Wednesday, 29 May 2013

Makinda:Kaa chini, nakwambia kaa chini


Spika wa Bunge Anne Makinda akizungumza wakati wa kikao cha Bunge,jijiniDodoma.
UBABE wa Spika wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Anne Makinda jana ulihamia kwa Mbunge wa Kawe (Chadema) Halima Mdee,wakati Mbunge huyo alipotoa hoja ya kutaka kauli ya serikali kuhusu tabia za vigogo kumiliki mashamba makubwa yasiyo endelezwa.
Mdee alitoa hoja hiyo wakati wa kujadili hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambayo ilihitimishwa bungeni jana. Mdee alivutana na Spika Makinda wakati wa kujadili bajeti hiyo kifungu kwa kifungu.
Katika hoja hiyo Mdee alitaka kufahamu kauli ya Serikali kuhusu kampuni zinazomiliki ardhi bila kuziendeleza na hatua zinazochukuliwa kuhakikisha zinarudishwa kwa Wananchi.
Swali hilo lilimfanya Spika Makinda atumie mamlaka yake na kumwamrisha Mbunge huyo wa Kawe akaye chini kwa kuwa hoja yake haina mashiko ya kufanya hivyo na kwamba kama anataka aiwasilishe kama hoja binafsi.
“Kaa chini, nakwambia kaa chini,” alisema Makinda huku Mdee akionekana kuendelea kuzungumza... “Nasema kaa chini,” alirudia na Mdee kukaa huku akikipeperusha karatasi hewani kuonyesha kutokubaliana naye.
Awali, Mdee alisema shamba la simanjiro ambalo Halmashauri ya wilaya hiyo ilipendekeza mwekezaji kupewa ekari 500 lakini Wizara ya Ardhi iliidhinisha ekari 25,000 ambazo mwekezaji hajaziendeleza zote wakati mashamba ya Kisarawe na mashamba ya mkonge Tanga ambayo wawekezaji wameyakopea fedha nayo hadi sasa hayajaendelezwa. 
Alitaka kauli ya Serikali kuhusiana na hali hiyo na jinsi ya kurudisha mashamba hayo katika miliki ya umma. Mbunge mwingine aliyetishia kutoa shilingi ni Dk Faustine Ndungulile wa Kigamboni (CCM), akijikita katika suala la ujenzi wa mji mpya wa Kigamboni akisema wananchi wake hawakushirikishwa katika mipango ya ujenzi huo. Akijibu hoja hizo, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka alisema wananchi wameshirikishwa kikamilifu katika mchakato mzima na kuahidi kukaa na mbunge huyo pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Fredrick Werema kuzungumzia suala la Kigamboni

No comments:

Post a Comment