Hebu tutafakari mahusiano ya muda mrefu au mahusiano yanayopelekea ndoa!
Kama mnapenda mapenzi yenu yadumu hadi pale “kifo kitakapo watenganisha”,basi ni bora kuhakikisha kwamba mahusiano ama mapenzi yenu yamejengwa katika msingi mkuu na imara ambao ni – URAFIKI.
URAFIKI ni msingi muhimu katika kutengeneza mahusiano imara na yenye mafanikio. Bila urafiki hamna lolote. Mambo mengine ni ya muhimu pia katika mahusiano, bila ya shaka, lakini unahitaji ya ziada ili kuweza kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika maisha ya mahusiano ambazo hakuna mtu ambaye anaweza kuzikwepa.
Kama mtu binafsi unapaswa kuboresha uwezo wako binafsi pale inapokuja suala la mahusiano. Badala ya kuangalia zaidi upande wa pili wa kutafuta mshirika wa mahusiano ni vyema zaidi ukatumia muda mwingi kutafakari ni aina gani ya mtu ambaye unatarajia kujenga naye urafiki. Kujenga urafiki ndiyo hasa mwanzo wa mahusiano. Ni kushirikiana zaidi kwa kufahamiana, kujuana, kufahamu malengo yenu katika maisha, thamani yenu na yale ambayo kila mmoja wenu anayapendelea ama hapendezwi nayo. Pamoja na mambo mengine mengi mazuri ambayo yatawafanya kuwa wa pekee.
Kuna muda wa kutosha sana katika maisha ya mahusiano kwa ajili ya mapenzi na kujitoa kwa mwenzako, hakuna haja ya kukimbilia hayo!
Ni kweli kwamba kadiri unavyo ahirisha kujiingiza katika mapenzi na kujenga urafiki, ndivyo jinsi ambavyo utaweza kujenga mahusiano yaliyo bora na mwenzi wako wa baadaye katika maisha. Kwa mwenendo huo mtajifunza na kuona kama mnaendana na mko tayari kila mmoja kwa mwenzake.
Hivyo basi kama itakuwa hamuendani ama mmoja hayuko tayari kwa mahusiano hayo ni rahisi kuachana huku kila mtu akiwa na utu wake kama mlivyokutana!
Kujenga msingi imara ni muhimu, mara baada ya kuujenga ni rahisi kuendelea kutengeneza maisha na mahusiano mazuri juu ya msingi huo. Chukua muda, fahamianeni, jengeni urafiki ambao mtaweza kuuenzi kwa muda wa miaka mingi katika maisha yenu na hatimaye kuweza kuwa na maisha bora ya mahusiano yenye mafanikio na faida kwa maisha ya pande zote husika.
No comments:
Post a Comment