Tuesday, 15 July 2014

UKATILI: Ndoa ya watoto yageuka majanga, nusura amuue mke kisa ng’ombe

Ghati Sagire ambaye licha ya umri wake kuwa mdogo, lakini sasa ni mke wa mtoto mwenzake.
Ni muda wa saa 5:45 asubuhi tunafika nyumbani kwa  Simioni  Sagire, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mifugo katika kijiji cha Kwitete kata ya Nyamoko wilaya ya Serengeti Mkoa wa Mara.
“Walioana wakiwa na umri wa miaka 14 mwaka jana”
Haikuwa kazi rahisi kufika kwenye mji huo, kutokana na kutokuwepo barabara ya kupita gari, inatulazimu kuacha gari na kutembea kwa miguu kwa dakika 45, kutokana na mazingira hayo.

Tunalakiwa na mama mmoja na binti mdogo akiwa amefunika kichwa chake kwa kitambaa cha mezani  kilichofumwa kwa nyuzi, uso wake ukiashiria kuwa anakitu kimemtokea, wakati wa kutusalimia anaonyesha kukunja uso ikiwa ni ishara kuwa anakabiliwa na maumivu makali, lakini pia amejaa hofu.

Hofu hiyo haikuwa kwa binti huyo tu bali hata mama aliyetulaki na  waliokuwepo hapo jirani, kwa kifupi ilitosha kuakisi kuwa kuna kitu kisichokuwa cha kawaida kimetokea ndani ya mji huo, walipata ujasiri kwa kuwa tulikuwa na Mwenyekiti wa Serikali ya kijiji hicho, anawaita kwa lugha ya Kikurya, wanaitikia kwa lugha hiyo hiyo.

Kwa nini tupande milima na kushuka mabondeni  

Kuzagaa kwa taarifa za vitendo vya ukatili  katika mji wa Mugumu aliofanyiwa mtoto  wa kike baada ya  kukatwa nyuma ya shingo kwa panga na kunusurika kufa, ndiyo msukumo wa kupanda milima na kushuka mabondeni.

Kumbe ni mke wa mtu  

Mama aliyetupokea anaketi jirani yetu na kujitambulisha kwa majina ya Rhobi Simioni (46) mke wa Simioni Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mifugo, tunamwomba atuitie mtoto wake aliyefanyiwa ukatili, kwa mshangao anasema, ”huyo ni mke wa mtoto wangu toka wameoana wana zaidi ya mwaka mmoja,”anasema na kutushangaza.

Anatambua mshangao wetu, kabla hatujasema kitu anamwita huyo mke wa kijana wake, anakuja kwa aibu na hofu lakini pia anahisi maumivu makali kutoka na shambulio lililolenga kumtoa roho.  Anajitokeza mtoto aliyekuwa amejifunika kitambaa kichwani, tunabaki kutizamana, lakini yeye bila hata chembe ya aibu anamtaka akae kwenye kigoda kisha aseme nasi kuhusiana na maswahibu yaliyomkuta.

Kabla hajasema kitu anatoa kitambaa kichwani na kutuonyesha shingo yake kwa nyuma,tunastushwa na hali hiyo, kisha anakaa na kujitambulisha kuwa anaitwa Ghati Sagire (15) mke wa Sagire (15)mtoto mwenzake ambaye sasa anaishi kwa kujificha akihofia kukamatwa kutokana na kumkata mke wake kwa panga.

Kisa ng’ombe walipigana malishoni

Ghati anajieleza kwa kusita huku akishindwa  kujieleza vizuri kwa Kiswahili, anasema alikatwa kwa panga na mume wake, baada ya kuwa ng’ombe wa baba mkwe wake kupigana na ng’ombe wa jirani, kitendo kilichomkasirisha mume wake na kuanza kumpiga.

“Mimi nilirudi nyumbani kuja kunywa maji, nikaacha ng’ombe wanachunga…kurudi nikakuta wanapigana wa kwetu na jirani…mume wangu alipofika tu akaanza kunipiga kwa nini nimeacha ng’ombe wakapigana…nikakimbilia  kwa wifi yangu Ghati Mkango ambaye amejifungua,” anasema

Anasema aliporudi  nyumbani kwa mama mkwe wake, alimrudisha  akachunge ng’ombe, akiamini ugomvi umeisha, akarudi mlimani kuangalia ng’ombe akiwa hajui mume wake kama bado ana hasira.

Jinsi alivyokatwa  Anasema akiwa anachunga ng’ombe wifi yake alimwomba amfuatie maji kisimani, ghafla akiwa amejitishwa maji alimwona mume wake akimjia kwa kasi ameshikilia panga,”nilirusha ndoo nikaanza kukimbia nikielekea kwa wifi…akarusha panga na kunikata shingo kwa nyuma…nilianguka nikipiga kelele kuomba msaada, alichukua panga lake na kumkabidhi, akatoweka,” anabainisha.

Apelekwa hospitali  

Anasema alifikishwa hospitali ya Nyerere akiwa hajitambui, hajui ameshonwa nyuzi ngapi na kipindi chote alichokaa hospitali akiuguzwa na mama mkwe wake mume wake hakuwahi kufika.

