Monday, 10 February 2014

Inakuaje mwanaume anakuolea mwanamke mwingine?

ASALAM alaikum/Bwana Yesu asifiwe!

Ndugu zangu, mashosti zangu, leo niwaletee swali na jibu lake, naamini litawasaidia wengi.

Kwanza nianze kueleza kuwa kwa kawaida mwanaume huwa anaoa kutokana na mambo mawili, kuna baadhi sheria inawaruhusu lakini wapo ambao licha ya sheria kuto wabana hawatamani kuoa zaidi ya mke mmoja lakini wewe mwenyewe mwanamke unamruhusu mumeo akaoe.

Unamruhusu kufanya hivyo kwa sababu ya kero zako, kujiamini kwako, uchafu wako pengine hata ndugu wa mume huwapendi.

Kwa nini inafikia hatua hiyo wakati uliahidi utaishi na mumeo kwa shida na raha na kwa mahaba mazito mwenyewe ukitamka mbele ya halaiki?


Wapo wanawake wanajisahau wanapokuwa kwenye ndoa. Kujisahau kwao ndiyo kunawafanya waume zao kutamani vitu wanavyovikosa kwa wake zao na kuamua kuvitafuta  kwingine.

Aidha, wanasababisha waume zao wawe na nyumba ndogo au kuoa kabisa na wakiwa na wake hao wapya husahau kabisa nyumba ‘kubwa’.


Kumbuka mwanamke anayejua mapenzi ukimchunguza sana unaweza ukasema anatumia uchawi kumbe ni mahaba tu anayompatia mumeo.

Wewe mwenyewe utawatangazia watu; “Mume wangu karogwa na mke mwenzangu au hawara yake” kumbe ni wewe mapenzi umepoteza, nikuambie shosti, utapoteza fedha nyingi kwa waganga ukitaka kurudisha penzi la mumeo kwako wakati dawa ni kukoleza penzi tu.

Nikwambie, huko alikoenda mumeo ataogeshwa, atalishwa, atabadilishiwa muonekano wa chumba, atang’aa mwanaume kama nyota angani kwa kusuguliwa bafuni.

Hapo sasa ulimi utakutoka kama umekimbia mbio ndefu za marathoni, utahaha wakati yote umejitakia mwenyewe. Ukweli ni kwamba wanaume wengi huwa hawachepuki nje ya ndoa bila kuwa na sababu, kikubwa mashosti zangu tuwe makini kuanzia mdomoni, vitendo vyetu na kujituma tunapokuwa nao kwenye uwanja wa fundi seremala.

Hebu jichunguzeni, mkiona mumepunguza mashamshamu kwa wandani wenu jirekebisheni msije mkajikuta mnashea penzi na mashosti wenu ambao wanaweza kuingia ndani nanyi kuondolewa.
Kwa leo yanatosha.

No comments:

Post a Comment