Tutakaa na kuamua nini cha kufanya kwa kuwa tayari ‘deadline’ (muda wa mwisho), yetu imeshafika na kauli ya Warioba tumeshaisikia na hawajafanya tuliyoyataka hivyo tutakaa na kutoa uamuzi mwingine,” Dk Slaa.
Sina mpango wa kujitoa kwenye Tume kwa kuwa nimekula kiapo kwa ajili ya Watanzania, hadi sasa sijaona sababu ya kutaka kujitoa, alisema Profesa Baregu.
Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeshindwa kutoa kauli kuhusu kujitoa kwake kwenye mchakato wa Katiba Mpya baada ya muda kilioutoa kwa Serikali kutaka kurekebishwa kwa baadhi ya mambo katika mchakato huo kumalizika juzi.
Mwenyekiti wa Chadema na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe alisema bungeni Aprili 11, mwaka huu kuwa chama chake kitajitoa katika mchakato huo endapo mambo muhimu mawili hayatapatiwa ufumbuzi hadi kufikia Aprili 30, mwaka huu.
Mambo hayo ni kufutwa kwa uchaguzi wa wajumbe wa mabaraza ya wilaya ya katiba uliofanywa na Kamati za Maendeleo za Kata (WDC), badala yake wachaguliwe moja kwa moja na wananchi wa kata husika bila kuchujwa na kamati hizo.
Hata hivyo, hivi karibuni Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba alisema tume haiwezi kufanya kazi kwa shinikizo la wanasiasa na kwamba itafuata mwongozo uliopo ambao utaisaidia nchi kupata Katiba ya Watanzania.
Kauli hiyo imepingwa na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilbrod Slaa ambaye amemtaka aanze kukikanya CCM akidai kuwa kimepanga mkakati wa kuhakikisha inapatikana Katiba Mpya yenye masilahi kwa chama hicho.
“Tuna ushahidi jinsi CCM inavyoshiriki kuharibu mchakato wa Katiba na sasa tunajipanga kufanya vikao vyetu vya ndani, baadaye tutatoa tamko zito tukieleza jinsi hawa watu wanavyofanya mchezo wao,” alisema Dk Slaa.
Kuhusu ahadi ya kujitoa katika mchakato wa Katiba Aprili 30, alisema Mbowe alitoa kauli bungeni kutokana na vikao vya nyuma vya chama hivyo kauli nyingine itatolewa baada ya vikao vingine.
“Tutakaa na kuamua nini cha kufanya kwa kuwa tayari ‘deadline’ (muda wa mwisho), yetu imeshafika na kauli ya Warioba tumeshaisikia na hawajafanya tuliyoyataka hivyo tutakaa na kutoa uamuzi mwingine,” alisema Dk Slaa.
Hata hivyo, taarifa zinaeleza kuwa tayari chama hicho kimeshafanya uamuzi wa kujitoa katika mchakato huo baada ya madai yao kushindwa kutimizwa na kimemtaka Mjumbe wake wa Kamati Kuu, Profesa Mwesiga Baregu ajitoe kwenye Tume.
Akizungumzia hilo, Dk Slaa alisema hawezi kuzungumzia masuala ya kujitoa kwa Profesa Baregu... “Mimi nazungumzia masuala ya chama.”
Alipoulizwa kuhusu uamuzi huo, Profesa Baregu alikiri kuelezwa kwa mdomo kuwa chama kimefikia uamuzi huo lakini akasema hautakisaidia chama wala nchi hivyo akashauri Kamati Kuu irejee upya uamuzi wake.
No comments:
Post a Comment