Thursday, 2 May 2013

Kwaheri Mutula Kilonzo; wakili wa Moi...........


Wakili Mutula Kilonzo akizungumza wakati wa uhai wake.Picha na Maktaba 

“Sisi wataalam tumefanya uchunguzi wa kina kwenye mwili wake, tunahitaji kupewa muda wa kupitia uchunguzi huo. Ninaamini kuwa kwa siku nane tutakuwa tumefanikiwa na kujua ni kitu gani kilichosababisha kifo chake. Siyo siri, tutasema na kuweka wazi sababu za kifo hiki. Inafaa msubiri, mtajua sababu hizi.”


Kama ni kifo, basi hiki cha Mutula Kilonzo kinashtua. Mshtuko huo ni mfululizo wa matukio ya ajabu ya vifo vya wanasiasa wa Kenya.
Yeye (Mutula), Seneta wa Makueni alikuwa ndiyo kwanza amechaguliwa katika uchaguzi wa Machi 5 mwaka huu kwa tiketi ya Chama cha Wiper, kilichogawanyika kutoka Orange Democratic Movement (ODM-Kenya).
Alifariki  ghafla Jumamosi   ya Aprili 27 mwaka huu na kuingia pengine katika orodha ya kina Tom Mboya, Dk Robert Ouko au hata Profesa George Saitoti, ambao wote vifo vyao bado vina utata.
Ingawa vifo vya  watangulizi wake kila kimoja kimekuwa na sababu zake ambazo nyingine hadi leo ni vigumu kuzieleza, hiki cha wakili Mutula kimeacha maswali.
Ni utata huo ambao umeifanya familia yake kutaka kifo hiki kichunguzwe kwa kina.
Uchunguzi huo umefanyika kwa saa nane, umefanywa na wataalamu waliobobea na matokeo yake yanasubiriwa kwa wiki nane zijazo.
“Imetuchukua muda mrefu kufanya uchunguzi, tulitaka umakini,” anaeleza Mchunguzi Mkuu wa Serikali, Dk Johansen Oduor.
Dk Oduor anaeleza kuwa uchunguzi na majaribio mengi yalihitajika ili kupata sababu ya kifo hiki cha ghafla.
Mtaalamu huyo (Dk Oduor) anasema kwamba sampuli kadhaa zitafanyiwa majaribio, uchunguzi na wataalam waliobobea na matokeo hayatakuwa siri.
Aliongeza:”Sisi sote, wachunguzi saba, tumefanya kazi hiyo, tumekubaliana katika hilo. Lakini, tusubiri, tuone matokeo, tunazo wiki nane.”
Kwanini uchunguzi ?
Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka wa Serikali (DPP), Polisi, wameafiki na kutaka kufahamu pasi na shaka kama kulikuwa na mchezo mchafu katika kifo hicho.
Familia yake ikamwalika mchunguzi kutoka Uingereza  ambaye alikuwa Afrika Kusini. Aliwasili  Nairobi mapema na kushiriki katika uchunguzi wa kifo huku mwili wa Mutula ukitarajiwa kuzikwa Mei 9.
Mchunguzi huyo, Dk Ian Madison Calder, pia kama Dk Oduor alisema kwamba wamekubaliana na wenzake.  “Tumekubaliana, matokeo yatachukua muda mrefu hadi kupatikana.”

No comments:

Post a Comment