Mithali 14:1“Kila mwanamke aliye na Hekima hujenga nyumba yake; Bali aliye mpumbavu hibomoa kwa mikono yake mwenyewe”
Kuna mithali isemayo “MAJUTO MJUKUU”, ni kawaida kwa wanandoa kuangalia na kulaumiana juu ya matatizo yanayojitokeza, badala ya kutafakari chanzo cha matatizo. Matatizo mengi ya ndoa yanatokana na wanandoa kutokuwa na elimu ya ndoa na kutofuata ushauri wa Mungu aliyeanzisha Ndoa. Baadhi ya sifa za Mwanamke mwenye Hekima – Pia Soma Mithali 31:10-31.
1. Hufumbua kinywa chake kwa hekima, Na sheria ya wema I katika ulimi wake (31:26). Wanawake wengi hawajui kuutumia ulimi vizuri – Ukali, maneno ya mikato, matusi, ukaidi n.k. kwao ni mambo ya kawaida. Wengi wanatawaliwa na HASIRA na WIVU, akiona mumewe anacheka na mwanamke ni Kosa la jinai, mwanamke anafura wala hata hawezi kuongea, hali ya hewa inabadilika hata paka nyumbani wanatambua kuwa hali ni Mbaya.
2. Hufanya kazi kwa Moyo na Huamka alfajiri na mapema
Kuna wanawake ambao ni wavivu kupindukia, inafika wakati hata kutandika kitanda anamtuma House Girl, wanaume ni rahisi sana kuvutwa na anayemhudumia kwa ukaribu, House girl akiandaa chakula, mara kitanda, mara maji ya kuoga, mara apige deki chumbani n.k. Haichelewi mwanaume kulipa fadhila kwa wema anaotendewa.
3. Ni msafi na anajua kuandaa mavazi yanayofaa kwa familia yake
Kuna wanawake ambao ni wachafu – usishangae kukuta sufuria kwenye makochi, chumba cha kulala ni stoo ya nepi za mikojo na nguo chafu, wengine kuoga ni anasa. Mwanamke ni MAJI, sharti mwanamke awe msafi muda wote. Wanaume wote wanapenda Usafi, marashi hata ya mchina yasikose, Mwanamke hakikisha “Reception” inakuwa Safi na kuwa katika hali ya kumfanya Mume ajisikie kujipumzisha kwa Raha mstarehe.
4. Jali na timiza Mahitaji ya NDOA kwa mume wako
Sulemani anasema mwanamke mwema “Taa yake haizimiki usiku”, kuna wanawake wavivu kwa swala hili, pia kuna wanaopenda kulipa visasi kwa kuwanyima waume zao huduma, utakuta wiki nzima mama apanda kitandani huku amevaa “KOMBATI” utafikiri ni askari anaenda vitani. Wanaume ni sawa na Mbuzi ambao hawachelewi kukata kamba wakikosa majani walipofungiwa. Fanya makosa yote, lakini usijefanya ujinga wa kumkomoa mume kwa kumnyima huduma ya Ndoa, hilo ni kosa la Jinai. Hakikisha huduma hizo zinaboreshwa, nenda na wakati ili mradi isiwe kinyume na taratibu za Mungu.
5. Mwanamke anatakiwa kujua kupika chakula kitamu, ambacho familia itafurahia.
Wanawake wengi hasa wa siku hizi hawajui kupika, ndio maana utakuta wanaume wengi wanaishia kula hotelini au kwa mama ntilie, kama umetoka bara basi usione aibu kujifunza kwa watu wa pwani namna ya kuunga NAZI kwenye chakula. Akina mama ni wajibu wao kujifunza Mapishi, Mchicha peke yake unaweza kuwa na mapishi zaidi ya 10, wanaume wanapenda chakula chenye ladha “Test”, mfanye mume akumbuke chakula cha nyumbani.
6. Mwamini Mume wako, wivu na hisia mbaya ni adui wa ndoa yako. Usitoe siri za ndoa yenu kwa mashoga au ndugu zako. Muda wote muombe Mungu akupatie hekima ya kuongea pindi tatizo linapotokea, Muombee mume wako ili Mungu amsaidie pia awe na Hekima ya kutunza Ndoa kwa Uadilifu na Upendo.
No comments:
Post a Comment