Saturday, 4 January 2014

CCM yamtolea uvivu Lowassa urais 2015


“Tutawaita wote walioonyesha nia ya kuutaka urais 2015 na kuwahoji kwa nini wanafanya hivyo wakati muda bado haujafika. Tumeshawa chunguza, tumebaini kuwa wanatoa misaada na kusafirisha watu, tunajua dhamira yao ni nini.” Phillip Mangula
  

Mangula alisema kama wanachama hao wasipochukuliwa hatua watakifanya chama hicho kupoteza mvuto katika medani ya kisiasa nchini

Dar es Salaam. Unaweza kusema sasa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeamua kumfungia kazi Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa baada ya jana Makamu Mwenyekiti wake (Bara), Phillip Mangula kusema kuwa wanachama wake walioanza mbio za kuwania urais mwaka 2015 watachukuliwa hatua kali za kinidhamu.
Mangula alisema kama wanachama hao wasipochukuliwa hatua watakifanya chama hicho kupoteza mvuto katika medani ya kisiasa nchini;
“Wapo watu wanataka waichanechane CCM kwa sababu ya uroho wao wa madaraka, uroho wa udiwani, ubunge na hata urais. Kuna makundi ndani ya chama kazi yake ni kuwabomoa wenzao, kamwe hatuwezi kuyafumbia macho.”
Akifafanua hilo Mangula alisema: “Tutawaita wote walioonyesha nia ya kuutaka urais 2015 na kuwahoji kwanini wanafanya hivyo wakati muda bado haujafika. Tumeshawachunguza katika mikutano wanayoifanya, tumebaini kuwa wanatoa misaada na kusafirisha watu, tunajua dhamira yao ni nini.”
Mangula ametoa kauli hiyo ikiwa imepita siku moja tangu Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye kusema mwanachama yeyote wa CCM anayetangaza nia ya kuwania urais kabla ya muda mwafaka kutangazwa atapoteza sifa za kugombea.
Nape alitoa kauli hiyo baada ya Lowassa siku mbili zilizopita, kutangaza nia ‘kimtindo’ akisema anaanza rasmi safari aliyoiita ya matumaini ya ndoto zake, ambayo pia itatimiza ndoto za Watanzania za kupata elimu bure, maji safi na maendeleo ya uhakika.
Lowassa ambaye amekuwa akitajwa kuwa mmoja wa wagombea wa nafasi ya urais kupitia CCM katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, alitoa kauli hiyo katika ibada ya shukrani ya kuupokea mwaka mpya, katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Monduli.
Mangula aliwashukia vigogo wa chama hicho wanaoutaka urais jana katika Kikao cha Halmashauri Kuu ya Kamati ya Siasa tawi la Ofisi ndogo za chama hicho Lumumba, wakati akitoa salamu za mwaka mpya kwa wanachama wote wa CCM nchini.
Ataja kanuni za uongozi
Katika mkutano huo Mangula alisaidiwa kusoma kanuni za uongozi na maadili ya chama hicho, kutolea ufafanuzi mambo mbalimbali na Katibu Tume ya Udhibiti wa Nidhamu ya Viongozi wa CCM na wanachama taifa, Masoud Mbengula.
Moja ya kanuni hizo inasema “Ni mwiko kwa kiongozi wa CCM kutumia dini yake au kabila au rangi au jinsia au eneo analotoka, kama sifa ya kushawishi wapiga kura wamchague ama yeye mwenyewe ama mgombea anayemuunga mkono.”
Mangula alisema kwa mujibu wa kanuni za chama hicho, mwanachama anayefanya mambo kinyume na kanuni huitwa msaliti na hafai kuendelea kufumbiwa macho kwani anaweza kukiangamiza chama wakati wowote.

No comments:

Post a Comment