Watanzania waliobobea kwenye taaluma ya Lugha ya Kiswahili wametakiwa kuchangamkia fursa ya kwenda kufundisha Kiswahili katika nchi mbalimbali ambazo lugha hiyo inakua kwa kasi.
Akizugumza na gazeti hili baada ya kuchaguliwa
kuwa Mwenyekiti mpya wa Baraza la Kiswahili (Bakita), Profesa Martha
Qorro alisema ukuaji wa Kiswahili unaenda sambamba na uibukaji wa fursa
ambazo zinaweza kuwa chanzo kikubwa cha ajira.
Qorro alisema kadiri siku zinavyokwenda, thamani
ya lugha ya Kiswahili inaonekana kukua katika mataifa mbalimbali hivyo
kuhitajika wataalamu wengi waliobobea katika lugha hiyo.
“Tuna kila sababu ya kuchangamkia nafasi hizi
kwania wanahitajika walimu na watafsiri, lakini tumejiweka nyuma matokeo
yake wenzetu Wakenya wanaendelea kunufaika, na hilo linatokea kwa kuwa
sisi hatuzitumii fursa hizo kama wanavyofanya wenzetu,” alisema Qorro.
Aidha, Qorro alivitaka vyombo vya habari
kushirikiana na Baraza la Kiswahili ili kupunguza kasi ya upotoshaji
katika matumizi ya lugha ya Kiswahili.
Alisema kuwa kwa kiasi kikubwa vyombo vya habari
vimekuwa mstari wa mbele katika kupotosha matumizi sahihi ya Kiswahili
kutokana na kuweka maneno yasiyo rasmi.
“Bakita imekuwa ikifanya kazi kubwa sana katika
kukuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili lakini bado vyombo vya habari
vinaendelea kushiriki kwa namna moja au nyingine kuweka maneno yasiyo
rasmi hali ambayo iarudisha nyuma juhudi hizi,” alisema Qorro.
No comments:
Post a Comment