NDOA
inafahamika kuwa ni heshima kwa kila mmoja, namaanisha kwa anayeoa na
anayeolewa. Mwanaume akioa, anaheshimika na anajiona ameingia kwenye
majukumu ambayo yanamlazimu atie akili ili aweze kukabiliana nayo.
Kwa wanawake
ndiyo usiseme. Yaani idadi kubwa ya wanawake wanalilia ndoa hasa kwa
wanaume ambao wamewapenda na kuwaamini kwamba wakiwa nao ndani maisha
yao yatakuwa ni ya furaha zaidi.
Kwa kifupi ndoa ni tamu ila kama utaijulia na ni chungu kama utakuwa
umeingia kwenye maisha hayo na mtu ambaye awali alikuwa akijifanya
anakupenda sana lakini baadaye akaamua kutoa makucha yake.
Wapo wanaume ambao leo hii wanalia, wanajuta ni kwa nini waliamua kuwaoa
wanawake ambao wamewaoa. Wanajuta kwa kuwa wanakutana na mambo ya ajabu
ambayo hawakuyatarajia.
Si hivyo tu, wapo wanawake ambao walifurahi walipovishwa pete za uchumba
na hatimaye kuvaa mashela lakini leo hii wanaomba talaka kutoka kwa
waume zao kutokana na mazingira tofauti wanayokumbana nayo.
Kwa kifupi baadhi ya walio kwenye ndoa wanalia, unaweza kuwaona wakipita
mbele za watu wanachekacheka na kuonesha kuwa wanapendana lakini kumbe
katika uhalisia, wamechokana na ndoa zao zimeshikiliwa na nyuzi.
Unaweza kujiuliza ni kwa sababu gani? Inakuwaje watu waliotokea
kupendana sana wanaishi kwa muda mfupi tu kisha wanaanza kujutia maamuzi
yao ya kuingia kwenye ndoa?
Hakuna sababu nyingine zaidi ya kwamba aidha walikurupuka kufanya
maamuzi hayo au kulikuwa na mazingira ya mmoja kujifanyisha na kumfanya
mwenzake aone amempata mtu sahihi kumbe hamna kitu.
Ukijaribu kuchunguza sana, utabaini kuwa wengi wako kwenye ndoa za
Kichina. Ndoa ambazo hakuna mapenzi ya dhati baina yao na kusalitiana
imekuwa ndiyo mtindo wa kisasa. Katika mazingira haya furaha haiwezi
kupatikana na ni lazima majuto yatokee.
Nini ninachotaka kuzungumzia leo? Ni kwamba, ndoa kweli ni heshima na
kama umetokea kuwa kwenye uhusiano na mtu ambaye unaona ana kila kigezo
cha kuwa mwenza wako, una kila sababu ya kufanya kila uwezalo
kukaribisha ndoa. Oa au olewa ili furaha yako iweze kukamilika.
Lakini sasa angalizo ni kwamba, si kila anayeonesha kukupenda sasa
anafaa kuwa mumeo au mkeo. Elewa kwamba kuna wanawake wengine ambao wao
kupenda kwao hawamaanishi ni ili waolewe, wanapenda tu na kufurahia
kampani lakini ukiwatajia ndoa, usije ukashangaa wakakataa kuolewa. Hawa
wa sampuli hii ukiwalizimisha utakiona cha mtemakuni.
Namaanisha kwamba, wapo wanawake ambao lile neno ndoa tu kwao
limewakalia kushoto lakini wanajua kupenda na kuwaridhisha wanaume. Ni
sawa na kulazimisha kumuoa changudoa ambaye ni mtaalamu wa kudatisha,
mtaalamu wa kubembeleza na mtaalamu wa kumpa furaha mwanaume yeyote kwa
kuwa ameona pesa.
Ukimuoa mwanamke wa aina hiyo ukidhani utapata mambo kama
hayohayo,umeumia. Hilo lipo pia kwa wanaume, kuna wale ambao wanaweza
kuonesha upendo wa hali ya juu lakini hawako tayari kuingia kwenye ndoa.
Ukilazimisha kuolewa na mwanaume huyo, umeula wa chuya kwani huwezi
kuyapa mapenzi aliyokuwa akikupa kabla ya ndoa.
Kwa maana hiyo nihitimishe kwa kusema kuwa, lazimisha ndoa lakini kwa
mtu ambaye una uhakika anahitaji kuingia kwenye ndoa na umemsoma vizuri
na kubaini hawezi kuja kukuletea maumivu siku za baadae.
No comments:
Post a Comment