KADIRI siku zinavyokwenda kumekuwapo na ugunduzi wa vitu mbalimbali vinavyochangia kuleta mabadiliko katika jamii. Mabadiliko hayo yanaweza kuwa hasi au chanya kutegemea na aina ya bidhaa iliyogunduliwa na matumizi yake. Zipo bidhaa zinazoonekana kuwa na matokeo ya haraka na mazuri baada ya kutumika, lakini wakati huo huo kuwa na madhara kiafya kwa mtumiaji.
Nchi nyingi zinazoendelea hasa zilizopo barani Afrika ikiwamo
Tanzania zimekuwa ndizo waathirika wakubwa wa bidhaa zinaotajwa kuwa na
madhara huku vijana wakiwa ndiyo kundi kubwa linaloathirika. Sababu za
kundi hilo kuathirika zaidi ni kutaka kwenda na wakati kwa kujaribu
kutumia kila bidhaa zinazotoka nje ya nchi bila kujua madhara yake.
Miongoni mwa bidhaa hizo ni nguo za ndani zilizoundwa maalumu kwa
ajili ya kupunguza unene, pia kutengeneza umbile la mvaaji katika
mwonekano wenye mvuto aupendao. Nguo hizo zimetengenezwa kwa mtindo wa
mbano, (Skin tight)ambapo ikivaliwa hubana eneo la tumboni hadi kwenye
mapaja na hufanya kazi ya kupunguza unene, zikiufanya mwili kuwa
mwembamba kulingana na nguo husika ilivyo.
Licha ya kufanya kazi hiyo kwa ufanisi na kusaidia kwa kiasi kikubwa
watu wengi kupunguza miili yao, utafiti wa kisayansi unaonyesha kuwa
nguo hizo za ndani huchangia kwa kiwango kikubwa uwezekano wa mvaaji
kupata matatizo ya kiafya.
Utafiti uliofanywa na wataalamu mbalimbali wa nchini Uingereza,
unaonyesha kuwa uvaaji wa nguo hizo unaweza kumfanya mvaaji kupata
maradhi ya mgongo, saratani na kiwango kikubwa cha asidi mwilini.
Mmoja wa wataalamu wa afya katika Hospitali ya The London Clinic, Dk
Johnson Wilson, anasema kubana kwa nguo hizo katika eneo la tumbo huzuia
mzunguko wa asidi inayozalishwa ndani ya mwili na kuisababisha kupanda
juu, badala ya kushuka chini.
Anasema kuwa hali hiyo inatokana na msukomo unaotokea kwenye tumbo,
hivyo kusababisha mlundikano wa asidi ndani ya mwili ambayo hupaswa
kutoka baada ya kuzalishwa.
“Nguo hii inapovaliwa inatenganisha eneo la kifuani na tumbo, hivyo
asidi inayozalishwa inashindwa kushuka chini na matokeo yake inashia
kwenya usawa wa matiti na kurudi kwenye mrija unaopitisha
chakula,”anasema DkWilson.
Kuhusu hatari ya saratani, Dk Wilson anasema kuwa kulundikana kwa
asidi katika mrija wa chakula, kunamweka mhusika katika hatari ya kupata
saratani ya koo na kinywa.
Anasema kwamba licha ya kuwa siyo watu wengi walioathirika na uvaaji
wa nguo hizo, lakini matokea yake huonekana baada ya muda mrefu kutokana
muda ambao mhusika atavaa nguo hizo.
“Hatari ipo zaidi kwa wanaovaa nguo hizi mara kwa mara, madhara yake
hayawezi kuonekana kwa haraka zaidi, lakini kiafya kuna hatari ya
kutengeneza saratani ya koo kutokana na kuzuia asidi na kusababishia
irudi na kulundikana kwenye mrija unaosafirisha chakula,”anaonya.
Pamoja na hatari hiyo uvaaji wa nguo hizoi pia unachangia kusababisha
ugonjwa wa ngozi unaotokana na mwili kubanwa kupita kiasi, hivyo hewa
kushindwa kupita.
Dk Wilson anafafanua kuwa ikifikia hatua hiyo, kuna uwezekano wa
kutengeneza mazingira ya bakteria na fangasi kujificha kwenye mwili
hivyo kusababisha mvaaji kupata maradhi ya ngozi yaliyo magumu kutibika.
Mtaalamu wa ngozi Dk Sam Bunting anasema, kubanwa kwa ngozi pamoja na
joto linalosababishwa na msuguano, vinachangia kuleta madhara makubwa
katika mwili wa binadamu.
“Hali hii inasababisha ugonjwa unaofahamika kwa jina la kitaalamu
kama Intertirgo, ambao huwatokea watu wanaovaa nguo maalumu za kubana
kwa ajili ya kutengeneza maumbile,”anasema.
Nguo hizo pia huchangia kuifanya misuli ya tumbo kuwa dhaifu,
kutokana na kubanwa muda mwingi, hata inapoachwa huru inashindwa kuwa na
nguvu yake ya kawaida.
“Kwa asili misuli ya tumbo haina nguvu na unapoibana kwa muda mrefu
unaisababishia kushindwa kufanya kazi yake kwa ufanisi, hivyo hulegea na
kuwa dhaifu zaidi hata inapofunguliwa au kutolewa nguo
inayobana,”anasema.
Kwa upande mwingine, mtaalamu wa misuli Dk Robert Shanks anasema kuwa
nguo hizo zinachangia pia kusababisha maumivu ya mgongo kwa mvaaji.
Anasema nguo hiyo inapovaliwa, kunakuwapo na ugumu kwa viungo vya mgongo
kujongea kwa urahisi, hivyo kusababisha maumivu ya mgongo mara kwa
mara.
“Viungo na mifupa iliyopo kwenye mgongo inapaswa kujongea, lakini
kuibana kupita kiasi kutasababisha kushindikana kwa hali hiyo hivyo
mvaaji lazima atakumbana na maumivu ya mgongo mara kwa mara”
Pamoja na madhara hayo, nguo hizi pia huweza kusababisha kizuizi
katika mzunguko wa damu kwani mishipa inayotakiwa kufanyakazi hiyo
inashindwa, kutokana na maeneo ya tumbo hadi kwenye nyonga yanakuwa
yamebanwa.
“Ni vigumu mzunguko wa damu kufanyika vizuri katika maeneo
yaliyobanwa kupita kiasi; ni wazi kuwa nguo hizi siyo rafiki, huifanya
damu isizunguke inavyopaswa,”anasema Dk Shanks na kuongeza:
“Ikifikia hatua hiyo, kuna dalili mvaaji kuweza kupata maimivu ya
miguu kwa kuwa mishipa ya damu iliyopo katika maeneo hayo inashindwa
kufanya kazi yake vizuri.”
Kwa upande wake mtaalamu wa masuala ya ngozi nchini Tanzania, Dk
Isack Maro, anasema kuwa madhara yanayotokana na uvaaji huo siyo makubwa
ikilinganishwa na ripoti ya utafiti unavyoeleza.
“Inawezekana kukawapo uwezekeno wa kupata maradhi ya ngozi kutokana
na mwili kubanwa kwa muda mrefu, hivyo jasho kushindwa kutoka na
kutengeneza mazingira ya fangasi,”anasema Dk Maro na kuongeza:
“Madhara yapo, lakini siyo kwa ukubwa huo. Inawezekana kuwakumba watu
wachache mno kati ya wengi, lakini sidhani kama yanaweza kuwa kwa
ukubwa huo.”
No comments:
Post a Comment