Ni matumaini yangu kwamba umzima na unaendelea vyema na mishemishe
zako za kila siku kama kawaida. Kwa wale Waislam niwape pole
kwa mfungo na kuwakumbusha tu kwamba, wahakikishe swaumu zao zinakuwa
timilifu kwa kujiweka mbali na yale ambayo yanaweza kuwaharibia.
Mpenzi
msomaji wangu, mapenzi hayana likizo hasa kwa wawili waliotokea
kupendana sana. Huwezi kusema unaenda likizo kumpenda mkeo au mpenzi
wako lakini kuna wakati unalazimika kuwa mbali naye kutokana na sababu
za msingi.
Kama nilivyoanza kueleza hapo mwanzo kwamba, sasa hivi Waislam wako
katika mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Wanatubu kwa mola wao
kutokana na makosa waliyotenda huko nyuma.
Ni kipindi ambacho hata
mke na mume wanazuiwa kukutana kimwili mchana lakini usiku kama kawaida.
Kwa wale ambao hawajaoa ndiyo kabisa hawatakiwi kuwa karibu kimapenzi.
Wapo ambao wanamudu kuuheshimu mwezi huu. Hawa ni wale wenye uelewa,
wanaojua nguvu ya mwezi huu. Wanajua njia sahihi za kuwasiliana na
wapenzi wao na kuhakikisha hawawatibulii swaumu zao. Pia wanawake
wanajua wavaeje ili kujisitiri wao lakini pia kutoteteresha swaumu za
wanaume wanaopishana nao mtaani.
Wakati hao wakifanya hivyo, wapo ambao naweza kusema ni malimbukeni.
Hawa ni wale wasiojua maana ya mwezi huu. Yaani hawana mabadiliko
yoyote, kwanza licha ya kwamba ni Waislam lakini hawafungi na hata tabia
zao hazina tofauti na miezi iliyopita.
Mbaya zaidi ni kwamba, watu hawa wana wapenzi wao ambao wanafunga
wakitafuta radhi za Mwenyezi Mungu. Sasa vuta picha, mwanaume anafunga
lakini mpenzi wake hafungi na wala hajui kama mwezi huu unatakiwa
uheshimiwe. Msichana huyo atavaa kihasara na atalazimisha kutaka akutane
na mpenzi wake pale anapojisikia.
Kinachosikitisha zaidi ni kwamba, msichana huyo akiambiwa na mpenzi
wake kuwa amefunga na ni vyema kipindi hiki wakawa mbalimbali,
anakasirika na inaweza kuwa tiketi ya kuachana.
Achilia mbali hao,
unaweza kukuta mwanaume anajua kabisa mpenzi wake kafunga lakini
analazimisha penzi tena mchana kweupe. Kama si kuomba penzi utamkuta
mwingine ikifika wikiendi ataomba waende klabu kujirusha na akikataliwa
anakasirika ile mbaya.
Jamani, siku 30 siyo nyingi sana, unashindwaje kuvumilia kuwa karibu
na mpenzi wako? Iweje ulazimishe mapenzi wakati unajua kabisa kwamba
mwenza wako yuko kwenye Mwenzi Mtukufu? Sawa, yawezekana wewe imani yako
haikubani lakini mwenzako inambana, kwa nini usimpe ushirikiano afunge
bila vikwazo?
Na kama wewe ni Muislam, hivi kweli hujui dhambi inayoweza kupatikana
ukijiweka karibu na mpenzi wako kama ambavyo mmekuwa mkifanya huko
nyuma? Usitake jamii ikushangae, ni kipindi kifupi tu hivyo
usimkasirishe Mungu kwa kufanya makosa unayoweza kuyaepuka.
Hukatazwi kuwasiliana na mpenzi wako na wala siyo vibaya kukutana na
kuzungumza mawili matatu yanayogusa maisha yenu. Kinachokatazwa hapa ni
kumtega mpenzi wako. Kumvalia nguo ambazo anaweza kukutamani au
kumtamkia maneno ambayo yanaweza kumfanya afungue.
Hivi
kuna haja gani kumtumia mpenzi wako picha ambazo siyo nzuri kupitia
kwenye simu yake? Mchana wa mwezi mtukufu unajipiga picha ukiwa
kitandani kimahaba kisha unamtumia mpenzi wako, huku si kumfanyia
mwenzako makusudi? Swaumu yake ikikataliwa wewe utafaidika na nini?
Tuache kumchezea Mungu! Kumbuka kwamba kipindi hiki unapomuomba Mungu
anakusikiliza zaidi kuliko siku zote. Kitumie kumuomba Mungu aupe uhai
uhusiano wenu, kama ni ndoa basi aidumishe, kama ni uchumba, aharakishe
ndoa yenu, kama ni wapenzi wa kawaida, awajaalie safari yenu iishie
kwenye ndoa.
Niwakumbushe tu kwamba, kama wewe ni Muislam na mpenzi wako ni
Muislam, hakikisha naye anafunga na anatekeleza nguzo za swaumu, ukiona
anakwenda tofauti na mawazo yako tambua hapo huna mtu, ni vyema
ukaachana naye kwani hata mkija kuingia kwenye ndoa mtasumbuana tu.
Kama wewe ni Muislam na mpenzi wako ni Mkristo, kama kweli anakupenda
kwa dhati ataiheshimu swaumu yako na hatakuwa mstari wa mbele
kukutibulia. Ukiona anakulazimisha mumuasi Mungu, ujue huyo si mtu mzuri
na ana nia ya kukuharibia maisha yako ya sasa na hata ya baada ya kifo.
No comments:
Post a Comment