Monday, 13 May 2013

Watuhumiwa wa bomu Arusha wameachiwa huru.

.

SIKU moja baada ya Mabalozi wa nchi za Falme za Kiarabu UAE na Saudi Arabia kuitaka serikali ya Tanzania kutoa maelezo ya kina kutokana na hatua ya raia wake kukamatwa kwa  tuhuma za kigaidi, Jeshi la Polisi Tanzania leo, limetangaza kuwaachia huru raia hao kwa madai kwamba hawakuhusika katika tukio hilo.

Mei tano mwaka huu Magaidi walilipua kanisa la Katoliki Parokia ya Olasiti jijini Arusha na kuua watu watatu, kujeruhi watu zaidi 62, ambapo katika uchunguzi wa awali Askari wa Jeshi la Polisi waliwakamata raia hao wa nchi za Falme za Kiarabu,Saudi Arabia  pamoja na watanzania wanne wakituhumiwa kuhusika katika shambulio hilo la kigaidi.

Akizungumzia na Waandishi wa habari jijini Arusha leo Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi wa Polisi Liberatus Sabas alisema kwamba Jeshi la Polisi limewaachia huru watuhumiwa wanne waliokuwa wakichunguzwa kuhusika katika tukio hilo.

"Raia wanne wa nchi za nje waliokuwa wakishikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kigaidi wa ulipuaji bomu katika Kanisa la Olasiti wameachiliwa huru baada ya kubainika kwamba hawakuhusika katika tukio hilo"alisema Sabas na kuongeza: Raia hao ni pamoja na  Said Abdalla Said (28), Abdulaziz Mubarak (30) na Said Mohsen wote kutoka  Falme za Kiarabu (UAE),wakati Jassini Mbaraka (29) anatokea Saudi Arabia".

Kamanda Sabas pia alisema kwamba  watuhumiwa wengine watukio hilo ambao ni watanzania wakiongozwa na George Batholomeo Silayo (23), mfanyabiashara na mkazi wa Olasiti, Arusha, Mohamed Sulemani Said (38) mkazi wa Ilala, Dar es Salaam na Jassini Mbaraka (29) mkazi wa Arusha wamefikishwa Mahakamani kujibu tuhuma zinazo wakabiri. 

No comments:

Post a Comment