Wewe ni mwanamke au mwanaume ulikuwa na mpenz wako Yawezekana mlikuwa
mnafanya kazi pamoja lakini mmoja akahamishiwa mkoa mwingine au mlikuwa
mnasoma pamoja na kuanzisha uhusiano lakini baada ya kumaliza masomo
kila mmoja akarudi kwao na kujikuta mkiwa mbali mbali licha ya kwamba
mnapendana kwa dhati.
Katika mazingira hayo, bado uhusiano wenu
unaweza ukaendelea na kila mmoja akajisikia amani moyoni mwake, kwa
vipi? Kwa kuzingatia haya ambayo nitayaeleza katika mada yangu ya leo
yanayokitia chumvi kichwa cha habari hapo juu kinachosema, wa kuliua ama
kulidumisha penzi na mpenzi wako aliye mbali ni wewe!
Funga safari, mtembelee
Kufanya safari ya mshtukizo ni kati ya mambo ambayo yatamfanya mwenzi
wako afurahi. Lakini lazima uwe makini kabla ya kufanya jambo hili. Ni
vyema ukawa na uhakika kwamba mna kipindi kirefu hamjakutana na kila
mmoja (hasa yeye) ana shauku sana na wewe.
Nenda bila kumtaarifu,
fikia hotelini, kisha mpigie simu ukijifanya upo sehemu ambayo
alikuacha. Baada ya hapo, ukishahakikisha umeteka hisia zake sawia, sasa
unaweza kumweleza ukweli kwamba upo katika makazi yake mapya.
Hakika itakuwa furaha kubwa, ingawa pia inawezekana ikawa huzuni, hasa
kama alikuwa anakusaliti. Kama ikiwa hivyo, si haba kwani angalau
utakuwa umefahamu ukweli kwamba mwenzi wako hakuwa wako, kwani ni
msaliti na aliyekuwa anakupotezea muda wako. Sina shaka utakuwa mpya!
Mawasiliano ya mara kwa mara
Kuwasiliana na mpenzi wako mara kwa mara, kunatajwa kama njia mojawapo
kati ya nyingi zinazoweza kukusogeza karibu zaidi na mpenzi wako aliye
mbali na hivyo kulitia mbolea penzi lenu.
Hata hivyo, wengi
hushindwa kujua aina ya mawasiliano na jinsi ya kutumia ili kuteka akili
za wapenzi wao na kuwafanya waendelee nao siku zote licha ya kuwa mbali
nao.
Kutokana na hilo nimeamua kuwaletea dondoo za mawasiliano ambazo zinaweza kutumika katika kumvuta mpenzi wako.
Kumwandikia email au kwa kiswahili tunaita baruapepe. Njia hii ya
mawasiliano kwa wapenzi walio mbali ni nzuri sana. Hata hivyo,
inategemea mpenzi wako yuko wapi, maana kuna maeneo mengine hayana
huduma za Mtandao wa Internet.
Kutokana na kukua kwa Teknolojia,
wengi humiliki kompyuta za mikononi (lap top) ambazo huwarahisishia
mawasiliano ya moja kwa moja na watu wengi. Kama mpenzi wako ni mmoja
wao, hii ni nafasi nzuri sana kwako.
Mtumie kadi nzuri zenye
ujumbe mwanana wa mapenzi kwa ajili ya kuhamasisha penzi, mwandikie
tungo za mapenzi ukionyesha ubunifu wako. Pia waweza kumtumia vichekesho
kwa ajili ya kumburudisha na kumfanya mwenye furaha.
Kumpigia simu
au kumtumia sms. Kuwasiliana kwa njia ya simu za mkononi ni moja kati ya
njia bora za mawasiliano na kuboresha uhusiano wa wapenzi. Mwenzi wako
anapokuwa mbali na wewe, kwa kutumia njia hii, unaweza kumsogeza karibu
yako na kufurahia uwepo wako, ingawa yupo mbali na wewe.
Umpigiapo simu lazima maneno yako yawe laini, zungumza naye kwa
unyenyekevu na kumtia hamasa ya kuzidi kuzungumza na wewe. Kadhalika
unapomwandikia meseji, kaa chini na utunge, siyo unamwandikia ‘sema mtu
wangu, uko shwari? Umeshakula?’. Hii si meseji ya kumtumia mpenzi wako
aliye mbali na wewe.
Unapaswa kumtumia sms za mapenzi, tungo za
mahaba, maneno ya utani, vichekesho na kejeli ni kati ya vitu vya
kufurahisha ambavyo vikifanywa, humfanya mwenzi wako kutokuwa tayari
kukusaliti.
Unaweza kumtumia meseji nyingi kadri uwezavyo
kulingana na uwezo wako wa fedha, ingawa mitandao mingi ya simu za
mkononi siku hizi huwa na ofa maalum ya kutuma sms nyingi kwa gharama
ndogo! Unaweza kujisajili kila siku kwa ajili ya kurahisisha mawasiliano
na mpenzi wako.
Pamoja na kwamba uwezo wako kifedha, muda na
majukumu vinaweza kukufanya uamue idadi ya sms utakazomtumia mpenzi
wako, lakini ni lazima umtumie angalau sms tano kwa siku.
Meseji
hizo hutumwa kwa muda maalum kama vile baada ya kuamka asubuhi ambapo
unapaswa kumtumia ujumbe mzuri wa kumtakia asubuhi njema na mafanikio
katika kazi zake za kutwa hiyo.
Mchana, mtakie mlo mwema na kazi
njema, alasiri mtumie ujumbe wa kichekesho. Usiku, mtumie ujumbe wa
kumpa pole kwa kazi, kisha malizia kwa kumtumia ujumbe mwanana wakati wa
kulala. Kama nilivyoeleza awali, unaweza kutuma meseji nyingi zaidi
kulingana na uwezo wako na muda huku ukizingatia majukumu yako ya kazi.
No comments:
Post a Comment