Wananchi wakimwadhibu kibaka baada ya kutumu kufanya mambo yanayopingana na jamii yenye watu wastaraabu. Picha ya Maktaba.
KIJANA mwenye umri wa miaka 20 mkazi wa
Kijiji cha Isagala, wilayani Kishapu, mkoani Shinyanga, ameuawa na watu
waliojichukulia sheria mkononi wakimtuhumu kuiba kuku wanne.
Aidha
katika tukio la wilayani Tarime mkoani Mara, mtuhumiwa wa ujambazi wa
kutumia silaha , Senso Mwita ameuawa katika kile kilichoelezwa ni kwenye
majibizano ya kurushiana risasi na polisi.
Kuhusu anayetuhumiwa
kuiba kuku, Polisi imemtaja ni Ngaga Shija ambaye alipewa kipigo na
kisha mwili wake kuchomwa moto, alikuwa akituhumiwa kuiba kuku hao
katika kijiji cha Ikonda.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa
Mkoa wa Shinyanga, Evaresti Mangala, kabla ya kifo, Shija alikuwa nje
kwa dhamana katika kesi iliyokuwa ikisikilizwa Mahakama ya Wilaya ya
Shinyanga, akikabiliwa na mashitaka ya unyang’anyi wa kutumia silaha na
kupatikana na mali ya wizi.
Aliuawa juzi saa 2 asubuhi katika
Kijiji cha Isagala Kata ya Mwamashele wilayani Kishapu. Hata hivyo
Kamanda alisema mmiliki wa kuku wanaodaiwa kuibwa, hajafahamika.
Katika
tukio la wilayani Tarime, mkoani Mara, mtuhumiwa wa ujambazi wa kutumia
silaha , inadaiwa alikuwa na wenzake wawili ambao walijibizana na
polisi kwa kurushiana risasi.
Mwita anayekadiriwa na umri wa
miaka kati ya 25 na 30, inadaiwa alikuwa akisakwa na Polisi muda mrefu
kwa kuhusika na matukio ya unyang’anyi wa kutumia silaha na mauaji
katika Tarafa ya Ingwe.
Kamanda wa Polisi Tarime / Rorya, Justus
Kamugisha alisema mwezi uliopita kulikuwa na matukio ya mauaji ya watu
katika vijiji vya Keisangura , Nyamwaga , Genkuru, Mriba na Nyarero.
Alisema
usiku wa kuamkia Januari 5, Polisi ilipata taarifa kutoka kwa raia wema
juu ya kuwepo na kuonekana kundi la majambazi katika kitongoji cha
Ntarechagini Kijiji cha Nyamwaga.
“Wakati askari wetu wakiwa
njiani kuelekea katika kitongoji hicho, ghafla walishambuliwa kwa
kurushiwa risasi na majambazi watatu na hapo ndipo askari wetu walianza
kujibu mapigo na kufanikiwa kumjeruhi mmoja wao kwa jina la Senso Magabe
Mwita,” alisema Kamanda.
Kwa mujibu wa Kamanda, Mwita alikuwa
na silaha aina ya SMG iliyofutwa namba zake na risasi 21. Wenzake
walitoroka na yeye alifariki kutokana na majeraha ya risasi akiwa njiani
kupelekwa hospitali ya wilaya.HABARILEO.
No comments:
Post a Comment