Uamuzi huo ni wa kihistoria kwa kuwa haujawahi
kutumika kokote duniani. Baadhi ya wajumbe wameonyesha kufurahishwa nao
na wengine kuupinga.
Kwa sehemu kubwa kura ya wazi ilikuwa ni msimamo
wa wajumbe wanaotoka kundi la wanasiasa hasa wanaotoka Chama cha
Mapinduzi (CCM).
Hata hivyo, miongoni mwa wajumbe hao wa CCM, wapo
ambao walipinga tangu mwanzo suala hilo, wakisema mfumo huo
unawakandamiza na hauna tija kwa taifa.
Miongoni mwa wajumbe ni Alli Keissy, Kangi Lugola, Deo Filikunjombe, Esther Bulaya, Juma Kapuya na James Lembeli.
Hatua ya wajumbe hao kupingana hadharani na
matakwa ya chama chao, inaweza kuchukuliwa kama ujasiri wa kipekee,
kwani wanafanya hivyo, wakijua ndani ya chama chao baadhi ya wajumbe
wameadhibiwa kutokana na kutofautiana kimtazamo na chama.
Kura ya mseto ilipitishwa kwa kila mjumbe kuitwa
jina lake na kueleza kukubali au kukataa. Hapo ndipo misimamo ya wengi
ilionekana.
Wabunge Kangi Lugola na Deo Filikunjombe
walionyesha misimamo yao hadharani baada ya kupingana na matakwa hayo ya
chama kwa kupinga kura ya wazi. Wakati kura hiyo inapigwa, wajumbe
James Lembeli na Profesa Juma Kapuya hawakuwapo ukumbini.
Nikiwa bungeni nimepata fursa ya kuzungumza na
Lembeli nikitaka kujua msimamo wake ulikuwa upi kama angekuwapo bungeni
siku hiyo ya kupiga kura na yafuatayo ni mahojiano yetu:
Swali: Mheshimiwa Lembeli, pole na
shughuli za hapa bungeni wakati wa kupitisha kanuni za 38 na 39,
sikubahatika kusikia sauti yako mle ukumbini hivi uliunga mkono kura
ipi?
Jibu: Asante, sijapoa maana kazi ndio imeanza, lakini na ninyi mmeanza uchokozi…(kicheko). Kweli haukunisikia kwa sababu sikuwepo.
Swali: Kama ungekuwepo kura yako ilikuwa katika mrengo upi mheshimiwa?
Jibu: Hata siku moja siwezi kula matapishi
yangu. Nimekuwa nikisimamia ukweli na ukweli ndio utakaoniweka huru siku
zote za maisha yangu. Mimi nataka kura ya siri na ndiyo ambayo
ningeitaka siku hiyo bila hofu.
Swali: Kura ya siri inapingwa na chama chako, ni vipi uendelee kuing’ang’ania kwani huogopi kushughulikiwa kisiasa?
Jibu: Vijana msipende kutishwa na
jambo la kushughulikiwa. Anayeshughulika na mwanadamu ni Mungu pekee si
mtu mwingine. Hapa tunafanya kazi za kujifurahisha tu jamani.
Ukisikia mtu anasema atakushughulikia, jiulize
mara nyingi anashughulika na wewe kwa namna gani au juu ya jambo gani,
je ni kwa jambo la ukweli au lile la kinafiki.
Swali: Kwa nini unasema hivyo, una maana chama chako hakina uwezo wa kufanya hivyo?
Jibu: Kinao, lakini najiuliza
hivi mtu anashughulika nami kwa jambo gani? Je, kwa matakwa ya wananchi
au kwa lipi hasa? Mimi nakipenda sana chama changu kuliko wengi
wanavyofikiri lakini nasimamia ukweli ambao chama pia kinautaka.
Swali: Kwa mtazamo wa wengi ni kwamba
Tanganyika uliyokuwa ukiishabikia sasa ndiyo imezikwa rasmi kutokana na
wingi wa kura za wanaopinga rasimu hii, wewe unasemaje?
Jibu: Haiwezi kufa ili mradi watu
wanataka ife. Subirini mle ndani mtatuona, nitaanzia kwenye kamati
yangu hadi tutakaporudi humu ndani. Nasema historia huwa haikarabatiwi.
Swali: Sasa umeshindwa kuonyesha msimamo
wako kwa wapiga kura ambao unasema ndio watu wa kuwaheshimu zaidi. Je,
unawaahidi nini katika mchakato huu?
Jibu:Nasisitiza kuwa msimamo
wangu haupingani na wapiga kura walionituma bungeni na nikipingana kwa
kupiga kura ya wazi hapo watakaponihukumu, lakini nikiwa pamoja na
mawazo yao lazima watanitendea haki.
Swali: Lakini umekuwa na mawazo kinzani wakati wote kuhusu Rasimu ya Katiba, nguvu ya aina hii unaipata wapi?
Jibu: Siyo mawazo kinzani. Naishi
kwa kujifunza na kuangalia watangulizi wetu walisema nini, mfano
Mwalimu Nyerere aliwahi kusema Watanzania wanataka mabadiliko na
wasipoyapata ndani ya CCM wanaweza kutafuta kwingine. Kwa hiyo
mabadiliko ni lazima yaanzie kwetu sisi wa chama tawala.
No comments:
Post a Comment