Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa akihutubia mkutano wa Operesheni Pamoja Daima katika mji wa Namtumbo mkoani Ruvuma juzi.
Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu amevishukia vyombo vya dola kwa kuvitaka kufanya kazi kwa weledi.
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeendelea na Operesheni Pamoja Daima katika mikoa mbalimbali nchini.
Kyela. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)
kimewataka madereva wa pikipiki zinazobeba abiria maarufu kama
`Bodaboda’ kuacha kumuunga mkono Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa.
Akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika jana
kwenye Uwanja wa Siasa ulioko mjini Kyela, Mbunge wa Mbeya Mjini kupitia
chama hicho, Joseph Mbilinyi aliwashauri watu wa bodaboda kupokea
misaada ya kiongozi lakini ikifika uchaguzi waichague Chadema.
Sugu, ambaye alikuwa amefuatana na Katibu Mkuu wa
Chadema, Dk Willibrod Slaa na Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter
Msigwa ikiwa sehemu ya Operesheni Pamoja Daima ya chama hicho, alisema
kuwa Lowassa anatafuta kuungwa mkono na makundi mbalimbali ili
kufanikisha malengo yake ya urais.
“Lowassa katika siku za karibuni amekuwa akitoa
misaada mingi kanisani sasa amehamia kwenye bodaboda,” alisema Sugu huku
akishangiliwa na umati mkubwa wa watu uliofurika kwenye mkutano huo.
Sugu alisema kuwa bodaboda wanapaswa kuachana na
Lowassa kwani ni mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho hakina
msaada kwao.
“Akiachana na CCM, akaamua kwenda chama kingine
basi mnaweza kumuunga mkono ila akibaki CCM achaneni naye,” alisema Sugu
wakati akimzungumzia Lowassa, ambaye hivi karibuni alishiriki katika
bonanza lililoandaliwa na Bodaboda jijini Dar es Salaam.
Mapema Dk Slaa na Mchungaji Msigwa waliendesha
operesheni hiyo kwa kupaa kwa helikopta jana asubuhi hadi wilaya za
Ludewa, Makete, Rungwe na Kyela huku wakiwekea mkazo masuala ya matatizo
ya ufisadi, matumizi mabaya ya rasilimali na vita dhidi ya ujangili.
Lissu avishukia vyombo vya dola
Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu amevishukia vyombo vya dola kwa kuvitaka kufanya kazi kwa weledi.
Akihutubia kwenye Uwanja wa Kiboroloni mjini
Moshi, Lissu alisema kuwa matukio ya polisi kuua raia na hata madhara
yaliyotokea kwenye Operesheni Tokomeza Ujangili yanatokana na matatizo
yanayokabili vyombo vya dola.
“Angalia matatizo yanayokabili Jeshi la Polisi kama makazi na masilahi duni ndiyo yanachangia wao kuua raia,” aliongeza Lissu.
Mnyika, Lema waunguruma
Pia viongozi wa Chadema waliendesha kampeni yao
katika mikoa ya Tabora na Katavi kwa kuhutubia Sikongwe, Mpanda
Mashariki, Mpanda Magharibi na Mpanda mjini.
Viongozi walioshambulia jukwaa ni pamoja na Makamu
Mwenyekiti wa Chadema kwa upande wa Zanzibar, Said Issa Mohamed,
Mkurugenzi wa Uenezi wa chama hicho, John Mnyika, Mbunge wa Arusha
Mjini, Godbless Lema.
Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo,
aliwashutumu viongozi wa Serikali kuwa wamekuwa wakitumia vibaya
rasilimali za nchi na kusababisha Watanzania kuendelea kuwa masikini,
huku wachache wakinufaika.
Naye Lema alizungumzia juu ya timuatimua
iliyowakumba viongozi kadhaa wa chama hicho akiwataka wananchi waamini
kuwa Chadema ni makini na kamwe hakitawavumilia wasaliti.
No comments:
Post a Comment