imewahi kutokea ukawa na mgogoro na mfanyakazi mwenzako au hata kundi fulani la wafanyakazi wenzako,bosi wako nk? J,umewahi kushuhudia wafanyakazi wenzako wakiwa katika mgogoro au kutokuelewana kiasi kwamba wote hapo kazini mkakosa amani? Iwe ni wewe mwenyewe ulikuwa katika mgogoro au umeshuhudia wafanyakazi wenzako wakikosa kuelewana,ni imani yangu kwamba hukufurahishwa na jambo lile.
Tangu uchumi wa dunia ulipotetereka,tafiti mbalimbali zimeonyesha kwamba migogoro katika sehemu za kazi nayo imeongezeka maradufu.Wana-saikolojia wanaihusisha hali hiyo na wasiwasi uliowakumba wafanyakazi wengi kuhusu kutokuwa na uhakika wa nini kitatokea kesho(fear of uncertainity)
Haishangazi kuona kwamba,leo hii,jinsi ya kutatua migogoro mbalimbali inayoweza kutokea makazini ni mojawapo ya majukumu makubwa ya mameneja,wakurugenzi na pia wafanyakazi wenyewe. Tafiti mbalimbali zinaonyesha kwamba asilimia 24-60 ya muda makazini hutumika katika kutatua migogoro. Isitoshe,migogoro isiyokwisha katika sehemu za kazi matokeo yake huwa ni utendaji mbovu wa kazi, viwango hovyo vya utoaji wa huduma na kama ni sehemu ya biashara basi ni hasara au upotevu mkubwa wa hela.
Bila shaka ndio maana swali la ni hatua gani utazichukua ili kutatua migogoro mbalimbali inayoweza kujitokeza katika sehemu ya kazi ni mojawapo ya maswali yanayoulizwa zaidi wakati wa usaili(interview).
Leo ningependa tukumbushane mambo ya kufanya au kutofanya ili kuepuka migogoro makazini.Mambo ya kufanya au kutofanya ili kuepuka migogoro yaweza kuwa mengi sana.Mimi nitaongelea 8 kama ifuatavyo.Nakukaribisha ndugu msomaji,uongeze(kupitia njia ya maoni/comments) njia mbalimbali ambazo pengine umewahi kuzitumia au unatambua kwamba zinasaidia katika kuepusha migogoro makazini;
- Punguza Kuongea: Maongezi ni jambo zuri. Lakini maongezi yakizidi huwa na tabia ya kuleta matatizo. Bahati mbaya zaidi ni kwamba punde maneno yakishakutoka,huwezi kuyarudisha.Utaomba msamaha,utaambiwa umesamehewa lakini ukweli ni kwamba ulichokisema kitabakia vichwani mwa mfanyakazi au wafanyakazi wenzako daima milele.Jitahidi kufikiri kwanza kabla ya kuongea.Njia pekee ya kuweza kufanya hivyo ni kuongea taratibu na kwa mpangilio.Kwanza utasikika vizuri zaidi na pili utaepuka migogoro inayoanzia kwenye maneno.
- Epuka Umbea: Umbea na majungu ni chanzo kikubwa cha migogoro makazini. Sasa kama wewe ni mwanaume usidhanie kwamba hili halikuhusu. Umbea na majungu ni kwa wanaume na wanawake ingawa kuna tofauti kidogo za kitakwimu linapokuja suala la nani zaidi.Kwa vyovyote vile jiepushe na umbea au majungu kuhusu mfanyakazi au wafanyakazi wenzako.Jitahidi kufanya kazi yako kwa bidii na maarifa. Isitoshe huo ndio mwanzo wa kuheshimika.Hautoheshimika kwa kuwa msambazaji wa maneno ya uongo na matukio ya kutunga.
- Subiri,tafakari kisha tenda: Makazini,kama zilivyo sehemu zingine ambazo binadamu hukutana,kupishana,kutofautiana kimavazi na kimawazo,huwa inatokea. Watu hukosa kuelewana.Inapotokea hivyo usikurupuke katika kuelezea malalamiko yako,mawazo yako au hata maoni yako.Unapojipa muda wa kutafakari unachotaka kukisema au kurekebisha, unajipa nafasi ya kuwa sahihi zaidi mara utakapoamua kutenda. Fanya utafiti wa kina kabla ya kusema.Kwa kufanya hivyo utaheshimika zaidi na pia utaepusha migongano isiyo ya lazima.Nasema isiyo ya lazima kwa sababu naamini kwamba wakati mwingine mashauri hujitokeza kwa nia njema ya kuwekana sawa.