Sababu za ugomvi wao zatajwa  

Pamoja na kutaja  ugomvi wa ng’ombe kama chanzo, baadhi ya majirani wanasema wana  ugomvi wa mara kwa mara kutokana na utoto, kutoaminiana , kutoheshimiana , wivu wa mapenzi na ushauri mbaya wa wazazi.

“Sagire mume wa Ghati amekuwa anachochewa na baba yake kuwa  anadharauliwa na mke  kwa kuwa anafuatwa na mpenzi wake wa zamani aliyekuwa mchunga ng’ombe kwao hadi kwake,” anasema jirani yao.

Aliolewa kwa ng’ombe wanane  

Kwa mjibu wa Rhobi mama mkwe wa Ghati anasema walitoa ng’ombe wanane kama mahari baada ya wao kupendana, pamoja na kuwa umri wao ni mdogo ambao wanatakiwa kuishi chini ya uangalizi wa wazazi na kijana huyo ni wa kwanza kwao wakaona bora kumuoza.

Alitishia wazazi kujinyonga  

Pamoja na umri mdogo huo Ghati alikataa shule  akiwa darasa la sita na kuwatishia wazazi wake kama hawatakubali aolewe basi atajinyonga, na kuwa hapendi kupata ujauzito akiwa kwake.

Adanganya umri  

Ili aonekane mkubwa amekuwa akitoa taarifa tofauti za umri wake, hasa baada ya kufanyiwa ukatili, taarifa zilizoko hospitalini zinadai ana miaka 15 umri unaoafikiwa na  baba yake mzazi, lakini baada ya kutoka hospitali wakwe zake wanamtaka aseme ana miaka 16.

Mama mkwe wake adai wao hugombana lakini hawakatani kama hao  Kuhusu ugomvi wao licha ya kujua chanzo alidai hata yeye hajui vizuri,”haya ni mambo ya watoto...hata sisi huwa tunagombana lakini si kukatana kama wao…chanzo sijakijua vizuri…wakiombana samahani wataishi tu,”anasema.

Hata hivyo alipotakiwa kubainisha kama wako tayari kumpeleka polisi kijana wao,”hospitali wameniambia Julai 8 akatolewe nyuzi kisha twende polisi,”  anasema.

Jirani  

Marwa Mwita (40) mkazi wa kitongoji hicho ambaye ni mume wa wifi wa Ghati akieleza kwa lugha ya Kikurya anasema akiwa shambani mtoto wake alimfuata na kumwambia mjomba wake amemkata panga mke wake, hata hivyo alikuta mama mkwe wake ameishampeleka hospitali.
Mwenyekiti wa Serikali ya kijiji  Joseph Manywele Mwita Mwenyekiti wa Serikali ya kijiji hicho anakiri kuwa wazazi wote wana makosa kwa kuruhusu ndoa ya watoto wadogo,”hawa ni watoto, ndiyo maana mlikuwa mkiuliza huyo mtoto ikawa ngumu kufahamika kwenye kundi la vijana …hata shughuli za maendeleo hawafanyi...ni watoto walipaswa kuwa shule,” anasema.

Wanaishi kwa kujificha

Baba wa mtuhumiwa na mwanaye wanaishi kwa kujificha kwa hofu ya kukamatwa, kwa kuwa kama kiongozi wa kitongoji anapaswa kumkamata mtuhumiwa ambaye ni mwanaye ampeleke polisi.  Baba mzazi wa

Ghati akana kupokea mahari  

Baba mzazi wa Ghati aliyejitambulisha kwa jina moja la Kinyunyi, ambaye anatambulika kama tajiri kijijini  hapo kutokana na kumiliki wanawake wanane na ng’ombe nyingim, anakana kupokea mahari ya mtoto huyo, madai ambayo yanakinzana na maelezo ya mtoto wake kuwa baba yake ndiye aliyepokea.

“Katoto hako ni kadogo nilikaambia kasome kakakataa…maana waliokubali nimewasomesha ….nina watoto wanane wako chuo kikuu, wengine wameishamaliza wanakazi zao…hata mahari yake ilichukuliwa na ndugu yake…unajua pamoja na kuumizwa hivyo sijaenda kumwona …nahitaji nikutane na baba wa kijana tuzungumze tuone nini cha kufanya,” anasema.

Polisi wanakosa ushirikiano  

Mratibu wa dawati la Jinsia la Polisi Sajenti Sijali Nyambuche anasema wameenda mara mbili kwao  mtuhumiwa bila mafanikio, na hawapewi ushirikiano na uongozi wa kitongoji na jamii inayowazunguka.

Hospitali wanasema jeraha ni hatari  Nyachamba Mulaga Muuguzi Hwospitali Teule ya wilaya ya Nyerere anasema, jeraha hilo ni hatari na kuwa mtuhumiwa alikusudia kumuua kwa kuwa eneo hilo lina mishipa mingi,”matukio ya ukatili wa kijinsia yamekithiri sana hapa…hatua kali zinatakiwa kuchukuliwa,“ anasema.

Mwanasheria  

Rodrick Maro Mwanasheria kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) anasema tukio hilo ni kosa la jinai, mtuhumiwa anatakiwa kushitakiwa kwa jaribio lake la kutaka kumuua mke wake,” lakini pia wazazi wa pande zote mamlaka zinatakiwa kuwachukulia hatua kwa kuwa wanakwenda kinyume na Sheria ya Mtoto namba 21 ya mwaka 2009,”anasema.

No comments:

Post a Comment