Kuna
ndoa ambazo ukizifuatilia zinasikitisha sana. Ni ndoa ambazo furaha
imetoweka, yaani kila mmoja yuko kwenye ndoa ili mradi tu yupo lakini
hatimizi yale ambayo yanatakiwa kufanywa na mwanandoa.
Upweke
ni jambo linaloumiza sana hasa kwa mtu aliye kwenye ndoa. Kuna dada
mmoja ambaye hivi karibuni nilizungumza naye kuhusiana na maisha yake ya
ndoa. Aliyonieleza yalinisikitisha sana na ndiye aliyenipa mwanga wa
kuandika mada hii.
Anasema: “Mume wangu anafanya kazi ila mimi ni mama wa nyumbani, nashukuru napata mahitaji yote muhimu kutoka kwake.
“Kikubwa ninachokikosa kutoka kwa mwanaume huyu ni penzi. Amekuwa ni mtu
ambaye yuko ‘bize’ sana, yaani anarudi nyumbani usiku, ukimgusa
anakuambia amechoka sana na anahitaji kupumzika.
“Mbaya zaidi, hata siku ambazo anastahili kuwepo nyumbani ananiambia
anakwenda kwenye mishemishe za kusaka pesa. Wakati mwingine namkubalia
lakini imefika wakati naona ni ‘too much’.
“Yaani sina muda wa kukaa na mume wangu, siku ikitokea hivyo ni kwa muda
mfupi sana hali inayonifanya niikose ile furaha ya kuolewa.”
Dada huyo aliongea maneno mengi lakini kwa kifupi utakuwa unaona ni kwa
jinsi gani anajuta kuolewa licha ya kwamba anapata mambo mengine ya
msingi.
Mapenzi si pesa, mapenzi si kumvalisha na kumlisha mkeo kila
anachokitaka. Mapenzi ni ukaribu wa wewe kwake. Unatakiwa kujua kwamba,
mumeo/ mkeo atajisikia faraja sana ukiwa pembeni yake pale
atakapokuhitaji.
Ni jambo linaloumiza sana kwa mke kukosa muda wa kuwa na mume wake eti
kisa ‘ubize’. ‘Ubize’ huu mpaka lini? Sikatai kuchakarika ndiyo maisha
lakini ndiyo iwe kila siku?
Hiyo furaha ya ndoa itapatikana vipi ikiwa wanandoa wenyewe hawapati
muda wa kuwa pamoja? Hili ni tatizo na kwa kweli tusipoangalia tunaweza
kuwanyong’onyesha wenza wetu bila kujua na mwisho kuwafanya waumie
kimoyomoyo.
Lakini cha ajabu ni kwamba, kama ilivyo kwa wanaume, wapo wanawake pia
ambao wanajifanya wako bize sana na maisha kuliko kuzijali ndoa zao.
Yaani wao wanakutana na waume zao kwenye tendo la ndoa kwa masharti na
tena kwa ratiba. Mapenzi gani haya? Mumeo anataka haki yake unamwambia
umechoka!
Sasa kuna faida gani ya wewe kuolewa? Kama unahisi kazi ni bora kuliko
kumjali mumeo, heri uwe muwazi kwake ili aoe mwanamke mwingine
atakayejali hisia zake.
Kikubwa ninachotaka kusisitiza kwenye makala haya ni kwamba, kila aliye
kwenye ndoa ahakikishe anatenga muda wa kutosha wa kuwa karibu na mwenza
wake bila kujali ubize unaotokana na mishemishe za kimaisha.
Hii itaimarisha ndoa na hakika kila mmoja atafurahia uwepo wa mwenzake.
Tukumbuke hakuna asiyetaka mwenza wake kujishughulisha kwani maisha bila
kuwa bize hayawezi kuwa mazuri lakini sasa ubize huu ukizidi kiasi cha
kumfanya mwenza wako akawa mpweke, inakuwa siyo poa.
No comments:
Post a Comment