo hivyo ili kuongeza usalama wa taarifa za wateja,” alisema Finn.
Anasema utafiti umebaini kuwa kompyuta 203 zilizo nunuliwa katika maduka 11 tofauti, zilibainika kuwa asilimia 61 ziliathiriwa na programu za kiwizi maarufu kama virusi vinavyoitwa trojans, worms, viruses, hacktools, rootkits na adware.

No comments:

Post a Comment