Wednesday, 22 January 2014

Wachovu Manchester United kujiuliza kwa Sunderland leo

Man United ambayo kwa sasa ipo nafasi ya saba katika ligi wakiwa nyuma kwa pointi 14, pia wameachwa kwa pointi sita katika kuifikia nafasi ya nne


London, England.

Manchester United wanatakiwa kusahau mwendo wao mbovu katika mbio za ubingwa wa ligi, lakini kocha David Moyes anatakiwa kuhakikisha wanamaliza msimu wakiwa hata na kombe moja la ndani.

Jumapili United walipokea kipigo cha mabao 3-1 kutoka kwa Chelsea na kuifanya nafasi yao kuwa finyu kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu na kufungwa na Swansea City katika Kombe la FA ni wazi taji pekee lililobaki kwa United msimu huu England ni Kombe la Ligi.
Leo watacheza na Sunderland katika mchezo wa marudiano baada ya mchezo wa kwanza kufungwa 2-1 kwenye Uwanja wa Light, na mshindi wa mechi hiyo atafuzu kwa fainali ambayo itakuwa dhidi ya Manchester City mwezi Machi.
Kipigo cha Chelsea ni mwendelezo wa matokeo mbaya wa Man United ambayo kwa sasa ipo nafasi ya saba katika ligi wakiwa nyuma kwa pointi 14, pia wameachwa kwa pointi sita katika kuifikia nafasi ya nne ambayo itawawezesha kucheza Ligi ya Mabingwa msimu ujao.
Japokuwa mashabiki wa United bado wanaendelea kuumunga mkono Moyes katika kila matokeo mabaya ya timu hiyo, Mscoti huyo aliyechukua mikoba ya Alex Ferguson msimu huu, alisema uchezaji wao mzuri nyumbani ni kutokana na kuhofia kuzomewa.
“Tutahakikisha tunafanya kila tuwezalo tunapata matokeo mazuri,” aliimbia (www.manutd.com) baada ya kufungwa na Chelsea ikiwa ni mechi ya saba kufungwa kati ya 22 za ligi walizocheza.
United imekuwa kwenye wakati mgumu tangu kuumia kwa washambuliaji wake Robin van Persie na Wayne Rooney, pamoja na chipukizi mwenye miaka 18, Adnan Januzaj wachezaji wengine wameshindwa kuziba pengo hilo.
Sunderland ilipata ushindi katika mchezo wa kwanza kwa bao la mkwaju wa penalti wa Fabio Borini  na kushinda 2-1, pia vijana hao wa Gus Poyet waliamka kutoka kufungwa mbili  na kusawazisha 2-2 dhidi Southampton Jumamosi iliyopita.
Kiungo Craig Gardner alisema sare hiyo imewasaidia katika kuhakikisha wanafanya vizuri katika mchezo wa leo.
“Kila mechi ni muhimu kwetu kwa sasa, tupo katika nusu fainali, lengo letu ni kusonga mbele, japokuwa tunategemea kupata upinzani mkubwa Old Trafford,” aliimbia tuvuti ya Sunderland (www.safc.com).
 

No comments:

Post a Comment