Polisi nchini India wamewakamata wanaume 13 waliohusishwa na genge la
wanaume waliombaka msichana mwenye umri wa miaka 20 katika jimbo la
Benghal Magharibi.
Inadaiwa wanaume hao walimbaka mwanamke huyo kufuatia amri ya wazee
wa kijiji ambao wamejipa wenyewe mamlaka ya mahakama ya kitamaduni.
Msichana huyo amelazwa hospitalini kwa matibabu akiwa katika hali
mahututi.
Inaarifiwa kuwa amri ya kumbaka mwanamke huyo ilitolewa na wazee wa
kijiji ambao walipinga uhusiano wake na mwanamume kutoka katika jamii
tofauti.
Hiki ndicho kisa cha hivi karibuni cha genge la wanaume kumbaka
mwanamke nchini India. Tangu kisa cha ubakaji wa mwanafunzi mwenye umri
wa miaka 23 uliofanywa na genge la wanaume mjini Delhi mwaka 2012 ,
swala la ubakaji limekuwa likiangaziwa sana nchini India.
Hasira ya mamilioni ya watu iliyotokana na kisa hicho ilipelekea
vyombo vya habari nchini India kuanza kuangazia tatizo hilo , swala
ambalo wengi walihisi lilikuwa limepuuzwa kwa muda mrefu.
Serikali nayo ilianza kuweka sheria kali kuhusu dhuluma za kingono
dhidi ya wanawake. Lakini utekelezwaji wa sheria hizo bado ni changamoto
katika nchi ambayo ustawi wa kijamii unakuwa kwa kujikokota na ukosefu
wa usawa likisalia kuwa tatizo jengine kubwa.
Wengi wameshangazwa kuwa katika kisa hiki, ubakaji umeamrishwa na
kikundi cha wazee wa kijiji ambao wamejipa mamlaka kama viongozi wa
kijamii.
No comments:
Post a Comment