Monday 22 April 2013

JENGA WATOTO KATIKA MSINGI MZURI WA KUOMBA NA KUMTEGEMEA MUNGU.......


WATOTO huwa kwa kawaida wanajifunza kutoka kwa watu wazima. Hujifunza kutoka kwa wazazi, walezi, watu wanaoishi nao au kuchangamana nao na kutoka katika jamii inayowazunguka kwa ujumla wake.
Viumbe hawa wamepewa uwezo mkubwa wa kudaka kila wanachoona ama kusikia, iwe ni kibaya au ni kizuri, wenyewe ni rahisi kukibeba tena kama kilivyo, ndio maana ni vyema watu wazima kuwa makini na kila wanachozungumza ama kufanya.
Kutokana na uwezo wao huo, ni vizuri mtoto ukamjengea msingi wa kumcha Mungu, mfundishe umuhimu wa kuomba na kumtegemea Mungu, haijalishi ni dini ama madhehebu gani.
Ukimjenga mtoto katika msingi wa kufahamu umuhimu wa kuomba, popote atakapokuwa awe na mzazi au mwenyewe atakuwa na uwezo wa kujiombea ama kumuomba Mungu ulinzi au chochote anachoamini Mungu wake anaweza kumpa. Kwa msingi huo ni vizuri mtoto anapoanza kuongea ukaanza kumfundisha kuongea na Mungu wake, hapa utakuwa unamjengea imani kwa Mungu wake.
Usisubiri awe mkubwa ndio umfundishe kuomba, anza mapema kumjengea msingi imara wa maombi, kwani yatakuja kumsaidia katika maisha yake huko mbele, sio tu kwamba ni kujiwekea ulinzi lakini pia atakuwa anajiamini maana anajua Mungu wake yupo.
Wazazi na walezi fundisheni watoto kumshukuru Mungu kwa mambo mbalimbali mfano afya, wazazi, michezo, chakula, nguo n.k., unaweza kuviona kuwa ni vitu vidogo ama havina maana lakini kwa Mungu kushukuru ni kushukuru tu, hajalishi unashukuru kwa kitu gani.
Wafundisheni kumuomba Mungu wanapata hofu, huzuni au kuumizwa, vilevile wajifunze kuwaombea wadogo na wakubwa zao, walimu, marafiki na majirani pia, yote ni katika kumjengea ufahamu wake kwamba kumtegemea Mungu ni muhimu. Lakini pia tabia hii itamjengea upendo kwa watu ambao anawaombea.
Lazima afahamu kuwa Mungu anampenda na anasikia maombi yake na anapenda kuzungumza naye, na hata akipata tatizo atakuwa ni mtu anayejiamini maana anajua Mungu atamtetea.
Jifunze kuomba naye wakati wa kula, akiamka asubuhi, usiku wakati wa kulala, anapokwenda shule na kuombea watu wenye mahitaji ama shida, lakini pia mfundishe umuhimu wa kumshukuru Mungu pale maombi yake yanapojibiwa.
Huu ni msingi ambao utawajenga katika muelekeo wa kumtegemea zaidi Mungu, kujiamini na kujitegemea badala ya kutegemea wanadamu.

Wazazi na walezi kumbukeni kile bora utakachopanda katika ufahamu na akili ya watoto wako kitatoa matunda mazuri katika maisha yake ya baadaye lakini kama atakuwa amebeba yasiyofaa katika ufahamu au akili yake ndicho pia kitakachotokea katika maisha yake ya baadaye.
Tuwajenge watoto katika misingi bora ili waje kuwa raia wema katika jamii wanazoishi

No comments:

Post a Comment