Makala
hii ni tafakari huru kuhusu mambo ya msingi katika mahusiano. Hapa utapata tafakari ya maana ya maneno na
imani ambazo zinatutatiza wengi wetu.
1. Mchanganyiko mkubwa kuhusu maana ya
mahusiano, mapenzi na ndoa:
Labda
kipengele hiki tuanze kwa kueleza kuwa kunaweza kuwepo ndoa, lakini yasiwepo
mahusiano wala mapenzi. Inaweza kuonekana kama inachanganya kidogo, lakini ndio
ukweli wenyewe. Ndoa ni namna tuu ambayo
wawili walio kwenye mahusiano wanaamua kuwataarifu rasmi watu wengine kuwa wao
wapo rasmi katika mahusiano.
Ndoa ni kiapo mbele ya watu wengine , na ni namna
ya kutaka kumuhakikishia mwenza wako kuwa endapo kiapo hicho kitatokea
kuvunjika, basi unakubali rasmi kuwajibika kwa mujibu wa taratibu zilizopo za
ndoa husika, ikiwemo kukubali kuitwa kwenye mabaraza ya usuluhishi, kugawana
mali, n.k. Na kwa upande wa kiroho, inabeba maana zaidi kuwa unaweka kiapo kwa
Mungu wako kuwa utalinda mahusiano yako na huyo unayemchagua.
Hivyo
basi, ndoa haijengi mahusiano wala mapenzi. Kiuhalisi inabidi kwanza yawepo
mahusiano na mapenzi kisha ndio kiapo kifanyike, kwani kinyume cha hivyo ni
kuwa unakula kiapo ‘feki’.
Ndio
maana basi, ni muhimu kwa wapenzi kutambua kweli kama wanahitajiana, kuwa
kwenye mahusiano na kutafakari kwa uhuru kama kweli wanataka kuweka kiapo rasmi
cha kuwa pamoja.
Kutumia
ndoa kama kinga ya kuhakikisha mahusiano yako yanadumu ni maamuzi magumu ambayo
pengine yanaweza yasilete faida hapo baadae.
2.Mahusiano na ndoa nyingi huyumbishwa na
Matarajio yasiyo halisi
Kabla
hata ya kuingia katika mahusiano na hatimaye ndoa wengi wetu huwa na matarajio
binafsi ya kimaisha. Matarajio haya yanajumuisha vile tunavyotaka sie wenyewe
kuwa hapo baadae, pamoja na matarajio ya vile tunavyotaka wenza wetu wawe.
Hata
hivyo katika hali halisi tunajikuta sisi wenyewe hatuwezi kujibadilisha au
kujiweka kwa usahihi vile tunavyotamani kuwa (kwa sababu kwa kila tunachojaribu
kufanya kuwa bora, tunajikuta bado tuna madhaifu mawili matatu). Pamoja na
ukweli huu, tunajikuta tupo na matarajio ya kuwafanya wenza wetu wawe watu wa
aina fulani. Kwakuwa kiasili binadamu ni kiumbe huru, tunajikuta wenza wetu nao
wakiwa ‘busy’ kutimiza ndoto za vile wanavyotamani kuwa iwe kimavazi, aina ya
marafiki, utafutaji wa kazi , kujiendeleza kimasomo, aina ya mali za kununua,
hata kufikiria tofauti aina ya maisha wanayotaka muishi.
Matokeo
yake ukinzani huu wa matarajio ni mkanganyiko wa mgongano wa mawazo kati ya
wawili nyie, na mwanzo wa vita ya chini kwa chini ya nguvu ya maamuzi katika
mahusiano yenu.
