Inakuwaje watu wangu? Natumaini kwamba mambo ni freshi na mnaendelea
vyema na majukumu yenu ya kila siku. Mimi ni mzima bukheri wa afya na
tunakutana tena kupitia safu hii, lengo ni kuwekana sawa katika masuala
flaniflani yanayogusa maisha yetu ya kimapenzi.
Ndugu zangu, hivi karibuni binti mmoja mwenye umri wa miaka 20
alijikuta kwenye wakati mgumu baada ya jamii inayomzunguka kubaini kuwa
anatoka kimapenzi na ‘mbaba’ mwenye umri zaidi ya miaka 65. Wakati watu
wakijiuliza inakuwaje mzee mzima kutoka na kibinti hicho, taarifa
zikazagaa kuwa, si penzi la kawaida tu bali wawili hao wanatarajia
kuoana hivi karibuni. Kweli Ijumaa iliyopita mzee huyo alimchukua
‘mtoto’ jumlajumla na sasa wanaishi kama mke na mume, watu wamebaki
midomo wazi! Lakini kila linalotokea lina sababu zake na kwa hili
nimeona nilizungumzie leo. Uchunguzi unaonesha kwamba siku hizi vibinti
vidogodogo vimecharukia sana mapenzi ya watu wazima.
Wapo ambao wanafikia hatua ya kuolewa na vijibabu vikiwemo vya
kizungu, ukiuliza unaambiwa bora maisha huku wengine wakishadadia kuwa,
vijana wa siku hizi ni pasua kichwa tu. Mapenzi yao yametawaliwa na
usanii.
Huenda hayo yanayosemwa yana ukweli na yawezekana ndiyo maana leo hii
tunaona kuna ndoa nyingi zinazofungwa huko mitaani kwetu ambazo anayeoa
ni kama vile anamuoa mwanaye au mjukuu wake. Inashangaza sana!
Lakini kama umekuwa ukijiuliza kwa nini haya yanatokea, leo nitakupa
sababu saba ambazo zinawafanya wasichana wadogo kuingia kwenye mapenzi
na watu wazima na wengine kuolewa kabisa.
1. Wanajua kupatiliza wanawake
Katika uchunguzi uliofanyika kwa kuzungumza na baadhi ya wasichana,
imeonesha kuwa wengi wao wanapapatikia watu wazima kwa kuwa wanajua
namna ya kumpatiliza mwanamke. Wanajua kujali, kubembeleza na kuwafanyia
wapenzi wao vitu ambavyo wanavitaka kwa wakati bila longolongo.
Inaelezwa kuwa, watu wazima wanawachukulia wapenzi wao kama watoto hivyo
kuchukua nafasi ya kuhakikisha wanakuwa ni wenye furaha wakati wote.
2. Wanajua kuhudumia
Inasemekana kuwa, mtu mzima anapoingia kwenye uhusiano, anakuwa mwenye
msimamo unaoweza kufanya mambo yakaenda kama alivyopanga. Akisema
anakupenda anamaanisha kweli na atakuwa tayari kwa gharama yoyote
kuhakikisha uhusiano au ndoa inadumu.
Linapokuja suala la fedha, watu wazima wanaonekana si wabahili. Wanajua
kuhudumia ili mradi tu wapewe penzi lenye ujazo unaostahili. Hapa ndipo
panapowagusa wengi.
Katika wasichana 10 niliowauliza sababu za baadhi yao kupenda watu
wazima, 9 walisema ‘wazee’ siyo bahili na wanajua kuhudumia na kumfanya
mwanamke aishi maisha ya raha mustarehe tofauti na vijana ambao mwanzo
wanaweza kuanza kwa kujifanya wanajua kuhudumia lakini baadaye wanageuka
kuwa ‘marioo’.
3. Wanajiamini
Asilimia kubwa ya wanawake ulimwenguni kote wanapenda kuwa na
wapenzi/waume wenye msimamo na wanaojiamini. Hata hivyo inaonesha kuwa,
watu wazima ni wenye msimamo na wanajiamini zaidi kuliko vijana na ndiyo
sababu ya baadhi ya wasichana kuwashobokea.
4. Wamepevuka
Watu wazima ni watu waliopevuka kiakili na kimwili hivyo wana uwezo wa
kuwafanya wapenzi wao nao wakapevuka kadiri siku zinavyokwenda. Ndiyo
maana baadhi yao wakishaolewa au kuwa kimapenzi na watu wazima
wanabadilika katika maamuzi. Hicho ni kitu kinachowafanya baadhi yao
kupenda kuwa na watu wazima.
5. Wameshafanya makosa mengi, wamejifunza
Mtu mzima ni lazima atakuwa amepitia uhusiano na watu wengi. Atakuwa
amepata uzoefu mkubwa kwani atakuwa amefanya makosa mengi na kupitia
hayo atakuwa amejifunza, hawezi kuyarudia.
Kwa maana hiyo mwanaume mwenye umri umri mkubwa akiingia kwenye uhusiano
na kabinti ni vigumu kukakwaza, kila atakalotaka kulifanya ambalo
atahisi atamkosea ni rahisi kuliacha hivyo kumfanya msichana aliyeingia
kwenye uhusiano naye kutopokea samahani za kila mara kwa mara.
6. Hawaigizi
Ni kweli wapo watu wazima wale tunaowaita mafataki ambao wanapomtokea
binti mdogo lengo lao si kuoa bali ni kuonja penzi kisha huingia mitini.
Hata hivyo, uchunguzi unaonesha watu wazima wengi wanajua kupenda na
wanaposema hivyo wanamaanisha kweli, hawaingizi sanaa na ndiyo maana ni
wepesi wa kuhudumia, kubembeleza na kuchukua nafasi ya ‘ubaba’. Hicho
kinawafanya wasichana wengi kukimbilia huko.
7. Hawana wivu wa kijinga
Wapo ambao wana wivu kweli lakini uchunguzi unaonesha kuwa, watu wazima
wengi hasa wale walio kwenye uhusiano hawana wivu wa kijinga unaoweza
kuwa kero.
Hawana tabia ya kupiga simu kila mara na kuuliza uko wapi, hawana
maswali kama vile; ‘yule uliyekuwa unaongea naye ni nani’, kwa kifupi
watu wazima wakipata kile wanachokitaka hawana ile kumfuatilia mtu licha
ya kwamba wakibaini wanamegewa wanaumia sana na ni wepesi wa kuchukua
maamuzi magumu.
KARIBU TENA WANGU!
No comments:
Post a Comment