Chalinze.
Mshindi wa kura za maoni za kugombea ubunge wa Jimbo la Chalinze kwa
tiketi ya CCM, Ridhiwani Kikwete amesema siasa anazofanya sasa hazina
uhusiano wala ubia na baba yake.
Akizungumza na waandishi wa habari
muda mfupi baada ya kutangazwa kwa matokeo ya kura za maoni za chama
hicho katika jimbo hilo kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Msata alisema
anafanya siasa kwa maisha yake na si kwa mgongo wa baba yake kwani
aliingia katika siasa akiwa na umri wa miaka mitano na hakuwahi kufanya
hivyo kwa sababu ya baba yake.
“Siasa ninayofanya haina uhusiano na
baba yangu, nafanya siasa kwa maisha yangu na sina ubia na baba yangu
katika hili” alisema mtoto huyo wa Rais Jakaya Kikwete.
Akijibu swali la kwa nini amejiingiza
katika siasa tofauti na maneno yake aliyowahi kutamka mwaka 2010 kuwa
hawezi kushiriki katika kinyang’anyiro cha ubunge katika jimbo hilo,
Ridhiwani alisema wakati huo hakuwa tayari.
“Kwenye siasa usiwe muwazi katika
kila kitu, ukiwa hivyo unawapa nafasi maadui kukushambulia, mimi hapa
Chalinze ni kwetu, kwa wazazi wangu na kule Bagamoyo tunakwenda tu
kikazi na ndiyo maana nikaamua kurudi nyumbani kuomba ridhaa. Nashukuru
kuongoza katika kura za maoni ninaona ni kiasi gani ninaungwa mkono,”
alisema.
Katika kura hizo za maoni Ridhiwani
alibuka mshindi kwa kura 758, akifuatiwa na Imani Madega aliyepata kura
335, Ramadhan Maneno (206) na Mkwazu Changwa (17).
No comments:
Post a Comment