Wednesday 22 January 2014

Mchungaji jela miaka minne kwa kuuza watu nje

Wakili Semali alidai kuwa, Februari 18 na 20 mwaka jana Kijiji cha Mbweera Masama, wilayani Hai, mshtakiwa aliwatorosha watoto hao hadi Dar es Salaam.


Mchungaji raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Jean Bamana amehukumiwa kwenda jela miaka minne baada ya kushindwa kulipa faini ya Sh10 milioni kwa kosa la kujihusisha na biashara ya kusafirisha binadamu.

Akisoma hukumu hiyo mjini Moshi juzi, Hakimu Mkazi Mkoa Kilimanjaro, Sophia Masati alisema iwapo mchungaji huyo atashindwa kulipa faini hiyo atamlazimika kwenda jela miaka minne.
Mchungaji huyo alikuwa akikabiliwa na mashtaka ya kuwatorosha wanafunzi wawili wa familia moja hadi Dar es Salaam, ili baadaye awasafirishe hadi nchi za Zambia, DRC na Afrika Kusini.
Upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali Kanda ya Moshi, Jullius Semali ulidai mchungaji huyo wa kilokole aliwaahidi watoto kuwatafutia shule katika nchi hizo.
Wakati wa tukio hilo, watoto hao mmoja mwenye umri wa miaka 17 na mwingine miaka 19, ni wanafunzi wa shule maarufu ya St Merigoret iliyopo Barabara ya Uru ya mjini Moshi.
Wakili Semali alidai kuwa, Februari 18 na 20 mwaka jana Kijiji cha Mbweera Masama, wilayani Hai, mshtakiwa aliwatorosha watoto hao hadi Dar es Salaam.
Mshtakiwa anadaiwa alikuwa awasafirishe watoto hao hadi kwenye nchi hizo tatu, kosa linaloangukia chini ya sheria ya kusafirisha binadamu (Human Trafficking) namba 6 ya mwaka 2008. Akitoa hukumu hiyo,

Hakimu Masati alisema mahakama hiyo imeridhika pasipo shaka yoyote na ushahidi wa mashahidi wanane upande wa mashtaka na kumuona mshtakiwa ana hatia. Kabla mchungaji huyo aliomba kuonewa huruma. na kumpunguzia adhabu kwa kuwa yeye ni mlemavu, ni mgonjwa na ni mchungaji.

No comments:

Post a Comment