Karibu ndugu yangu katika safu hii ambayo imekuwa ni msaada hasa kwa watu wenye ndoto za kubadilika katika maisha.
Ambacho nataka kusisitiza ni kwamba haijalishi uko
katika hali gani ya maisha, unaweza kuondoka katika hali hiyo ngumu na
kuwa na maisha bora. Hata kama uko mdogo kimafanikio kiasi gani, fahamu
kuwa hata mbuyu ulianza kama mchicha. Ni kawaida yetu wanadamu kuanza
wadogo kisha kuwa wakubwa, kwa maana hata kuzaliwa tunazaliwa tukiwa
wadogo, polepole tunakua hatimaye tunakuwa watu wazima.
Lakini hata unapokuwa mkubwa kwa maana ya
mafanikio kuna wakati unaweza kupigwa...yawezekana ni madeni, yawezekana
ni fitina umefanyiwa, ukafukuzwa kazi na kadhalika, lakini ni makosa
kukata tamaa. Unapaswa kuangalia wapi ulipojikwaa, ili uweze kwenda
mbele bila kujikwaa tena.
Haijalishi wewe hapo ulipo una cheo gani, ni suala la msingi sana kuyatengeneza maisha yako kuwa katika hali ya kujitegemea.
Wachumi maarufu Duniani wanabainisha kuwa
ulimwengu unaendeshwa na watu wasiozidi asilimia 10, hao ndio waliobuni
gazeti unalolisoma, waliobuni karatasi, magari tunayopanda, pikipiki,
taa na kadhalika, huku wengine tukiwa ni wanunuzi wa huduma au ugunduzi
wao.
Wanasema kwamba wengi wa watu ni waoga wa
kujaribu, huku wengi wao wanachokifahamu ni kula starehe kuliko
kuangalia namna ya kujiimarisha kiuchumi.
Katika kitabu the Law of Success (Sheria za
kufanikiwa) cha mwandishi nguri Duniani, Napoleon Hill, ni kwamba msingi
mkubwa wa kufanikiwa kwa mtu kwanza kabisa ni kuwa na nafsi ya
kuthubutu kufanya jambo.
Anasema kwamba mtu akiwa na fikra hizo na akazifanyia kazi, kwa vitendo, kufanikiwa si jambo gumu kwake.
Katika kitabu cha Mwongozo wa Kutengeneza bidhaa
mbalimbali zikiwemo keki, vyakula vya kuku, sabuni na bidhaa zingine
zinazoweza kumsaidia mtu kuanzisha biashara yake, nilieleza pia jambo
kama hili, kwamba mtu yeyote anaweza kuwa na maisha yenye mafanikio kama
pia atakuwa anafanya kazi nyingi.
Ni sawa umeajiriwa lakini wangapi walikuwa na
ajira leo wanalia, wengine walikuwa mawaziri, leo wamepunguzwa, wako
nyumbani wanalia, wengine walikuwa wakuu wa mikoa, wakuu wa polisi na
kadhalika. Lakini ukiwa na mradi wako imara, hata kama utafukuzwa kazi,
huwezi kulia sana. Hata kama utaumwa unaweza kuajiri watu kuendesha
mradi wako, lakini kwenye ajira, ukiumwa sana, mwajiri anayo haki ya
kukuondoa kazini.
Tatizo kubwa la wengi ni kwamba hawafanya yale
yaliyo ya maana, unakuta mtu anatoka kazini anaingia kwenye ulevi,
anahonga au matumizi mengine yasiyo ya maana; si wengi wanaowaza namna
ya kufanya ili wawe na miradi yao imara.Ni sawa unaweza kuringia ajira,
unaweza kuringia ubosi, kumbuka kiti unachokalia, kuna watu walikikalia,
iko siku na wewe utatoka, je, umejiandaaje kama ikitokea unafukuzwa
kazi? Tafakari, chukua hatua.
Ni suala la msingi sana familia kuwa na mradi wao,
ni ujinga kwa mfano watu wameoana halafu kila mtu anawaza namna ya
kujenga kwao au kujenga kwa siri; hekima ni kwa watu wa familia
kujadiliana namna ya wao wenyewe kuwa na mradi fulani wa maendeleo kwa
pamoja, ili hatima ya uzee wao iwe nzuri.
Watu wengi wanakufa haraka baada ya kustaafu kwa sababu wanakuwa hawana fedha za kuendesha gharama mbalimbali za maisha; je, kama unafukuzwa leo hapo kazini unaweza kuishi miezi mitatu bila kuteteleka? Kama unaweza wewe ni mtu imara unayefaa, kama huwezi hilo ni kosa kubwa, jipanga haraka kuimarisha uchumi wako.
Watu wengi wanakufa haraka baada ya kustaafu kwa sababu wanakuwa hawana fedha za kuendesha gharama mbalimbali za maisha; je, kama unafukuzwa leo hapo kazini unaweza kuishi miezi mitatu bila kuteteleka? Kama unaweza wewe ni mtu imara unayefaa, kama huwezi hilo ni kosa kubwa, jipanga haraka kuimarisha uchumi wako.
No comments:
Post a Comment