Katibu wa Itikadi na Uenezi waCchama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye
Katika mabadiliko hayo, Rais aliwateua mawaziri wapya 10 na kuwapandisha manaibu wanne kuwa mawaziri kamili.
Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimesema leo kitatoa ufafanuzi kuhusu mawaziri walioshindwa kutekeleza majukumu yao lakini hawajaguswa, licha ya Rais Jakaya Kikwete kufanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri na kuwatosa mawaziri watano.
Katika mabadiliko hayo, Rais aliwateua mawaziri wapya 10 na kuwapandisha manaibu wanne kuwa mawaziri kamili.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape
Nnauye, aliliambia gazeti hili jana kuwa kumekuwa na kauli tata
zinazotolewa na watu wa kada mbalimbali kuhusu kubaki kwa mawaziri hao.
“Kesho (leo) nitatoa ufafanuzi kuhusu mawaziri hao
maana kumekuwa na kauli tata na nyingine za ajabu kabisa kuhusu
mawaziri hao,” alisema Nape.
Desemba 14 mwaka jana, CCM kupitia kikao chake cha
Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa, ilimtupia mpira Rais Kikwete
kuamua hatma ya mawaziri hao, huku kikifafanua kuwa ilimshauri ama
kuwafukuza, kuwahamisha wizara au kuwahimiza wafanye kazi.
Mawaziri hao ni, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya
Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika,
Christopher Chiza, Naibu Waziri wa Fedha Saada Mkuya (alihojiwa kwa
niaba ya aliyekuwa Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa ambaye kwa sasa ni
marehemu).
Wengine ni, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk
Abdallah Kigoda, Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo
David, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma, Celina Kombani na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu,
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia.
Katika ufafanuzi wake wa jana, Nape alisema CCM
ilivyowataja mawaziri hao ilitoa mapendekezo mengi na kwamba vyombo vya
habari vimekuwa vikiripoti habari tofauti na kilichozungumzwa na chama
hicho.
Mawaziri hao waliotajwa kuwa ‘mzigo’ waliitwa na
kuhojiwa katika kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho na kutakiwa kutoa
maelezo ya masuala yaliyoibuliwa na wananchi wakati wa ziara ya viongozi
wa CCM wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma.
Tofauti na ilivyotarajiwa na wengi, kati ya mawaziri hao wanaotajwa kuwa ni ‘mzigo’ hakuna hata mmoja aliyeguswa.
Badala yake walioondolewa katika mabadiliko hayo ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk Terezya Huvisa.
Wengine ni Goodlucky Ole Medeye (Ardhi), Gregory
Teu (Viwanda na Biashara), Benedict Ole Nangoro (Maendeleo ya Mifugo na
Uvuvi) na Philipo Mulugo (Elimu na Mafunzo ya Ufundi).
No comments:
Post a Comment