“Naomba nichukue nafasi hii kumwomba Rais Kikwete amwondoe Pinda katika nafasi hiyo, la sivyo akimwacha ajue Serikali itakuwa legelege, haitaweza kutekeleza wajibu wake ipasavyo
Waziri Mkuu Pinda hatoshi na amepwaya, baadhi ya mawaziri wanamdharau na ndiyo maana wengi hupuuza hata kuhudhuria vikao vya Bunge. Kwa hali ilivyo sasa nchi hii inahitaji Waziri Mkuu ambaye kama mawaziri hawamheshimu, ni lazima wamuogope,”
Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila amesema sehemu kubwa ya udhaifu wa kiutendaji katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unachangiwa na ukimya wa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Kafulila amesema udhaifu huo unatokana na baadhi
ya watendaji wa Serikali kumdharau Pinda kwa sababu kiongozi huyo siyo
mkali kwa watu wanaokwenda kinyume na maadili, miko ya uongozi, pamoja
na wale wanaofanya uzembe kazini na kujihusisha na ufisadi.
Mbunge huyo ametoa kauli hiyo kwenye mikutano ya
hadhara katika Vijiji vya Uvinza, Kandaga na Nguruka alipokwenda kueleza
mafanikio na changamoto alizopata katika miaka mitatu ya uongozi wake.
Kauli hiyo inakuja ikiwa zimepita wiki mbili tangu
Waziri Pinda alipolieleza gazeti kwamba atazungumzia shinikizo la
kutakiwa kujiuzulu linalotolewa na wabunge mbalimbali, baada ya Sikukuu
ya Krismasi na Mwaka Mpya.
Shinikizo la kutaka Waziri Mkuu ajiuzulu liliibuka
upya baada ya kutolewa kwa ripoti ya uchunguzi wa utekelezaji wa
Operesheni Tokomeza Ujangili ambayo ilisababisha Rais Jakaya Kikwete
kutengua uteuzi wa mawaziri wake wanne, huku baadhi ya wabunge wakimtaka
Pinda naye aachie ngazi.
Jana Mwandishi wa Habari wa Ofisi ya Waziri Mkuu,
Irene Bwire alipoulizwa juu ya suala hilo alisema, “Mheshimiwa Pinda
hakuwepo na amerudi jana tu (juzi), ila si aliwaahidi kuwa atazungumza
baada ya sikukuu, subirini atazungumza tu.”
Katika mkutano wake wa hadhara Kafulila alisema,
“Waziri Mkuu Pinda hatoshi na amepwaya, baadhi ya mawaziri wanamdharau
na ndiyo maana wengi hupuuza hata kuhudhuria vikao vya Bunge. Kwa hali
ilivyo sasa nchi hii inahitaji Waziri Mkuu ambaye kama mawaziri
hawamheshimu, ni lazima wamuogope,” alisema Kafulila.
Alisema Waziri Mkuu amekuwa na lugha laini na
isiyotisha kwa watendaji wa chini yake kiasi kwamba hakuna anayehofu
hata inapotokea waziri huyo anafanya ziara mikoani kama ilivyowahi
kutokea kwa baadhi ya wawaziri waliotangulia kabla yake.
“Mara nyingi utamsikia Waziri Mkuu akijibu maswali
ya Wabunge kwamba; tutaangalia, bado tunatafakari, mara oooh tuvute
subira kidogo, tutachukua hatua. Majibu ya namna hii kwa kiongozi mkuu
wa Serikali ni hatari na yameendelea kuwapa kiburi wasaidizi wake kiasi
kwamba hawahofu tena kuchukuliwa hatua za kinidhamu, hizi kauli
zinaathiri ustawi na maendeleo ya wananchi” alifafanua Kafulila.
Amesema njia pekee ya kuleta nidhamu ni kuondolewa
kwa Pinda Serikalini na kuteuliwa mtu mwingine atakayesimamia kwa dhati
majukumu ya Serikali ikiwa ni pamoja na kudhibiti rushwa ambayo
imekithiri zaidi katika Serikali za Mitaa.
No comments:
Post a Comment