Dodoma. Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Lediana Mng’ong’o amelitaka Bunge kupiga marufuku unywaji wa pombe kali zinazowekwa katika pakiti maarufu kwa jina la viroba akisema zinaharibu vijana wa shule na madereva ambao ni nguvukazi ya taifa.
Akichangia mjadala wa Bajeti wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii juzi, Mng’ong’o alisema pombe hiyo inahatarisha afya za Watanzania kwa kiasi kikubwa. Alisema madereva wamekuwa wakiendesha magari huku wakinywa viroba na wanafunzi wamekuwa wakienda darasani baada ya kunywa pombe hiyo.
Alisema Serikali inapaswa kufuata nyayo za Kenya na Uganda ambazo zimepiga marufuku pombe hiyo.
Pombe hiyo ya pakiti imekuwa ikitumiwa na watu wengi kutokana na kuuzwa bei ya chini kati ya Sh500 na 1,000.
Gazeti hili liliwahi kuandika habari ya athari ya pombe ya viroba na ilibainika kuwa watu wengi walikuwa wanatembea wakiwa wamelewa huku wauzaji wakisema ndiyo biashara inayofanya vizuri zaidi.
Mbali ya viroba, Mng’ong’o pia aliitaka Serikali kutatua changamoto zinazowakabili watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi, ambao alisema wanakabiliwa na unyanyapaa, lishe duni na wanakosa dawa.
“Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo watoto wana lishe duni zaidi. Kwa mfano, takwimu zinasema kuwa asilimia 42 ya watoto wote wana lishe duni,” alisema na kuongeza kuwa lishe duni inasababisha watoto wasiwe werevu darasani na kuwa na malezi duni.
Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Roswita Kasikila alielezea kukerwa kwake na deni la Sh52 bilioni ambalo Bohari ya Dawa (MSD) inaidai Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii akisema linaifanya bohari hiyo kuwa dhaifu kiutendaji.
“MSD inafanya kazi kama mama lishe, mpaka iuze dawa ndipo inunue dawa nyingine? Ndiyo maana inashindwa kufanya kazi vizuri,” alisema Kasikila.
Aliitaka Serikali kulipa deni hilo ili MSD inunue dawa na vifaa tiba vya kutosha kwa ajili ya kuimarisha huduma za afya nchini.
Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalumu (CUF), Magdalena Sakaya alimtuhumu Mganga Mkuu wa Kituo cha Afya Kombe, Kata ya Usinde, Tabora akisema ana tabia ya kulewa akiwa kazini na kuwauzia wajawazito kadi za kliniki.
Sakaya alisema daktari huyo baada ya kushtakiwa kwa tabia zake za kuuza kadi za kliniki na kulewa akiwa kazini, aliwalipizia kisasi waliomshtaki kwa kukataa kuwatibu.
No comments:
Post a Comment