Mwenyekiti mteule wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta akipongezwa na Mjumbe wa Bunge hilo, Edward Lowassa baada ya kutangazwa matokeo bungeni, Dodoma jana.
Akitoa shukurani zake baada ya kuchaguliwa, Sitta alisema hana uhasama wowote na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge ambaye naye awali alikuwa na nia ya kuwania nafasi hiyo kabla ya kujitoa.
Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta amechaguliwa kwa kishindo kuliongoza Bunge Maalumu la Katiba, huku akisema kuchaguliwa kwake ni sawa na kumrudisha chura kwenye dimbwi la maji.
Jana, Sitta ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la
Urambo Mashariki kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), alipata kura 487 na
kumbwaga mpinzani wake, Hashimu Rungwe wa Chama cha Ukombozi wa Umma
aliyepata kura 69.
Wajumbe wengine, Dk. Terezya Huvisa pia wa CCM na
John Chipaka wa Tadea, walijitoa katika kinyang’anyiro hicho ambacho
tangu awali Sitta alionyesha kujiandaa kwa kutengeneza vipeperushi
alivyovisambaza kwa wajumbe kama sehemu ya kujinadi.
Akizungumza na wajumbe ambao muda mwingi walikuwa
wakimshangilia, Sitta alionekana kujiamini kabla na baada ya uchaguzi.
Pia alitumia misemo lugha ya picha ikiwamo ya chura kuishi majini,
akimaanisha kuwa wajumbe wamemchagua mtu mwenye uwezo, uzoefu na weledi
wa kuongoza shughuli za Bunge.
“Jamani kunichagua mimi ni kama kumrejesha chura
kwenye dimbwi la maji alilolizoea. Msiwe na wasiwasi ataogelea tu na
ninawaahidi kuwa ikiwa kwa kudra za Mwenyezi Mungu, mtanichagua
nitawatumikia kwa uaminifu, sitakubali upendeleo wa aina yoyote,
nitasimamia kanuni tulizozipitisha hapa,” alisema.
Aliongeza kusema: “Nitawaongoza kwa utumishi
uliotukuka na uadilifu ili tupate Katiba bora, yenye viwango na kwa
wakati. Nina hulka ya kuwapenda wale ninaowaongoza, kwa hiyo nitakuwa
mtetezi wa shughuli mbalimbali…Ninawaahidi Watanzania kutenda haki na
kuwapatia Katiba yenye viwango na kwa wakati.
Kuanzia mwaka 2005 hadi 2010, Sitta alikuwa Spika
wa Bunge la Tisa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Akiongozwa na
falsafa yake ya Bunge la kasi na viwango. Pia anatajwa kufanikiwa
kuliongoza Bunge hilo kwa weledi wa hali ya juu.
Kwa sababu ya mafanikio hayo, alipokuwa akiomba kura za wajumbe wa Bunge hilo, hakusita kujifananisha na chura kurudi majini.
Aidha, alisisitiza kuwa ataliongoza Bunge kwa
kutumia falsafa yake ya kasi na viwango, huku akiahidi kulisimamia Bunge
kwa haki na bila upendeleo kwa kundi lolote.
Matokeo ya kura
Akitangaza matokeo, Msimamizi wa Uchaguzi, Dk.
Thomas Kashillilah, alisema Sitta alipata kura hizo 487 ambazo ni sawa
na asimilia 86.5, kati ya kura 563 zilizopigwa.
Dk Kashillilah alisema kwamba mpinzani wa Sittta,
Hashim Rungwe ambaye jana tulimwandika kimakosa kuwa anatoka NCCR-
Mageuzi alipata kura 69, sawa na asilimia 12.3 ya kura zote. Alisema
kura saba ziliharibika.
Moja ya mambo yaliyovuta hisia za wajumbe wengi ni hatua ya
Sitta kushikana mikono ya kupongezana na Waziri Mkuu wa zamani, Edward
Lowassa baada ya kumaliza kuomba kura kutoka kwa wajumbe.
Sitta na Chenge
Akitoa shukurani zake baada ya kuchaguliwa, Sitta
alisema hana uhasama wowote na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew
Chenge ambaye naye awali alikuwa na nia ya kuwania nafasi hiyo kabla ya
kujitoa.
“Namshukuru pia ndugu yangu Andrew Chenge ambaye
watu walivumisha kwamba tulikuwa na mchuano wa uhasama ndani ya chama,
jambo ambalo siyo kweli, “alisema na kuongeza;
“Mheshimiwa Andrew Chenge tuna historia ndefu
sana, nikiwa Waziri wa Katiba na Sheria mwaka 1993, mimi ndiye
niliyependekeza jina kwa Rais wa Awamu ya Pili, Rais Ali Hassan Mwinyi
ili ateuliwe kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.” alisema.
Kwa upande wake, Chenge alisema: “Mambo yote
yaliyozungumzwa na Sitta ni mambo yaliyopita, kilichopo ni kutazama kazi
iliyo mbele yetu.’’
No comments:
Post a Comment