Saturday, 14 September 2013

LEO KATIKA MAHUSIANO:Unataka kuingia kwenye mapenzi sawa, upo tayari?



UAMUZI wa kuingia kwenye uhusiano wa kimapenzi si sawa na kufanya uchaguzi wa aina ya chakula unachopenda kula. Haufanani na uamuzi wa kuchagua muda wa kulala. Haufanani na kitu chochote kile.
Ni uamuzi makini, ambao unahitaji utulivu na uamuzi wa ndani. Si kukurupuka, maana mwisho wake unaweza kuwa machozi. Hebu jiulize, wewe ambaye unataka kuanzisha uhusiano wa kimapenzi upo tayari?

Suala la utayari halikuhusu wewe kama wewe kwa uamuzi binafsi na hisia zako za ndani pekee, lazima uwe na sifa muhimu ambazo zinakidhi wewe kuwa na mwenzi. Tupo pamoja marafiki?
Yapo mambo ya msingi ambayo lazima yawe yametimia kwako, ndipo uwe na hadhi ya kuwa mpenzi wa mtu. Wanasaikolojia ya Uhusiano, wameelekeza wazi vipengele muhimu ambavyo kijana anapaswa kuvizingatia kabla hajaamua kuingia katika uhusiano wa kimapenzi.
Hata hivyo, tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa vijana wengi wanaobalehe au kuelekea kubalehe huwa hawafahamu vipengele hivyo muhimu na hata hao wachache waliopata elimu hiyo elekezi bado hujikuta wakishindwa kufuata taratibu hizo kulingana na mazingira.
Vipo vitu vingi vya kuzingatia, lakini nitafafanua vile vya msingi zaidi, ambavyo vitakuongoza wewe kijana kabla ya kuamua kuingia kwenye uhusiano.
Ni mada nzuri zaidi kwa vijana ambao bado hawajaanza uhusiano, lakini hata kwa aliyeanza, itamsaidia kujua yupo katika kundi gani na nini cha kufanya. Lazima kuna kitu cha kujifunza katika mada hii. Twende darasani.
SUALA LA UMRI
Hili ni la kwanza kati ya yale muhimu zaidi ya kuzingatiwa, lazima uangalie una umri gani? Inawezekana ukawa na umri ambao unadhani una uwezo mkubwa wa kupanga na kuamua mambo yako lakini kumbe siyo!
Unaweza ukaingia katika uhusiano, ukadumu humo kwa muda mrefu sana, lakini wakati huo ukiendelea kukua kiakili, hapo sasa ndipo utakapogundua kuwa kuna makosa uliyofanya awali.
Inashauriwa kwamba vijana ambao wana umri chini ya miaka 18, wasijiingize kabisa katika uhusiano. Huu ni ushauri na mahali pengine siyo ushauri ni lazima! Kama unajijua upo chini ya umri huu, achana kabisa na mapenzi, huu ni muda wako wa kupanga maisha yako ya baadaye.
KWA WANAFUNZI...
Inawezekana ukawa na umri zaidi ya miaka 18, lakini ukawa masomoni, je unaruhusiwa kuwa na mpenzi? Jibu ni hapana...wewe uliye masomoni hususan Elimu ya Msingi na Sekondari hushauriwi kuwa katika uhusiano kwa kipindi hiki. Masomo ni magumu sana kwa ‘levo’ hii na inawezekana ukashindwa kufanya mitihani yako vizuri kutokana na kuwaza mambo mawili kwa wakati mmoja.
Kimsingi ni vitu viwili tofauti ambavyo havichanganyiki. Hii siyo amri, ni ushauri tu! Kama kweli unataka kufanikiwa katika maisha yako ya baadaye, soma kwanza achana na mambo ya mapenzi katika kipindi hiki.
Andaa maisha yako kwanza. Siku moja ukiwa mitaani baada ya kumaliza masomo, ikiwa utabahatika kusoma makala haya kwa mara nyingine gazetini, mtandaoni au hata kwenye kitabu, utajuta na inawezekana ukalia, wakati huo muda utakuwa umeshapita!
FEDHA INAHUSIKA?
Mapenzi na fedha ni vitu viwili tofauti rafiki zangu, lakini kuna wakati fedha inakuwa na nafasi yake katika mapenzi. Siyo kwa maana ya kuhonga au kununua penzi, lakini kwa ajili ya mahitaji ya hapa na pale.
Sasa jiulize, ikiwa wewe ni mwanafunzi, unayetegemea kupewa fedha za matumizi na wazazi wako, utawezaje kugharamia penzi lako?
Ikiwa umekwishamaliza masomo yako, na umri wako unaruhusu (zaidi ya 18), kipengele hiki hakikuhusu, maana penzi la dhati halizingatii fedha. Kama upo masomoni, basi yakupasa usome kwa bidii hadi utakapomaliza masomo yako, mapenzi yapo, utayakuta!
IPO DAWA!
Najua wengi watakuwa na maswali mengi, kwamba kwa sababu tu, mtu anasoma ndiyo asiwe na mpenzi? Au mwingine anawaza atawezeje kuishi bila kuwa na kampani ya jinsia tofauti? Hayo yote ni mawazo yenye maana kubwa katika mada hii. Wataalam wanawashauri wanafunzi kuwa mbali na mapenzi, kwa sababu mapenzi huteka hisia, muda mwingi huweza kuutumia kumuwaza mpenzi zaidi kuliko masomo, sasa kuna haja gani ya kuchanganya mambo wakati inawezekana kuacha?
Haikatazwi kuwa na rafiki wa jinsi tofauti na yako, lakini iwe kwa wema. Kuna mambo mengi unaweza kufanya na rafiki yako kuliko kuwa katika uhusiano wa kingono. Itapendeza kama mtasaidiana kimasomo au kuanzisha mijadala itakayowapa mwanga wa maisha yenu yajayo.
Pamoja na hayo, najua ni vigumu sana kuweza kudhibiti hisia, lakini hilo linawezekana kama utakuwa mtu wa mazoezi, msomaji wa vitabu mbalimbali vitakavyokujenga na mengineyo.
Mchukie kama rafiki yako wa kawaida, weka hisia za mapenzi pembeni, endelea na maisha yako na siku moja muda ukifika na ukiwa tayari utaingia katika uhusiano makini utakaokufurahisha siku zote za maisha yako.
MUHIMU
Katika vipengele vyote nilivyoanisha hapo juu, hasa katika kijisehemu cha kipato na masomo, haviwahusu wanafunzi wa vyuo! Hii inakuwaje? Kwa sababu wengi wao huwa ni watu wazima tayari, wenye ufahamu juu ya mambo mbalimbali ya maisha yao. Wanajua kupambanua mambo na wanajua wanachokifanya.
Wengine huwa tayari wapo katika ndoa au kuingia katika ndoa wakiwa vyuoni, hawa vipengele hivyo haviwahusu. Pamoja na hayo, angalia moyo wako unazungumza nini kabla ya kuingia katika uhusiano. Naamini nimeeleweka.
Tukutane hapa wiki ijayo kwa mada nyingine kali.

No comments:

Post a Comment