Imezoeleka kusikia kwamba wanawake ndio wanaonyanyaswa; sasa
taarifa mpya ni kwamba idadi ya wanaume wanaonyanyaswa na wanawake
nchini inaongezeka.
Jambo la msingi ambalo ningependa lifahamike ni
kwamba kitendo cha unyanyasaji si kizuri iwe amefanyiwa mwanamke au
mwanamume. Ukweli ni kwamba kila mtu anapaswa kufikiria namna ya
kumfanyia jambo zuri mtu mwingine, kwani ubaya hauna maana.
Ni kama zamu ya wanaume kuteswa
Baada ya kelele za muda mrefu kwamba wanaume
wanawatesa wanawake kwa kuwapiga, kuwanyanyasa kwa kauli na matendo yao
mengine, taarifa za hivi karibuni zinaonyesha kuwa kasi ya wanaume
kunyanyaswa na wanawake na hata kuteswa inaongezeka.
Wanaume kwa sasa wanateswa kwa sababu nyingi, kwa
mfano wengine wako kwenye ndoa lakini hawana uhakika wa ‘ndoa’; hawana
sauti, wakiongea sana wanaambiwa aaah bwana eeeh usinisumbue...jana
nilikupa na leo unataka kwani mimi ni gogo au ng’ombe sichoki”.
Baadhi ya wanawake wamekuwa hawana kauli nzuri,
hawana ile hali ya kushuka ili kuruhusu mazungumzo thabiti kufanyika
kunapotokea jambo. Je, tunakwenda wapi katika hali kama hii?
Kijamii inafahamika kwamba kazi za aina fulani ni
za watu wa jinsi fulani na hizi za jinsi ya fulani, lakini kwa namna
tunavyoona mambo ni kwamba wapo wenye kulazimisha kazi ambazo ni maalumu
kwa wanawake zifanywe na wanaume.
Mishahara ya wanawake wengi haijulikani
inatumikaje, mwanaume akihoji huwa ni ugomvi. Ninachotaka kusema hapa ni
kwamba iko haja kwa Watanzania kila mtu kwa nafasi yake aangalie namna
anavyoishi na kurekebisha kasoro ili Taifa letu liweze kuendelea vema.
Kuwa na uhusiano mbaya ni hatari kwa ustawi wa
nchi kwa jumla, kila mtu awe chanzo cha mabadiliko ambayo anataka
kuyaona.Je, unayofanya kwa mwenzi wako au watu wengine ungependa
kufanyiwa? Hili ndilo la kujiuliza na kulifanyia kazi.
Matendo ya wanaume wengine ni kinyaa
Mwanaume ni kichwa, hii ni kwa mujibu wa vitabu
vyote vitakatifu, kwa maana hiyo wanapaswa kuwa kweli vichwa kwa kauli
na matendo yao.Kichwa kinapofanya mambo ya bangibangi, ni ngumu sana
ubavu (mke) kuwa na moyo thabiti wa kuendesha maisha au uhusiano wao.
Ingawa wapo wanawake wenye matendo ya kunuka, kwa
lolote ambalo linatokea ni vizuri kupata muda wa kuzungumza ili kuondoa
tofauti.
Kulalamika kwamba wanawake ndio watu wabaya siku hizi au wanaume
ni watu wabaya, haina maana, kilicho cha maana ni kuangalia namna gani
tunaweza kuondoa kasoro ili maisha yaweze kwenda.
Kwa hali ilivyo sasa kila kundi linamlalamikia
mwenzake, wanawake wengi wanawalaume kwamba wengi hawana utulivu, huku
wanaume nao wanasema kwamba wanawake wengi siku hizi ni ‘chenga’ yaani
hawaeleweki.
Hakuna sababu kwa wanawake kulipiza kisasi kwa
kuwatendea mabaya wanaume, labda kwa sababu wamewahi kuwatendea mabaya,
wala hakuna sababu kwa yeyote kufanya hivyo. Kilicho cha msingi ni kila
mmoja kujiona kwamba analo deni la kumtendea haki mwenzi wake au jamii
inayomzunguka.
Imani yangu ni kwamba kila mtu akiwa na moyo wa
kupendana kwa dhati na kuamini tunalo deni la kufanyiana mazuri,
Tanzania itakuwa na maendeleo kwa kasi. Vitendo vya kutendea mabaya,
huenda havitakuwepo tena, hivyo kufanya kila mtu, wakiwemo watoto wetu
watayafurahia maisha. Duniani tunapita, ya nini kutesana!
No comments:
Post a Comment