Saturday 4 May 2013

Rufaa ya ‘mbunge wa CCM’ sasa yaiva....


Dar es Salaam. Hukumu ya rufaa ya aliyekuwa mbunge wa Sumbawanga Mjini kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Aeshi Hilary, sasa imeiva.
Habari tulizozipata jana kutoka Mahakama ya Rufani, zinasema kuwa jopo la majaji watatu waliosikiliza rufaa hiyo tayari limeshakamilisha kuandika hukumu hiyo na kwamba imepangwa kutolewa keshokutwa Jumatatu.
Hilary alivuliwa ubunge huo na aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo , Bethuel Mmila, April 30, 2012, kutokana na kesi ya uchaguzi iliyofunguliwa na aliyekuwa mgombea wa kiti hicho katika Uchaguzi Mkuu 2010, Nobert Yamsebo wa Chadema akipinga uhalali wa matokeo yaliyompa ushindi.
Katika hukumu yake, Jaji Mmila pamoja na mambo mengine, alikubaliana na madai ya Yamsebo (mjibu rufaa), kufanyiwa vurugu zilizozuia mikutano yake na kampeni katika vijiji viwili, huku pia akimtuhumu Hilary kutoa rushwa.
Hata hivyo, Hilary alikata rufaa katika Mahakama ya Rufani kupinga hukumu hiyo, huku Mwanasheria Mkuu wa Serikali naye akikata rufaa kupinga hukumu hiyo.
Rufaa hizo zilisikilizwa kwa pamoja April 19 na jopo la majaji watatu, likiongozwa na Jaji Edward Rutakangwa, akisaidiana na Jaji Profesa Ibrahimu Juma na Jaji Steven Bwana.
Wakati wa usikilizwaji wa rufaa hizo, mawakili wake Hillary wakidai kuwa kesi iliyomvua ubunge ilikuwa ni batili kwa kuwa ilisikilizwa kinyume cha sheria.
Madai hayo yalitolewa na Wakili Mkuu wa Serikali, Michael Luena akisaidiana na Wakili wa Serikali, Karim Rashi, kwa niaba ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, na Richard Rweyongeza, Juma Nassoro na Abubakar Salum wanaomtetea Hilary.
Mawakili hao walifafanua kuwa kesi ilisikilizwa kabla ya mlalamikaji kuweka mahakamani dhamana ya kesi hiyo kisheria kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 2010 na kwamba haikupaswa kusikilizwa, badala yake ilisikilizwa kimakosa.
Wakili Rashid alidai kuwa kwa mujibu wa mwenendo wa maombi ya kupangiwa dhamana ya kesi, maombi hayo yaliamuriwa katika muda wa siku 42, badala ya siku 14 kama kifungu cha 111 (3) cha sheria hiyo kinavyoelekeza.
“Hivyo tunaomba Mahakama itengue uamuzi wote uliofikiwa na Mahakama Kuu Sumbawanga kwa kusikiliza kesi hiyo bila kuwapo “security for cost.”, alidai Wakili Rashid.
Kwa upande wake, Wakili Rweyongeza alidai kuwa hata hati ya dhamana ya kiwanja iliyowasilishwa mahakamani hapo na aliyekuwa mlalamikaji, hazikuwa nakala halisi na kwamba haikuwa imesajiliwa, kinyume cha matakwa ya Sheria.

No comments:

Post a Comment