Saturday, 22 March 2014

Wajumbe washindana kushangilia bungeni

Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba jana waligawanyika katika kushangilia hotuba ya ufunguzi wa Bunge hilo iliyotolewa na Rais Jakaya Kikwete.


Mwanachi ilishuhudia baadhi ya wajumbe wa CCM wakidiriki hata kusimama, huku wakipiga makofi wakati Rais Kikwete alipokuwa akielezea upungufu aliouona katika Rasimu ya Pili ya Katiba.
Pia kwa upande mwingine, baadhi ya wajumbe kutoka Zanzibar walionekana wakishangilia baadhi ya sehemu ambazo zilionyesha kuwa na udhaifu uliopo katika muundo wa Serikali mbili.
Baadhi ya maeneo ambayo yalishangiliwa kwa kiasi kikubwa na wajumbe kutoka CCM, ni pamoja na kuondoa jambo la mafuta katika mambo ya Muungano.
Kadhalika, wajumbe walishangilia kwa nguvu wakati Rais Kikwete alipowataka wasisite kuondoa mambo yasiyostahili na yanayostahili kuboreshwa yaboreshwe na kwamba katika Serikali mbili yanatekelezeka mambo yote ambayo yametajwa kuwa masuala ya Muungano katika Rasimu ya Katiba.
Maeneo mengine ambayo yaliamsha hisia kwa wajumbe wa CCM hadi kusababisha baadhi yao kusimama ni wakati aliposema; “Sisi tulioko katika CCM tunaamini Serikali mbili, tunaamini kuwa haya yote yanatekelezeka.”
Hotuba hiyo iliyochukua saa 2.40, upande unaounga mkono muundo wa Serikali tatu ulionekana kushangilia wakati Rais aliposema; “Uamuzi wako usiwe wa kuambiwa na akili za kuambiwa changanya na zako.”
Ufunguzi huo ulipambwa na gwaride pamoja na bendi. Baada ya kufika katika Viwanja vya Bunge, Rais Kikwete alikagua gwaride lililoandaliwa na polisi kisha kuimbwa Wimbo wa Taifa.
Rais Mstaafu wa Zanzibar, Amani Karume alikuwa kiongozi wa kwanza kuingia ukumbini, akifuatiwa na Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi aliyeshangiliwa kupita kiasi.
Aliyefuatia ni Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omari Othman Makungu na kisha Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Othman Chande.
Wengine waliotangulia kuingia ukumbini kabla ya Rais Kikwete, ni Makamu wa Pili wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Seif Sharif Hamad na kisha Rais wa Zanzibar, Dk Mohamed Shein akifuatiwa na Makamu wa Rais ya Jamhuri ya Muungano, Dk. Ghalib Bilal kisha aliingia Rais Kikwete.
Wengine waliohudhuria ufunguzi huo ni mke wa Rais, Mama Salma Kikwete, mke wa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Asha Bilal, mke wa Rais wa Zanzibar, Mwanamwema Shein, mke wa Waziri Mkuu, 

Mama Tunu Pinda, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Mtungi, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Rehema Nchimbi, Mama Maria Nyerere, mke wa Rais wa Awamu ya Pili, Mama Sitti Mwinyi, mabalozi na wawakilishi wa taasisi za dini.

No comments:

Post a Comment