- Sikiliza,usibishe: Imeshawahi kukutokea mfanyakazi mwenzako au bosi wako akakujia juu na kukulalamikia kwa kosa au kitu ambacho hujui chanzo wala mwisho wake na zaidi unaamini kabisa hujakosea wala kutenda jambo lolote baya? Hali hiyo inapokutokea huwa unafanya nini? Wengi wetu huwa tunaanza kwa kubisha na kujaribu kwa nguvu zetu zote kuhakikisha kwamba anachokisema mfanyakazi mwenzako au bosi wako sio kweli bali uongo mtupu.Bahati mbaya njia hii mara nyingi hutufikisha pabaya zaidi. Wakati mwingine watu hurushiana hata ngumi! Badala yake sikiliza kwa makini unachotuhumiwa nacho na kisha taratibu sema “Nasikitika kusikia kwamba unadhani mimi ndiye niliye…”.Kisha mueleze mwenzio au bosi wako ukweli au unachokijua kuwa ukweli. Mara nyingi ukishampa mtu nafasi ya kusema kila kitu kilichoko moyoni mwake, hasira humpotea na akili timamu hurejea na hivyo mazungumzo yenye kujenga huwezekana.
- Weka nukuu ya kila kitu: Binadamu wa kawaida ana mambo chungu mbovu kichwani kwake. Sio rahisi kukumbuka kila kitu kinachotokea iwe ni kazini, mitaani na hata majumbani. Kwa bahati mbaya mambo mengi yanayotokea kazini huwa yana thamani kubwa zaidi ya kukumbukwa. Jitahidi kuweka kumbukumbu ya kila kitu unachokiona,ulichoambiwa na wakuu wako wa kazi,mfanyakazi/wafanyakazi wenzako nk. Hiyo itakusaidia siku mgogoro utakapokuwa unafumuka. Kumbukumbu sahihi zitasema ukweli na pia zitaonyesha jinsi gani ulivyo makini katika kazi yako.Kumbukumbu sahihi zitakuepusha na mgogoro usio wa lazima baina yako na mfanyakazi mwenzako au hata utawala wa sehemu yako ya kazi.
- Weka mipaka: Kila binadamu ana mipaka yake.Kama hauna basi nakushauri uanze leo kujiwekea mipaka. Kwa upande wangu mojawapo ya mipaka ambayo huwa sina uvumilivu nayo sana mtu anapoivuka ni “unafiki”.Sipendi mtu/watu wanafiki”.Una jambo unataka kuliongelea kuhusu mimi,basi jitahidi tu kuniambia bila kuficha na kusemeasemea pembeni. Katika maeneo ya kazi ni muhimu kujiwekea mipaka ya mahusiano ya kikazi. Tambua majukumu yako,tambua wajibu wako.Majukumu yaw engine na wajibu wao,waachie wenyewe. Kumbusha majukumu na wajibu kama nafasi yako inakuruhusu kufanya hivyo.
- Heshima na ubinadamu: Sasa niliposema hapo juu kwamba weka mipaka sikumaanisha kwamba uishi katika “dunia ya peke yako” mbele ya wafanyakazi wenzako. Jitahidi kuwa na mahusiano bora kabisa na wafanyakazi wenzako.Wajulie hali,wasalimie,wasaidie inapobidi,shiriki katika kila shughuli ya kazini(ndani na nje ya sehemu ya kazi).Usije ukaacha kushiriki shughuli kama misiba,harusi,ubarikio nk.Kumbuka maisha ni kushirikiana.
- Usijaribu kuwabadili wenzako,badilika mwenyewe: Wapo binadamu ambao kila kukicha wao hujaribu kuwabadilisha wenzao? Kama wewe ni miongoni mwa watu wa namna hiyo,nasikitika kukuambia kwamba kazi kubwa ipo mbeleni mwako. Sio jambo rahisi kumbadili mtu. Ni sawa kabisa na kupoteza muda. Badala yake,jaribu wewe kubadilika.Kama mfanyakazi mwenzako ni ile aina ya watu wanaopenda kusifiwa sifiwa,msifu kisha ishia zako.Kwani utapungukiwa na nini?
Mwisho,kumbuka mambo kadhaa ya msingi.Upendo, heshima na uvumilivu. Mambo hayo ndio msingi wa kwanza wa mafanikio na siri ya kuepusha migogoro makazini. Mpende kila mtu(hata kama unadhani hapendeki),mheshimu kila mtu bila kusahau kujiheshimu wewe mwenyewe.Jitahidi kuwa mvumilivu.Kila mtu anastahili kuvumiliwa, ukiwemo wewe na mimi pia. Kazini ni sehemu ya kujitafutia riziki,kujenga mahusiano bora ya kibinadamu,kujiendeleza,kuwaendeleza wengine na muhimu zaidi kujifunza na siyo sehemu ya kutengeneza migogoro.
No comments:
Post a Comment