3. Kuweza kumbadili tabia mwenza wako
Mojawapo
ya jambo ambalo hufanywa na wengi walio katika mahusiano ni kuwa na ‘tamaa’ ya
kutaka kumbadili tabia fulani mwenza wake. Hata hivyo ‘tamaa’ hii ni sehemu ya
yale tunayoyaita matarajio yasiyo halisi, kwani tabia ya mtu hujengwa na mambo
mengi sana, ikijumuisha aina ya makuzi, aina ya mfumo wa imani mtu anaouamini,
aina ya marafiki alio nao, uwezo wake wa kujiamini katika kubadili tabia kwani
wengine wameshakata tamaa kuwa hawawezi kukata tamaa, na zaidi sana, mabadiliko
ya tabia huhitaji mfumo endelevu na wenye kusoma vema asili ya tabia ili kuweza
kuirekebisha.
Hata
hivyo wengi wetu kwenye mahusiano, hutegemea ‘mapenzi’au vitisho tuu kama vile
‘nitakuacha mie ’, kama sababu ya
kumfanya mtu abadilike kitabia.Udhaifu wetu katika kutambua asili ya tabia ya
mtu husika na mbinu za kisayansi za kubadili tabia hufanya zoezi la
kubadilishana tabia kuwa gumu na pengine lisilowezakana.
4. Kuvumilia ndio kuonyesha upendo na ndio
kudumisha mahusiano
Hii
ni aina nyingine ya matarajio ambayo sio halisi kwani kiukweli kila mtu analo
jukumu la kufanya bidii kuwa mtu mwema, hivyo hauhitaji kubeba ‘uzembe’ wa
mwingine kwa kisingizio tuu cha kuwa unaonyesha upendo hususani pale ambapo ni
kwa uzembe tuu au kutokujali kwake mwenza husika amefanya jambo fulani
.
Kwa
jinsi kasumba hii ilivyo enea sio ajabu kukuta mtu akifanya mambo mabaya kwa
mwenza wake kwa makusudi ili tuu eti apime kama kweli mwenza wake ni mvumilivu.
Kumbuka
hapa hatumaanishi kuwa kusamehe ni kosa. Hapana, kusameheana ni muhimu, lakini
sio kwamba ni muhimu tuu katika mapenzi. Kusameheana ni jambo la asili, na
tunapaswa kusameheana kwa mambo mengi nje hata ya mahusiano.
Tunachosema
ni kuwa kuna kasumba ya baadhi yetu
kuona kuwa wanayo ‘haki’ ya msingi ya kukosea eti tuu kwakuwa tuu mwenza wake
analazimika kusamehe ili kuonyesha kweli anao upendo wa dhati.
Amini usiamini, kasumba hii ya kutarajia aina
ya pekee ya kusamehewa na kuvumiliwa kwa kisingizio tuu cha kuwa upo kwenye
mapenzi na mwenza wako, hurudisha nyuma maendeleo ya mahusiano yenu kwani
mwenzi wako nae ni binadamu na kumbuka anayo matarajio mengine ya maisha,
isitoshe na yeye anahitaji upendo na kujaliwa na wewe, hivyo kutarajia kwako
kusamehewa na kuvumiliwa kuna mnyima haki mwenza wako. Hatimaye kutegema kwako
kusamehewa kila wakati, kunamfanya mwenza wako atilie mashaka upendo wako
kwake.
5. Uaminifu = Upendo= Kudumu kwa mahusiano
Pamoja
na ukweli kuwa mwenza wako anatarajia utakuwa muanifu kwake, elewa kuwa kuwa
mwaminifu pekee katika mahusiano yako sio tiketi ya kudumu kwa mahusiano yenu
kwakuwa watu wanaingia kwenye mahusiano sio tuu kwa kuwa wanataka kuwa na mtu
mmoja muaminifu bali wana mahitaji mengine wanayohitaji.
Zungumza
na mwenza wako, fanya utafiti wako binafsi kuhusu mpenzi wako ujue mambo
mengine anayohitaji toka kwako.
Pia msikilize anapokutaka urekebishe mambo
kadhaa au ufanye mambo fulani. Inapendeza pale unapomfanyia mtu mambo
yanayompendezesha kwa kuwa hivyo ndivyo anavyotaka, sio kwakuwa tuu wewe
unadhani kufanya hivyo kutampendezesha mhusika.
No comments:
Post a Comment