KUNA mambo unapaswa kuyaweka mbali sana. Hakikisha hayaingii kwenye
mapenzi yako. Kuyafanya, maana yake unakuwa unauchimbia kaburi uhusiano
wako mwenyewe.
Tunapenda kuongozwa na fikra zetu. Kila mmoja anataka
mwongozo wa maisha yake uendane na halmashauri ya ubongo wake. Hufanya
hivyo, bila kujua kuwa kuna kikomo fulani ndani yake. Akili na matakwa
ya moyo, wakati mwingine vinaweza kukupoteza.
Moyo unaweza kumpenda
mchawi na ukawa huelewi kitu kwa chochote utakachoambiwa. Penzi la
jambazi likikuingia, serikali ndiyo utaiona ni katili kwa sababu
inamsaka mwenzi wako usiku na mchana. Hii ina maana kuwa mapenzi ni
zaidi ya fikra za kila mtu.
Hutokea watu kuachana
wakati bado wanapendana. Migogoro midogo inawafanya watengane, matokeo
yake kila mmoja anabaki akiumia kivyake.
Huo ni mfano mmoja kati ya
mingi inayoonesha kwamba mapenzi yapo juu ya fikra za kawaida. Inahitaji
utulivu wenye mashiko ya sayansi ya saikolojia.
Kuna ambao waliishi
kwa mategemeo ya kuachana. Wakiamini wamechokana, matokeo yake kwenye
ubongo wao wakatengeneza maneno: “Ipo siku.” Hata hivyo, miezi na miaka
ikakatika mpaka wakazikana. Kumbe Mungu aliwaandikia wawe pamoja mpaka
kifo ila wao hawakujua.
Dosari ya aina hiyo inatokana na wawili
wanaopendana lakini upendo wao ukapofushwa na migogoro ya hapa na pale.
Nasisitiza kuwa watu ni lazima wagundue mapema matatizo yao kabla ya
kuhisi kwamba kati yao hakuna mapenzi. Vilevile, kila mmoja amuelewe
mwenzi wake ni binadamu na siyo malaika.
Ana mapenzi naye, tena
mapenzi makubwa. Hata hivyo, hiyo haimfanyi awe malaika. Ni binadamu,
kwa hiyo wakati anadumisha mapenzi yake, anaweza kufanya makosa mengi.
Jaribu kumvumilia kwa sababu ameumbwa na udhaifu, hajakamilika.
Baada
ya utangulizi huo, ni vizuri kujua kuwa yapo makosa ambayo wengi
huyafanya, tena mara nyingi bila kujua. Tunaishi nayo, matokeo yanakuwa
ni mazoea. Hata hivyo, mara nyingi hutokea yanaharibu uhusiano ndiyo
maana nimechagua tuyajadili. Yafuatayo ndiyo makosa yenyewe:
KULICHEZEA KAMARI PENZI LAKO NA MAISHA YAKO
Hapo
ulipo hujawahi kuona mtu anapambana kuhakikisha mwenzi wake anabadilika
tabia? Bila shaka tayari ulishajionea. Je, umejifunza nini kutoka kwao?
Ni kweli kabisa kwamba mwenzi wako si malaika, kwa hiyo mnapokutana
lazima mtatofautiana, je, ikitokea hamuendani kabisa?
Umejitahidi
kumuweka kwenye mstari unaotaka lakini mwenzako haendi. Unasubiri nini?
Kung’ang’ania penzi la mtu ambaye huendani naye, ni sawa na kuuchezea
kamari moyo wako, vilevile ni sawa na kuyachezea karata tatu maisha
yako.
Upo na mwenzi wako ambaye hakutoshelezi. Mnakutana mara nyingi lakini hakufikishi pale unapotaka upelekwe na mwandani wako.
Unanyamaza
tu kwa imani kuwa ipo siku ataweza, siku zinakwenda na mabadiliko
hayaonekani. Unajipa matumaini kedekede kwamba kuna siku nyoka ataota
miguu na jongoo atakuwa na macho.
No comments:
Post a Comment