WAKATI akili yangu ikianza kupata ufahamu, nilikuwa natatizika na kuwaza kitu gani hasa katika mapenzi kinaweza kumfanya mtu atulie ndani ya penzi lake.
Niliamini kuwa na fedha ndiyo dawa ya mtu kumtuliza mpenzi wake au kwa mwanamke kuwa mzuri na mwenye sifa zote, ndiyo dawa ya kumfanya mpenzi wako atulie.
Baada ya kukua na kuingia katika dunia ya ufahamu wenye mitihani mingi ya mapenzi, nimegundua kuna utofauti mkubwa katika vitu nilivyoviwaza.
Wakati nakua, nilikutana na matukio ambayo niliona kama ngamia kupita kwenye tundu la sindano, lakini baada ya kupevuka, nilipata majibu ya maswali yaliyonisumbua kipindi kile cha utoto.
Sikuamini mke wa tajiri kufanya mapenzi na muuza mchicha, mwanaume mwenye mke mzuri kutembea na changudoa au msichana wa kazi asiyejua kuvaa wala kuoga.
Baada ya kuingia katika kazi hii ya kukumbushana mambo ya mapenzi, nilipata maswali mawili ya watu wawili tofauti lakini yalikuwa na jibu moja.
Mmoja alilalamika ana mke, anamhudumia kila kitu ikiwemo familia yake lakini alichomlipa ni kutembea na mtu asiye na mbele wala nyuma. Mwingine alilalamika kuhusu mpenzi wake kutembea na mwanamke wa nyumba ya pili ambaye haufikii hata mguu wake kwa uzuri.
Kabla ya kulizungumzia hilo, nirudi kwao kuwaeleza kukosa uamini hakuangalii katembea na tajiri au mwanamke anayekushinda uzuri, kutoka nje ya uhusiano au ndoa ni kosa kwa vile penzi ni la watu walioridhiana au kuoana wakiwemo waliooa wake zaidi ya mmoja.
Leo nawajibu wote kuwa fedha au uzuri wa mtu havibebi ndoa au uhusiano. Nimekuwa muumini mzuri wa kuwaeleza penzi la kweli lipo vipi, mapenzi ni upendo wa dhati kutoka moyoni, kuwa tayari kujilinda na kujiheshimu bila kujali una fedha au ni mwanamke mzuri.
Mapenzi ni mbegu inayohitaji udongo wenye rutuba ya upendo ili mbegu hiyo imee. Siku zote mwenye mapenzi ya kweli humuangalia mtu, si kitu.
Tajiri na fedha zake asipopendwa huwa katika mateso na kukonda wakati ana kila kitu. Penzi la kweli halinunuliwi kwa gharama yoyote.
Tabia ya asili huwa sawa na moto unaowaka kwenye pamba, ukitoa moshi ujue hakuna kilicho salama. Wapo watu wasiokuwa na mapenzi ya dhati, utakuta mtu anajifanya anakupenda ukiwa naye lakini mkiachana hana habari na wewe, hata kama mnakaa nyumba moja na kulala kitanda kimoja.
Mtu anapoamua kutoka nje ya ndoa wakati ndani ana mke mzuri au mume wa ukweli anayempa kila kitu, kuna mawili:
Mosi:
Huenda mwanamke aliyenaye alimtamani kutokana na sura na umbile lake na hakumpenda kwa dhati. Matokeo yake baada ya kumchoka, mwanamke huonekana hafai na hukaa naye kimazoea.
Upande wa mwanamke, naye huenda amekwenda kwa mwanaume kutokana na kujua ana fedha lakini anakuwa hana mapenzi naye. Hapo lazima atatafuta penzi la nje ili afurahishe nafsi yake, kwa hiyo watu hawa kutoka nje sishangai.
Pili:
Tabia ya kutoridhika na mpenzi mmoja, watu wa aina hii huwa hawajisikii kula kitu cha aina moja kwa muda mrefu, lazima atatafuta mtu wa kumfanya abadili mboga.
Vitu hivi vyote huwa vinawachanganya watu, hasa wale wanaoamini kuwa mwanaume anapokuwa na fedha au mwanamke anapokuwa mzuri, ni kila kitu katika mapenzi.
Mapenzi ni bahati, hasa kumpata uliyemkusudia, basi muombe Mungu utakayemchagua naye awe kweli
amekukubali, hata ukiwa mbali kila mmoja amlindie mwenzake heshima, kwa kutanguliza uaminifu mbele.
No comments:
Post a Comment