MSISIMKO ni jambo la msingi kwa walio kwenye uhusiano wa mapenzi. Ndiyo muongozo wa kihisia kwa wapenzi. Kwa maneno mengine kama mmoja akipoteza msisimko kwa mwenzake ni hatari kubwa sana inayoweza kugharimu uhusiano.
Ndiyo somo tunalojadili hapa katika Let’s Talk About Love ambapo leo ndiyo ninahitimisha. Kama kawaida ya kona hii nina imani kuna jambo kubwa utakaloondoka nalo. Hutakuwa kama ulivyoanza kusoma. Lazima kuna kitu utajifunza kichwani mwako.
Kama mtakumbuka, wiki iliyopita nilieleza kwamba, lazima uchunguze ujue kama ni kweli mwenzi wako amepoteza msisimko, lakini jambo kubwa zaidi ambalo nilisisitiza ni kwamba, mwenzi anapoteza msisimko kutokana na sababu nyingi, ikiwemo makosa/maudhi madogo au makubwa uliyoyafanya kwake.
UFAFANUZI
Yapo maudhi madogo madogo ambayo mtu anaweza kuwa hayapendi, lakini kwa sababu yanajirudia mara kwa mara yanazidisha chuki na hatimaye kupoteza msisiko kabisa.
Kuna maudhi/makosa makubwa ambayo mwenzi anaweza kuoenekana amesamehe lakini kumbe bado yanafukuta kwenye moyo wake. Haya mambo yapo marafiki zangu. Ni vyema kufuatilia ili kufahamu tatizo lilipo.
Yote kwa yote, hapa tunadili zaidi na suala la kupoteza msisimko ambalo sasa, kwa kuwa unaupenda uhusiano wako ni kazi yako kuhakikisha unamrudisha mwenzi wako katika hali yake ya kawaida. Wiki iliyopita nilishauri kuacha kabisa kulaumu badala yake kushughulikia tatizo husika.
Sasa twende tukaone zaidi juu ya mada hii ambayo naamini itawatoa wengi gizani.
ULIMI WAKO VIPI?
Kuna watu wengine wanashindwa kuelewa kwamba kauli chafu pekee inatosha kabisa kumuudhi mpenzi na akapoteza hisia za mapenzi kwa mwenzake. Majibu ya hovyo, kauli nyepesi ambazo hazina uungwana na heshima zinatosha kabisa kumkimbiza mpenzi wako.
Ufanye ulimi wako uwe mtamu, zungumza na mwenzako kwa mapenzi motomoto. Achana na kauli moto au zile zilizokosa mahaba. Jenga mapenzi kwa mwenzako, achana na mazoea.
Maana kuna wengine, kwa sababu ameshazaa, basi utasikia mama naniii, baba Joseph n.k. Achana na majina hayo, mwite kwa majina ya kimapenzi au jina lake halisi, utafaulu kudumisha hisia za mpenzi wako.
DHARAU NI MBAYA!!!
Hata kama mpenzi wako si mwerevu katika maeneo fulani, usimwoneshe dharau. Inawezekana ana udhaifu fulani katika mambo yake, hupaswi kumuonesha kwamba yeye si lolote. Jambo kubwa kwa mwenzi wa aina hiyo ni kumfundisha.
Yes! Kumpa ujuzi, maana umeshagundua kwamba ana udhaifu katika eneo fulani, mwoneshe njia. Mtu yeyote akigundua kwamba anadharauliwa, haonekani kama ana mchango katika jambo fulani, huchukia.
Ataanza kwanza kujichukia mwenyewe, halafu mwisho wake atamchukia mtu ambaye anamshusha thamani kwa kumdharau halafu hatma yake, atapoteza msisimko kwa mtu huyo. Akimuona tu, moyoni anajisikia huzuni. Hawezi kuwa na furaha kwa mtu ambaye anamdharau.
JENGA TABIA YA KUMSIFIA
Hakuna mtu ambaye hapendi kuonekana anaweza. Akijua anaonekana anaweza, hujiamini sana. Huu ndiyo ukweli ambao hakuna anayeweza kuukimbia. Hata wewe bila shaka unapenda kusifiwa kwamba unaweza kitu fulani.
Mmwagie sifa mpenzi wako, akivaa vizuri mwambie, akitengeneza nywele vizuri msifie...kifupi mfanye ajione kwamba yeye ni muhimu kwako. Atakapogundua kwamba yeye ni muhimu kwako, utakuwa umefanikiwa kwa kiasi kikubwa sana kuteka hisia zake.
FARAGHA SASA...
Namna ya kuwasiliana faragha pia husababisha kupoteza au kuamsha hisia za mpenzi wako. Utakuta mwingine anamwambia mpenzi wake bila woga, kwamba hawezi mapenzi, hilo ni kosa kubwa sana kwa wapenzi.
Ni sawa na kumtukana. Katika hali ya kawaida, ukimwambia mpenzi wako hawezi mapenzi, ni dhahiri utakuwa umekata moja kwa moja hisia zake. Hata mkikutana siku nyingine atakuwa hajiamini, atajiona anakwenda kukutana na mtu ambaye hawezi kumridhisha.
Kuliko kumsema, ni bora kumfundisha.
OMBA MSAMAHA
Kuomba msamaha ni kiunganishi kikubwa cha mapenzi. Hapa sitazungumza sana, maana naamini kila mmoja anafahamu maana ya msamaha na wakati muafaka wa kuutumia. Usibaki na vitu moyoni, kama unajua kweli umemkosea mwenzako, haraka sana mwombe msamaha na muendelee na mambo mengine.
Kubaki na vinyongo husababisha hasira ya kudumu, ambayo mwisho wake hutafuna msisiko na hivyo kukosa furaha katika uhusiano wenu.
Haya ni mambo ya msingi kabisa kwako kuyazingatia ili uweze kuwa bora na kuhakikisha msisimko kwa mwenzi wako unakuwa wa kudumu. Ndiyo nguzo ya penzi. Ahsanteni sana kwa kunisoma. Kwa hapa naweka kituo kikubwa.
No comments:
Post a Comment