Rais wa Uganda, Yoweri Kaguta Museveni akitia saini muswada wa sheria dhidi ya wapenzi wa jinsi moja kwenye Ikulu ya Entebbe juzi. Muswada huo sasa unakuwa sheria kwa ajili ya kutumika kuwashughulikia watu wenye hulka hiyo. Picha na Daily Monitor.
Kampala. Siku moja baada ya Rais Yoweri
Museveni kusaini sheria inayotoa adhabu kali kwa wapenzi wa jinsi moja,
Marekani imesema inaangalia upya uhusiano wake na nchi hiyo kama
ilivyoainisha awali.
Katika taarifa yake iliyotolewa jijini Washington
DC jana, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry alisema Serikali
ya Rais Barack Obama itahakikisha ushirikiano wowote na Uganda
utachujwa kupitia sheria za kupinga ubaguzi ambazo inazisimamia.
“Sheria imeshapitishwa, tunaanza kuchuja uhusiano
wetu na Uganda kwa kuangalia mambo muhimu, ikiwemo maeneo
tunayowawezesha,” alisema Kerry katika taarifa yake jana.
Awali, akitia saini muswada huo kuwa sheria juzi,
Rais Museveni alipuuza vitisho vya Marekani na kusema mataifa ya nje
ambayo yamekuwa yakimtaka asisaini muswada huo pamoja na viongozi wa
kidini hawana nafasi katika mambo ya ndani ya nchi yake.
“Watu kutoka nje hawawezi kutuamuru tufanye au
tusifanye mambo yetu. Kama hawataki kwenda nasi, basi wanaweza kuchukua
misaada yao,” alisema.
Akizungumzia onyo lililotolewa na baadhi ya
viongozi wa kidini akiwemo Askofu Desmond Tutu wa Afrika Kusini,
Museveni alisema: “Kumbuka hata Yesu aliuawa na maaskofu, ndiyo maana
huwa sisikilizi watu hao (viongozi wa kidini).”
Mataifa ya Afrika yenye sheria kama iliyopitishwa Uganda
Wakati Marekani na baadhi ya washirika wao
wakitishia kuzuia misaada kwa Uganda, mataifa mengi ya Afrika, isipokuwa
Afrika Kusini yana sheria kali za kupiga marufuku wapenzi wa jinsi
moja. Sheria zimekuwa zikitekelezwa kwa muda mrefu sasa.
Shirika la Haki za Binadamu, Amnesty International
linasema uhusiano wa kimapenzi wa watu wa jinsi moja umeharamishwa
kisheria katika nchi 38 kati ya 54 barani humo na adhabu ya kifo
imehalalishwa nchini Mauritania, Sudan na Somalia.
Nchi zilizoweka sheria kali kuwabana wapenzi wa
jinsi moja ni pamoja na Uganda ambayo imepiga marufuku wapenzi wa jinsi
moja na kutoa adhabu ya hadi kifungo cha maisha gerezani kwa wale
wanaorudia vitendo hivyo.
Sheria hiyo inazuia kutangaza masuala yahusuyo wapenzi wa jinsi moja na kuwataka watu kuwatenga na kuwakataa mashoga.
Nigeria, pia imeweka sheria maalumu iliyoanza
kutekelezwa Januari mwaka huu. Sheria hiyo inatoa adhabu ya kifungo cha
hadi miaka 14 jela kwa wapenzi wa jinsi moja wanaoishi pamoja.
No comments:
Post a Comment